Mafuriko ni wingi wa maji uliopitiliza, wingi huo wa maji hutokana na nguvu za asili. Hakuna mwanadamu awezaye kuyatengeneza mafuriko kama ilivyo vigumu kwa kuyazuia, hakuna awezaye kuyazuia mafuriko. Hiyo ni nguvu ya asili. Pamoja na ujanja wote wa binadamu bado hajaweza kuizuia nguvu ya asili.
Bwawa la maji hata liwe na ukubwa wa aina gani, kama bwawa lenyewe ni la kutengenezwa na binadamu ambalo Waingereza wanasema “man made”, wingi wa maji yake hauwezi kuitwa mafuriko hata kama bwawa lenyewe lina ukubwa kama ilivyo nchi ya Tanzania, bado litaitwa bwawa tu.
Nimetoa maelezo hayo kufuatia neno linalotumika kisiasa hapa nchini kwa wakati huu. Neno mafuriko lilitamkwa kwenye siasa kwa mara ya kwanza na mgombea urais kupitia Chadema kwenye muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Ngoyai Lowassa, alipokuwa akielezea wingi wa watu wanaompenda agombee urais wakati huo akiwa bado yuko kwenye chama chake cha zamani cha CCM.
Kutokana na watu kumpenda wakimualika ahudhurie kwenye sehemu mbalimbali zenye mikusanyiko ya watu, yalianza kutoka madai kwenye chama chake kwamba anaanza kampeni za urais kabla ya wakati. Ilifikia kipindi akapewa adhabu ya zaidi ya mwaka mmoja ndani ya chama chake ya kutotakiwa kujihusisha na masuala ya kampeni.
Baadaye ndipo yeye akasema kwamba watu wengi wanaomwendea ni sawa na mafuriko, na kwamba yeye hakuwa na uwezo wa kuyazuia mafuriko hayo. Aliufananisha wingi huo wa watu, waliokuwa wanamwendea bila yeye kuwaita, sawa na mafuriko ambayo hutokea bila watu kuyaita lakini wakiwa hawana namna ya kuyazuia.
Tangia hapo wingi wa watu, hasa kwenye mikutano ya kisiasa, umegeuzwa jina na kuitwa mafuriko.
Baada ya Lowassa kufanyiwa mizengwe kwenye chama chake huku baadhi ya watu ndani ya chama hicho wakidai kwamba wameweza kuyazuia maji ya mafuriko kwa mikono, ndipo mafuriko yakaonyesha nguvu zake za asili za kwamba hakuna binadamu awezaye kuyazuia.
Ndipo Lowassa akakaribishwa kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kupitia katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo ili akaendelee na kile ambacho wananchi wanamtaka akifanye, kugombea urais wa nchi hii. Waliodhani wamemuweza kwa mizengwe ndani ya CCM kwa sasa wanahaha kwa njia mbalimbali kuyazuia mafuriko kwa mikono!
Jinsi Lowassa alivyopokewa ndani ya umoja huo na mambo mengine yaliyofuatia, ikiwa ni kupewa kadi ndani ya Chadema, kuteuliwa kuwa mgombea wa umoja huo kupitia chama hicho, kwenda kuchukua fomu za kugombea urais kupitia chama chake hicho kipya, kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuchukua fomu za kugombea urais, ilijidhihirisha wazi kuwa kweli mafuriko hayazuiwi kwa mikono.
Umati wa watu waliojitokeza kumsindikiza uliwatia kiwewe wapinzani wake hasa wale waliomfanyia mizengwe ndani ya chama chake cha zamani cha CCM. Kwahiyo katika kujibu mapigo hayo zikaanza kufanyika mbinu za kila aina, ama ziwe za kujaribu kuyapunguza kasi mafuriko hayo au kuyafanya yaonekane yako kwingine pia na hivyo kuyafanya mafuriko halisi ya Lowassa yaache kuonekana ni ya kutisha zaidi na yasiyo ya kawaida.
Kwahiyo wakati CCM kinazindua kampeni zake katika viwanja vya Jangwani zilifanyika jitihada za kila aina kuhakikisha watu wanakuwa wengi kwenye mkutano huo wa uzinduzi kusudi ionekane kwamba kinachofanyika kwa Lowassa hata na kwa upande wa CCM nako kipo.
Kwahiyo CCM, sijui kama ni kwa kutumia pesa au umaarufu wake unaotokana na mamlaka kiliyo nayo, kikaandaa magari ya kusomba watu kutoka kila kona ya Jiji la Dar es salaam na viunga vyake na hata nje ya hapo. Mabasi ya UDA na daladala yalikuwa yanalandalanda kila mahali huku yakitolewa matangazo ya kwamba kila anayetaka kwenda Jangwani kwenye mkuatno wa CCM usafiri ulikuwa ni wa bure na upo! Ilifikia kiwango cha magari hayo kuonekana yanagonga hodi kila mlango wa nyumba!
Mbali na usafiri huo nilishuhudia watu wakipewa sare za CCM na kofia za kapero ikiwa ni pamoja na khanga nyepesi kwa kina mama. Waliotaka kwenda walipanda usafiri huo wa bure kwenda zao Jangwani huku ikidaiwa kuwa hata posho zilitolewa!
Kule vilikuwa vimeandaliwa vitu mbalimbali vya kuwavutia watu, zilikuwepo burdani za kila aina wakiwemo wasanii wa muziki unaoitwa wa kizazi kipya, wasanii ambao watu wengi hasa vijana wanavutiwa nao kwa kiasi kikubwa. Kwahiyo watu wengi walikwenda kule kwa kuvutiwa na watu hao kiasi kwamba baadhi ya watu walioenda kule walikuwa wakisema kwamba huo haukuwa mkutano ila ilikuwa ni “fiesta”, tamasha la kisanii linalofanywa na vijana.
Ila kwa wengine ambao wamekamia kujilinganisha na Lowassa wanadai kwamba hayo nayo yalikuwa mafuriko! Ndipo ninapowambia kwamba haijawahi kutokea mafuriko yakatengenezwa, mafuriko yanatokea tu kwa nguvu za asili. Sana sana ninachoweza kukubaliana nacho ni kwamba CCM walijitahidi kutengeneza maji ya kugema, wala hayo hayaitwi mafuriko.
CCM katika kuhakikisha wanapimana ubavu na nguvu za asili waliweka viti katika uwanja wa Jangwani ulipofanyika mkutano ili kuonyesha kwamba sehemu kubwa ilikuwa imekaliwa na watu, lakini katika mkusanyiko wowote wa Lowassa hakuna sehemu inayoweza kuwekwa viti na bado watu wakapata mahali pa kuenea. Hiyo ndiyo tofauti ya nguvu za watu na nguvu za asili.
Uzinduzi wa kampeni za Ukawa, Jumamosi ya Agosti 29, 2015, umethibitisha kila kitu. Kwa mtazamo wa harakaharaka watu waliokuwepo kwenye uzinduzi huo ni zaidi ya mara nne ya wale waliokuwa kwenye uzinduzi wa kampeni za CCM. Hakuna usafiri wa bure, nguo za bure wala posho vilivyotolewa! Hayo ndiyo tunayoweza kuyaita mafuriko. Yamekuja yenyewe kwa nguvu za asili.
Kuna usemi wa zamani wa Kingereza wa kwamba unaweza kumlazimisha punda au farasi kwenda kisimani lakini ni vigumu kumlazimisha kunywa maji. Hicho ndicho kilichotokea siku ya uzinduzi wa kampeni za CCM, watu wengi hasa vijana, walikwenda Jangwani siku hiyo kwa ajili ya kuwaangalia wasanii kama vile Diamond Platnumz, Msechu na wengine, wasanii hao walipomaliza kutumbuiza vijana, kwa wingi, wakaanza kutafuta nafasi ya kujiondokea bila hata kusubiri usafiri wa bure uliokuwa umepangiwa kwamba ungeanza kuwasomba watu kurudi makwao baada ya mkutano kuisha.
Tunawezaje kuilinganisha hali hiyo na mikusanyiko ya Lowassa ambayo haina vinywaji baridi, usafiri wa bure wala posho? Watu wanakwenda kwenye mikusanyiko ya Lowassa yeye akiwa ndiye kila kitu. Kwahiyo wa kwenda kwa miguu haya, wa bodaboda twende, wa kupanda daladala ndiyo kwao nakadhalika. Ni nguvu za asili tu, hayo ndiyo tunayoweza kuyaita mafuriko. Yanakuja bila kuwepo mtu yeyote wa kuyaratibu.
Jambo linaloonyesha kuwa haya ni ya kweli ni kitendo cha mamlaka husika kuanza mizengwe ya kuikataza Ukawa kuutumia uwanja wa Jangwani kwa madai yasiyoeleweka. Inaeleweka kwamba hayo ni maelekezo kutoka juu yanayotokana na kiwewe kilichowapata wahusika.
Lakini hata hivyo sikuelewa ni kwa nini Ukawa wameamua kuung’ang’ania uwanja huo wa Jangwani, sababu kwa vile kinachofanyika kwa Ukawa kinatokana na nguvu za asili sio haikuwa lazima wakatumia uwanja huo ambao kimwonekano ni mdogo kiasi cha kuwafanya watu wengine wakae kwenye barabara ya Morogoro wakati wa mkutano, uwanja huo ulikuwa unawafaa tu watu wanaokusanywa kwa kubembelezwa. Lakini kwa watu wanaokuja kwa hiari yao na kwa mapenzi yao ulikuwa ni mdogo mno.
Mimi nadhani hata kama ingesemwa kwamba mkutano wa uzinduzi wa Ukawa unafanyika katika eneo la wazi kati ya Mlandizi na Chalinze watu wangekwenda kwa wingi tu, na kule ndiko kungewafaa zaidi Ukawa.