Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imetaja changamoto saba za mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji nchini.

Imetaja changamoto hizo ni pamoja na gharama kubwa katika mchakato wa uwekezaji zikiwamo kodi na tozo na muda wa kuanza biashara.

Nyingine ni muda mrefu wa kukamilisha taratibu za awali za uidhinishaji wa biashara na uwekezaji, urasimu usiokuwa na tija, udhibiti uliokithiri hususani katika kudhibiti kodi na mapato kwa bidhaa zenye thamani kubwa na migongano ya sera, sheria, kanuni na majukumu ya taasisi za udhibiti.

Rasimu imetaja changamoto nyingine ni wafanyabiashara kukabiliwa na mzigo wa kodi, ada na ongezeko la gharama kutokana na mahitaji mengi ya leseni, vyeti na vibali, vinavyochangiwa na vyombo vya udhibiti vilivyopewa jukumu la kukusanya mapato.

Rasimu ilieleza kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo zinahitajika juhudi za ziada katika kuimarisha mazingira ya biashara na kukuza uchumi na uwekezaji.

Makamu wa Dk Philip Isdor Mpango, akionesha kitabu cha Muongozo wa Mchakato wa Maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, baada ya kuzindua mchakato huo , akishudiwa na Waziri wa Fedha na Mipango,Dk Mwigulu Lameck Nchemba (katikati), na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Natu El-Maamry Mwamba jijini Dodoma Aprili 2023(Picha na Wizara ya Fedha).

Rasimu inatarajia kuwa ifikapo 2050 katika mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji Tanzania itakuwa nchi inayoongoza kwa kuvu tia uwekezaji ikiwa ni kati ya nchi tatu bora Afrika zenye wepesi wa kufanya biashara na uwekezaji.

Pia inatarajia nchi itakuwa na sera endelevu na zinazotabirika ili kuweka mazingira bora ya uwekezaji yanayovutia kampuni za ndani na nje pamoja na kuwa na uchumi mpana unaotokana na ongezeko, ukuaji na uendeleaji wa wajasiriamali wadogo na wa kati pamoja na kampuni kubwa shindani za kimataifa.

Rasimu inatarajia kutakuwa na mfumo jumuishi, unaobadilika na kuchangia ukuaji endelevu wa biashara, kutoa motisha ili kuzalisha ajira, kuwa na jamii yenye utamaduni wa kuweka akiba, kuwekeza ili kutengeneza utajiri na kuwa na maisha bora.

Sekta binafsi imara Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 inaeleza kuwa na sekta binafsi yenye nguvu na inayowajibika ni injini ya uchumi imara na endelevu.

Inaeleza kuwa Tanzania imefanya jitihada za kushirikisha, kukuza ushiriki wa sekta binafsi, ikiwa ni pamoja na majadiliano ya sekta ya umma na binafsi, kuanzishwa kwa mfumo na sera ya ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi.

Pia, diplomasia ya kiuchumi imekuwa ni kipengele muhimu katika sera ya mambo ya nje pamoja na mipango kadhaa ya ujumuishaji wa kifedha imetekelezwa ili kuongeza upatikanaji wa mtaji wa kifedha.

Rasimu inabainisha kuwa kumekuwa na jitihada za kuandaa sera ya taifa inayohimiza matumizi ya rasilimali za ndani katika miradi ya maendeleo kama njia mbadala ya ushiriki mdogo wa kampuni za ndani katika miradi ya uchumi kwa sababu mafanikio ya sera hii yatategemea ufanisi katika utekelezaji na usimamizi.

Matarajio ya rasimu katika sekta binafsi imara ni kuwa na huduma ya umma inayolenga sekta binafsi ili kukuza mazingira wezeshi ambayo biashara binafsi zinaweza kustawi na kuchangia kwa ufanisi katika maendeleo ya kiuchumi.

Pia, kuwa na sekta binafsi yenye ushindani, imara na jumuishi ambayo inaongoza maendeleo ya kijamii, kiuchumi na sekta inayoweza kushindana katika soko la kimataifa kwa kutumia nafasi iliyo nayo katika mnyororo wa thamani
kimataifa.

Aidha, matarajio mengine ni kupungua kwa kiasi kikubwa cha idadi ya sekta zisizo rasmi katika uchumi. Kutokana na sababu hizo, rasimu inaelekeza uwepo wa mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji ili kuwa na uchumi imara na endelevu nchini.

Hivyo inataka kupitiwa upya kwa sheria na kanuni, kupunguza na kuondoa ada na kodi na kuoanisha majukumu ya vyombo vya udhibiti. Aidha, inaeleza kuwa mipango hiyo inalenga kuimarisha ufanisi wa mifumo ya sheria, kurahisisha utawala na udhibiti wa biashara na kuongeza uwazi katika michakato ya udhibiti.