DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Wiki iliyopita wahariri, wamiliki wa vyombo vya habari na waandishi waandamizi walikutana na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Ashatu Kijaji, katika kikao maalumu cha kufahamiana.

Mambo kadhaa yalijadiliwa kuhusu wizara hiyo, miezi michache baada ya Idara ya Habari kuondolewa kwenye iliyokuwa Wizara ya Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, kufuatia ombi la Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile, kwa Rais Samia Suluhu Hassan, alilolitoa Juni 28, 2021.

Dk. Ashatu ameahidi kuyashughulikia yote yanayohusu sekta na tasnia ya habari aliyoyakuta mezani kwake na anayopelekewa sasa, majibu yaliyotoa faraja kwa wadau wa sekta hiyo nchini.

“Ndugu wahariri, lengo la mkutano huu ni kujitambulisha kwenu baada ya kuteuliwa. Hili ni jambo muhimu hasa baada ya Rais kuamua tasnia ya Habari isimamiwe na wizara yangu na kuunda wizara mpya; yaani Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Kwa hiyo ndugu wahariri, ninaomba ushirikiano katika kukuza hii tasnia,” anasema waziri.

Anasema ushirikiano kati ya wadau na wizara ni sehemu ya kutimiza matakwa ya Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayotamka kuwa kila mtu yuko huru kutoa maoni na mawazo yake, kutafuta, kupokea na kutoa habari kupitia chombo chochote bila kujali mipaka ya nchi.

Dk. Ashatu amevishukuru vyombo vya habari kwa kuendelea kuelimisha na kutoa ushirikiano katika changamoto ya UVIKO-19, akiwataka waendelee kutoa elimu kwa jamii ili iweze kuchukua uamuzi sahihi wa kuchanjwa na kujikinga na madhara ya janga hilo.

“Pamoja na juhudi kubwa mnayoifanya, ninaendelea kuwaomba ushirikiano ili tuweze kuiendeleza sekta ya habari na kutangaza masuala muhimu na mazuri yanayofanyika nchini, ikiwa ni pamoja na miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali, wadau wa maendelo na wananchi kwa ujumla,” anasema Dk. Ashatu.

Katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru, waziri anasema upo umuhimu wa vyombo vya habari kuelezea nchi ilikotoka, ilipo na inapokwenda pamoja na mambo mbalimbali yaliyofanyika tangu uhuru ulipopatikana Desemba 9, 1961.

Anasema Watanzania wote hawana budi kujivunia miaka 60 ya Uhuru wakiwa na amani na maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwamo tasnia ya habari.

“Naomba nitumie fursa hii kuwaomba wanatasnia ya habari kushiriki kikamilifu katika kutangaza shughuli zote zinazohusu Uhuru wetu kama sehemu muhimu ya kutoa elimu kwa Watanzania na dunia kwa ujumla. Umoja wetu katika jambo hili utasaidia sana kuelimisha wananchi,” anasema.

Akijibu swali lililoibuliwa na wahariri kuhusu maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, Dk. Ashatu anasema maagizo yote yaliyotolewa kuhusu kufunguliwa kwa vyombo kadhaa vya habari, wizara inayafanyia kazi na atahakikisha ufumbuzi unapatikana haraka.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Zainabu Chaula, amevitaka vyombo vya habari kufanya kazi kwa weledi na kwa kufuata sheria, kwani kwa kufanya hivyo tasnia itakua na kuwa na wataalamu zaidi.

“Waandishi wa habari, tukifanya kazi kwa weledi hakuna kuvutana na fujo haziwezi kutokea, tukifanya kazi zinazotuhusu hakuna vurugu yoyote, kwa hiyo tufanye kazi kwa kufuata sheria na kutumia taarifa vizuri ili kutoa taarifa za kuaminika,” anasema Dk. Zainabu.