Na Lookman Miraji
Diwani wa Kata ya Kisarawe 2, iliyoko katika Wilaya ya Kigamboni, Issa Hemed ameuzindua rasmi msimu wa nne wa mbio za hisani zijulikanazo kama Mbio za Jerusalem.
Mbio hizo ambazo hufanyika kila mwaka chini ya uratibu wa asasi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na malezi ya watoto ijulikanayo kama Jerusalem (Jerusalem Children Home Organization.)
Asasi hiyo isiyo ya kiserikali imekuwa ikiandaa mara kwa mara mbio hizo hasa zikiwa na lengo la kuchangia mahitaji muhimu kwa watoto yatima na wenye uhitaji. Kwa miaka ya hivi karibuni asasi hiyo imekuwa ikisimama mstari wa mbele katika kusaidia watoto waishio katika mazingira duni katika jamii ya kitanzania.

Kupitia asasi hiyo yenye kituo chake binafsi cha kulea watoto kilichopo maeneo ya Kibada wilayani Kigamboni mpaka sasa jumla ya watoto 32 ambao wamekuwa wakilelewa katika kituo hicho.
Kupitia asasi hiyo ya Jerusalem imekuwa ikitoa na kufanikisha mahitaji yote muhimu kwa watoto wote ambao wanaishi na kukuwa chini ya uangalizi wa kituo hicho.
Kwa mara kadhaa tukio la mbio za Jerusalem zimekuwa zikifanyika kila mwaka zikiwa na lengo la kusaidia watoto wadogo wenye uhitaji.
Katika misimu kadhaa iliyotangulia mbio hizo zimepelekea kupatikana kwa mafanikio kadhaa yaliyopatikana na kusaidia kukuwa kwa kituo hicho na kupelekea kuongezaka kwa idadi ya watoto wanaopatiwa msaada wa kimalezi na kituo hicho.

Mojawapo ya mafanikio muhimu yaliyofikiwa na kituo hicho kwa miaka ya hivi karibuni ni uwekezaji mwingine unaofanywa na asasi hiyo katika maeneo ya Mwasonga wilayani Kigamboni ambapo jumla ya mita za mraba elfu 8 zimenunuliwa na asasi ya Jerusalem huku hatua za mwanzo za ujenzi wa kituo kikubwa cha kulelea watoto pamoja ujenzi wa vituo vya huduma muhimu za afya na elimu zikiendelea.
Akizungumza wakati uzinduzi wa msimu wa nne wa mbio hizo za Jerusalem zilizofanyika katika mradi unaoendelea na ujenzi, maeneo ya Mwasonga katika kata ya Kisarawe, Diwani wa kata hiyo, Issa Hemed ameishukuru asasi ya Jerusalem kwa hatua muhimu inazochukua kukabiliana na changamoto ya malezi katika jamii.
Diwani huyo mbali pongezi hizo alizotoa kwenda kwa asasi ya Jerusalem pia ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa katika kufanikisha ujenzi wa vituo vya afya na elimu unaosimamiwa na asasi ya Jerusalem.

Bi Upendo Ngoda ambae ndiye muanzilishi na mkurugenzi wa asasi hiyo ameelezea matumaini na malengo ya taasisi hiyo kuwa Ina malengo kutoa msaada wa kimalezi kwa watoto 100.
“Kupitia kituo hichi tunachokijenga tutaweza kufikia idadi ya watoto 100 ambao watakuwa wakilelewa na kupatiwa mahitaji yote muhimu. Na hilo limekuwa lengo letu tangu mwanzo tulipoanza.”
Aidha Bi: Upendo ameongeza kuwa kupitia mpango ujao wa mbeleni utakaohusisha ujenzi wa hospitali shule utaweza kusaidia kuleta unafuu kwa makundi mbali mbali ya watoto na wazee juu ya kupata huduma za afya.
Akiongeza nae, Isaya Lyimo ambae ni mwenyekiti wa mbio za Jerusalem and kwa mwaka huu amesema kuwa mbio hizo kwa mwaka huu zimelenga kuwafikia wakimbiaji zaidi ya elfu mbili.
Mbio za Jerusalem msimu wake wa nne kwa mwaka huu zinatarajiwa kufanyika Julai 19, 2025, katika Eneo la Kibada wilayani Kigamboni.