Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini(HESLB), imetangaza kufunguliwa dirisha la kuomba mkopo kwa wanafunzi wa mwaka wa masomo 2024/2025 huku waombaji wametakiwa kusoma mwongozo kabla ya kuomba.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 6, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji WA HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kuzindua miongozo Mei 27, 2024 waliiweka miongozo hiyo kwenye tovuti ya Bodi ya Mkopo ambayo Www.heslb.go tz.
“Kwa mwaka wa masomo 2024/2025 dirisha la kuomba mkopo kwa njia ya mtandao lipo wazi kwa siku 90 kuanzia Juni 1 hadi Agosti 31, 2024,” amesema Dkt. Kiwia.
Hata hivyo, Dkt. Kiwia amesema muda wa siku tisini unatosha kwa waombaji na wanatakiwa kuandaa nyaraka muhimu, na itachukua dakika 40 kukamilisha maombi yake kwa njia ya Mtandao.
“Tunasisitiza waombaji kuzingatia muda uliotolewa kwa kuwa hatutarajii kuongezwa baada ya Agosti 31, 2024,” amesema.
Amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imetenga Sh. Bilioni 787 kwa ajili ya mikopo na ruzuku kwa jumla ya wanafunzi 250,000 ambapo idadi hiyo imeongezeka kutoka wanafunzi 224,056 mwaka 2023/2024 ambapo ni ongezeko la jumla wanafunzi 25,944.