* Asema suala la Tanzania kuwa na nishati ya uhakika si la kusubiri
* Taasisi ya Kimataifa ya Umeme Jua (ISA) yaonesha nia ya kuwekeza
*Kituo cha umahiri wa umeme jua kuzinduliwa Arusha Juni mwaka huu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Kuendeleza Nishati ya Jua (ISA), Dkt. Ajay Mathur yenye Makao Makuu yake nchini India ambaye ameeleza nia ya ISA kuwekeza katika miradi ya umeme jua nchini.
Mazungumzo kati ya Dkt. Biteko na Dkt. Mathur yamefanyika jijini New Delhi nchini India ambapo Dkt. Biteko alishiriki Wiki ya Nishati India ambayo ilienda sambamba na mikutano mbalimbali kuhusu nishati.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002512066.jpg)
“ Tunawaalika mje kuwekeza Tanzania kwani tunahitaji kuwa na miradi mingi ya umeme kutoka vyanzo tofauti ili kuweza kutosheleza mahitaji ya watu wetu na kinachotupa msukumo zaidi kwa sasa ni mpango mahsusi wa misheni 300 tuliousaini mwezi Januari 2025 ambapo Tanzania tunapaswa kupeleka umeme kwa wananchi milioni 8.3 ifikapo mwaka 2030.” amesema Biteko
Dkt. Biteko ameishukuru Taasisi ya ISA kwa kuona Tanzania kama sehemu sahihi ya uwekezaji na kueleza kuwa kazi yake ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na miradi mingi ya nishati ambayo italeta utoshelevu wa umeme na kuchagiza maendeleo huku akisisitiza kuwa suala la kuwa na umeme wa kutosha si la kusubiri miradi inapaswa kutekelezwa sasa.
Kuhusu miradi ya umeme Jua nchini, Dkt. Biteko amesema Tanzania imeanza kutekeleza mradi wa umeme jua wa megawati 150 wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kwa kuanza na megawati 50 ambapo megawati 100 zitaanza kutekelezwa baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002512063-1024x683.jpg)
Ameongeza kuwa, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pia limepata maeneo matatu kwa ajili ya miradi ya umeme jua ambayo ni Zuzu, Dodoma (MW 60), Mkwese, Manyoni – Singida (MW 199) na Same, Kilimanjaro (MW 50) ambapo ameishukuru ISA kwa kukubali kufanya upembuzi wa awali katika maeneo hayo.
Ili kuwezesha uwekezaji wa Taasisi hiyo nchini, Dkt. Biteko amewataka Watendaji hao kuainisha maeneo ambayo wanahitaji kuwekeza ili Wataalam waanze kuyafanyia kazi.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya ISA, Dkt. Ajay Mathur alimweleza Dkt.Biteko kuwa Taasisi hiyo inataka kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya umeme jua nchini huku msukumo wakiupata pia kutoka kwenye Mkutano wa Misheni 300 ambao ulieleza nia ya Afrika kufikisha umeme kwa watu milioni 300 Tanzania ikiwemo.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002512062-1024x683.jpg)
Amesema Taasisi ya ISA inafanya kazi kwenye nchi 122 duniani na inashirikiana na Serikali mbambali katika utekelezaji wa miradi ya umeme jua kwa njia mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo kwa wazawa kuhusu utengenezaji wa vifaa vya umeme jua, kusaidia serikali kutengeneza sera zinazowezesha uwekezaji katika nishati ya jua, kuwajengea uwezo wahandisi wa nishati ya jua na watunga sera za nishati katika maeneo mbalimbali yanayohusu uendelezaji wa Nishati ya Jua.
Katika hatua nyingine, Mathur amesema kuwa tayari Taasisi ya ISA imeanza kufanya kazi Tanzania kwa kuanzisha Kituo cha Uendelezaji wa Teknolojia ya Nishati ya Jua (Solar Technology Applications Resource Center – STAR-C) ambacho kitakuwa na majukumu mbalimbali ikiwemo uendelezaji wataalam wa ndani ya nchi na kufanya tafiti ambazo zitasaidia Utekelezaji wa miradi ya Nishati jua kwa kuzingatia Mazingira ya nchi yetu, kuandaa mitaala, kufanya ukarabati na ujenzi wa majengo ya maabara kwa ajili ya tafiti na kufundishia, ununuzi wa vifaa kwa ajili ya kufundishia na upimaji wa viwango vya ubora wa vifaa vya Umeme Jua.
Vilevile kituo hicho kitasaidia ubunifu wa bidhaa na huduma zinazohimiza matumizi ya nishati ya jua, pamoja na kusaidia biashara katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Ameongeza kuwa, kituo hicho ambacho kimejengwa katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kitazinduliwa mwezi Juni mwaka huu.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002512065-1024x683.jpg)
Kwa Afrika, ISA imeanzisha vituo vya STAR C nchini Uganda, Ethiopia, Somalia, Ivory Coast na Ghana ambapo tangu kuanzishwa kwake vituo hivyo vimefundisha maelfu ya wataalam katika sekta ya nishati ya jua.
Mazungumzo kati ya Dkt. Biteko na Dkt. Mathur yalihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga.