Diwani wa Kata ya Kijichi, Anderson Chale, analalamikiwa na wananchi wa mtaa wa Mbagala Kuu, Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam kwa kuvamia eneo la barabara na kujenga jingo.
Wananchi hao wanasema kutokana na uvamizi huo uliofanywa kwa makusudi na Diwani Chale, barabara waliyokuwa wakiitumia kwa kipindi kirefu kwa ajili ya kupita vyombo vya usafiri imefungwa na hivyo kuwaletea usumbufu mkubwa wakazi wa mtaa huo.
Wanasema, Chale, kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alijenga uzio wa kwanza zaidi ya miaka saba iliyopita ambao uliwapa fursa ya kupitisha vyombo vya usafiri, uzio uliojengwa kwa taratibu zinazokubalika kisheria.
“Kutokana na vitendo vya ubabe, Aprili 30 mwaka huu aliamua kujenga uzio wa pili nje ya ule wa kwanza na kuziba kabisa njia tuliyokuwa tukiitumia kwa shughuli mbalimbali za kijamii,” anaeleza mkazi mmoja wa mtaa huo.
“Mbali na kuziba njia hiyo, ameharibu miundombinu ya maji na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi, na viongozi tufiwakishia malalamiko yetu wanamwogopa,” anasema.
Hata hivyo, wameieleza JAMHURI kwamba kutokana na cheo chake hicho cha kisiasa amekuwa akitumia madaraka yake vibaya kwa kuwaeleza: “Yeye ni diwani wa CCM kwa miaka 15, hivyo wananchi hao hawawezi kufanya lolote kwake na iwapo wataendelea kumfuatilia wote atawaweka ndani.”
Kutokana na vitisho hivyo alivyovitoa kwa wananchi wa mtaa huo, wanasema waliamua kulifikisha suala hilo kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbagala Kuu, Fabian Chilumba, wakashauriwa waende Baraza la Ardhi.
Wanasema walipofikisha malalamiko yao Baraza la Usuluhishi Kata ya Mbagala Kuu ambalo Mei 6 mwaka huu lilitoa amri kwa Chale kusimamisha ujenzi (stop order) eneo hilo la barabara, iliyopewa kumbukumbu namba BUK/MBK/SO/5/2015, lakini pamoja na amri hiyo aliendelea na shughuli za ujenzi.
Baada ya kukaidi amri hiyo ya kwanza alipewa nyingine Mei 14 mwaka huu ikiwa na kumbukumbu Na. BUK/MBK/SO/6/2015.
“Unatakiwa kuanzia siku hii ya leo ya (tarehe 14/5/2015) usiendelee na ujenzi mpaka matatizo yahusuyo sehemu hii yatakapotatuliwa kisheria,” ilieleza sehemu ya amri hiyo iliyotolewa na Baraza la Kata hiyo.
Wanasema pamoja na amri hiyo iliyotolewa mara ya pili, Chale aliendelea na shughuli za ujenzi kwenye eneo hilo na kuharibu mindombinu ya maji na kuwaletea usumbufu wakazi wa eneo hilo.
Pamoja na hayo, wanaeleza kwamba woga wa baadhi ya viongozi wa mtaa huo umesababisha kuendelea kumfanya akaidi amri hizo za kusitisha ujenzi na kuvunja uzio uliokuwapo awali kwa lengo la kupoteza ushahidi.
Japo Chale hakupatikana kutolea ufafanuzi suala hilo, lakini Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbagala Kuu, Chilumba, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo lakini alikataa kulielezea kwa madai kwamba suala hilo linashughulikiwa kisheria.
Licha ya kiongozi huyo kuvamia eneo la barabara na kujenga, imeelezwa kuwa jiji la Dar es Salaam ndilo lenye maeneo mengi yanayovamiwa na kubadilishwa matumizi yake kutokana na vitendo vya rushwa vilivyokithiri kwa maofisa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, halmashauri za majiji, miji na manispaa.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, zaidi ya viwanja 100 vya wazi vimevamiwa jijini Dar es Salaam na kuwataka wavamizi hao kubomoa majengo yao na kuyarejesha maeneo hayo.
Lakini hadi sasa wavamizi wa maeneo hayo ya wazi, kwa kutumia jeuri ya fedha waliyonayo ama urafiki wao na baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali, wamekaidi agizo hilo lililotolewa na wizara hiyo.
Januari mwaka huu, wizara hiyo ilisimamia ubomoaji wa jengo la mgahawa lililojengwa kinyume cha sheria ndani ya eneo la wazi la bustani ya Samora na Kampuni ya Easy Payment Limited.
Hatua hiyo ilikuja baada ya gazeti JAMHURI kuandika habari ya uchunguzi kuhusu viongozi wa Jiji la Dar es Salaam ‘kuuza’ eneo hilo la wazi kwa kampuni hiyo. Jengo hilo lilikuwa likijengwa bila vibali vya ujenzi nyakati za usiku na siku za mapumziko.
Sheria ziko wazi ikiwamo Sheria Na. 8 ya Mipangomiji ya mwaka 2007 ambayo imefafanua kwamba maeneo yote ya wazi ni kwa ajili ya matumizi ya umma, na suala la kujenga majengo ya biashara au makazi ndani ya maeneo hayo haliruhusiwi.
Pia gazeti hili liliwahi kuripoti habari iliyoihusu Manispaa ya Kinondoni kuruhusu mmliki wa Shule ya Saint Florence iliyopo Mikocheni ‘B’ kujenga jengo la shule eneo la barabara na kuziba kabisa njia hiyo iliyokuwa ikitumika kwa muda mrefu na wakazi wa eneo hilo.
Malalamiko ya wakazi hao yameshafikishwa Wizara ya Ardhi, na Manispaa hiyo, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na wahusika hao licha ya kuthibitisha kufungwa kwa barabara hiyo na jengo kujengwa hapo.
Baadhi ya wakazi wa jiji hili wameiomba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kubomoa nyumba zote zilizojengwa katika maeneo ya barabara na viwanja vya wazi, badala ya kuweka nguvu kubwa kwa wananchi wanyonge na maskini waishio katika maeneo ya mabondeni.
Wanasema kama kazi hiyo itaendelea kufanyika kwa kuwaogopa baadhi ya matajiri na viongozi, inaweza kuitia doa kubwa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imejenga imani kubwa kwa wananchi kwa muda mfupi tangu ilipoingia madarakani.