Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
JESHI la Polisi Mkoani Pwani,
limewakamata Diwani wa kata ya Kiromo Mstaafu Hassan Wembe na Askari Mgambo Abdallah Mgeni na baadae kupewa dhamana, kwa kosa la kumshambulia kwa maneno makali, vitisho, dharau na kutishiwa kufungwa pingu Waziri na Mbunge Mstaafu Dkt Shukuru Kawambwa pamoja na Cathbert Enock Madondola huko Kitopeni, wilayani Bagamoyo.
Aidha watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Pwani, Pius Lutumo, alieleza, tarehe 25 april mwaka huu kupitia mitandao ya kijamii ilionekana clip ikimwonesha dkt Kawambwa akishambuliwa kwa maneno na vitisho na kudhalilisha , kufokewa na kutishiwa kufungwa pingu kama mhalifu hali iliyosababisha taharuki kubwa kwa jamii.
“Ukweli ni kuwa April 24 saa 8 mchana dkt Kawambwa na mtu mwingine Cathbert Madondola walishambuliwa kwa maneno, vitisho na kutishiwa kufungwa pingu na diwani Mstaafu kata ya Kiromo Hassan Wembe akiwa na askari mgambo Abdallah Mgeni.”alifafanua Lutumo .
Vilevile Kamanda huyo, amemtaka mtu aliyechukua na kusambaza video ya dkt Kawambwa na Cathbert Madondola wakishambuliwa kwa maneno makali na kutishiwa kufungwa pingu na diwani Mstaafu huyo Wembe ajisalimishe kituo cha polisi Bagamoyo mara moja.
“Katika clip iliyokuwa inasambaa mitandaoni iliambatana na maneno yaliyosomeka kuwa Shukuru Kawambwa Waziri wa Miundombinu enzi hizo sasa ni dalali wa viwanja Bagamoyo na mhalifu wa kawaida (common criminal) jambo hili linachunguzwa pia kubaini ukweli” alisema Lutumo.
Alitaja chanzo cha tukio hilo ni magari ya mchanga ya mtuhumiwa Hassan Wembe kuharibu barabara na mashamba ya watu yakipita kwenda kubeba mchanga eneo hilo hali iliyopelekea wananchi kufunga barabara kwa magogo ili kuzuia uharibifu wa barabara.
Lutumo aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, bali wafuate sheria za nchi na kuwatumia viongozi waliopo kwenye maeneo yao kutatua matatizo yao.
Wakati huo huo Dkt Shukuru Kawambwa amesikitishwa na kitendo alichofanyiwa na dwn Mstaafu, Hassan Wembe kwa kumkashifu kuwa ni dalali wa viwanja wakati katika eneo hilo walikuwa wameziba njia na hakukuwa na kesi ya kuuza au kufanya udalali wa viwanja.
“Mimi sijawahi kwenda shamba lolote,kufanya lolote, Wembe kanidhalilisha,na naamini vyombo vya kisheria vitachukua hatua”
Alitoa ufafanuzi kwamba, walikaa katika kikao cha wananchi wa eneo hilo na kuamua kwa asilimia 100 barabara ifungwe isitumike tena kwani wanaharibu miundombinu ya barabara.
“Na mvua zikimalizika atengeneze barabara pia achepushe njia nyingine kupitia eneo lake kwenda barabara kuu ili afanye kazi zake kwa Uhuru kuliko kukera wananchi” alisema Dkt.Kawambwa.