Diwani wa kata ya Kisaka wilayani Serengeti, Chacha Togoche, ‘amewangukia’ wezi akiwaomba kutorudia kuiba sola katika zahanati ya kijiji cha Nyiboko.
Togoche ametoa wito huo wakati akikabidhiwa sola mpya jijini Dar es Salaam juzi, iliyonunuliwa kwa fedha zilizochangwa na rafiki zake wa jijini hapa ili kurejesha huduma zilizosimama katika zahanati hiyo baada ya iliyokuwepo kuibwa.
Amepokea sola hiyo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya FM Solar Energy, Fredrick Maro, ambaye amejitolea kuisafirisha kutoka Dar es Salaam na kwenda kuifunga katika zahanati hiyo bila malipo.
“Ninashukuru wadau wote waliochanga Sh 400,000 kugharimia sola hii, lakini kikubwa ninawaomba wezi husika popote walipo wasirudie kuiba hii na kukwamisha tena huduma katika zahanati ya Nyiboko,” amesema Togoche.
Kwa mujibu wa diwani huyo, wizi wa sola iliyokuwepo umesababisha kusekana kwa friji na umeme wa uhakika katika zahanati hiyo inayohudumia wanakijiji zaidi ya 3,000.
Ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wakazi wa kata hiyo na wadau wengine kujitolea kuchangia uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii katani humo.
Kwa upande wake, Maro amesema amelazimika kuuza sola hiyo kwa Sh 400,000 badala ya Sh 550,000 lakini pia kugharimia usafirishaji na ufungaji wake kutokana na kuguswa na maendeleo ya kata hiyo ukiwamo uboreshaji wa zahanati hiyo.
Diwani huyo amefuatana na Mwenyekiti wa kuhamasisha maendeleo ya kata hiyo, Butoto Mwita na mdau mwingine, Maneno Masiana, wakati wa kukabidhiwa sola hiyo.