Viongozi wa dini nchini wamekubalina kutoa tafsiri ya kuchinja kwa waumini wao, kuondoa upotoshaji na kurejesha uelewano baina yao.
Makubaliano hayo yamo katika tamko la pamoja lililotolewa katika kikao cha majadiliano cha viongozi wa dini mkoani Dar es Salaam, wiki iliyopita.
Mkuu wa mkoa huo, Saidi Meck Sadiki, amewambia waandishi wa habari kuwa viongozi hao wataandaliwa utaratibu wa kuzungumza kupitia vyombo vya habari kuhusu dini na imani zao.
“Viongozi wa dini waendelee kufanya kazi yao ya kuelimisha waumini, na hasa vijana juu ya umhimu wa kulinda amani tuliyonayo na kuishi kwa kushirikiana baina ya waumini wa dini zote,” amesema.
Amesema viongozi na waumini wa dini ndiyo wenye dhamana ya kuhahikisha amani na utulivu vinadumu katika mkoa wa Dar es Salaam na Tanzania kwa jumla.
Katika tamko hilo, wamekubaliana kutoa elimu ya Katiba na sheria za nchi kwa viongozi wa dini kuhusu uhuru wa imani, kuabudu, kueneza, kuhubiri dini na kuendesha shughuli za dini.
Ameongeza kuwa wamekubalina pia kutumia sheria kuwabana wote wanaotoa kauli za uchochezi na kuvuruga amani na utulivu nchini.
Amesema viongozi hao walikubalina kuimarisha elimu ya dini shuleni ili kujenga misingi imara ya kuvumilina na kuheshimiana kwa misingi ya imani tofauti za dini zao.
Ameyataja makubaliano mengine kuwa ni mihadahara ya dini kufanyika bila kuathiri uhuru wa kuabudu wa watu wengine na kufanyika katika mazingira ambayo hayatawakera wala kuwabugudhi watu wengine.