Wakati sakata la Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla la matumizi mabaya ya madaraka likiendelea kushika kasi, msanii Abdul Nassib (Diamond) ‘amemkaanga’ waziri huyo kupitia kwa meneja wake, Hamisi Taletale (Babu Tale).

Taletale amezungumza na JAMHURI na kuanika undani wa sakata la wasanii kulipwa mamilioni kwa kile kinachodaiwa kuwa ni ushiriki wao kwenye kutangaza utalii.

Baada ya taarifa za wasanii hao kuandikwa wiki iliyopita, baadhi yao, akiwamo Babu Tale, walijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kujaribu kujinasua na sakata la matumizi ya fedha za umma.

“Hiyo post ya Instagram ni yangu, nimeumia sana baada ya kusoma gazeti lako, sisi hatukulipwa. Sisi tulijitolea kwa ajili ya serikali, ni kweli sisi tulilala Mount Meru Hotel – Arusha, lakini tulifanya hivyo kwa fedha zetu.

“Msanii ambaye hapa nchini anaonekana hafanyi kazi bila kulipwa ni msanii wangu Diamond Platnumz…kilichotupeleka huko kwenye shughuli ya kupanda Mlima Kilimanjaro na waziri ni kuionyesha serikali kuwa inaweza kututumia sisi kutangaza utalii wetu, maana sisi ni brand.

 “Sisi tulifanya hiyo kama demo tu ili tulipwe baadaye. Waziri Kigwangalla hajatulipa hata kipande cha fedha, tena hadi tumetumia gharama zetu kukodi gari lenye hadhi hatujarudishiwa fedha zetu kiasi cha Sh milioni 1.6 hadi leo.

“Sisi tulikuwa watu wane, yaani mimi (Babu Tale), Diamond, mpiga picha pamoja na mlinzi binafsi wa Diamond…msanii kulipwa Sh 150,000 hadi 300,000 ndiyo kulipwa huko? Sisi hatuchukui hizo Sh milioni 5 wala Sh milioni 50, sisi dau letu linajulikana. Kama wanaweza kuweka tangazo la utalii pale kwenye Uwanja wa Wembley nchini Uingereza kwa nini sisi washindwe kutulipa?” anahoji Babu Tale, na kuongeza:

“Ninachoweza kukwambia ni kwamba sisi (Wasafi) tuliomba sponsorship (udhamini) wa tamasha letu la Wasafi Festival ndiyo maana uliona tulikuwa tunatembelea maeneo kama Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Ngorongoro, Mikumi…hii haina uhusiano wowote na suala la kwenda kwenye hiyo programu ya Waziri Kigwangalla.”

Anasema amepata wakati mgumu kwa Dk. Kigwangalla, hasa baada ya waziri huyo kulalamika kwa mmoja wa wasanii ambao yeye Babu Tale anasema ni swahiba wa karibu wa waziri, kuhusu kutofurahishwa na kitendo cha kuingia mitandaoni kujibu mapigo kwenye habari iliyoandikwa na Gazeti la JAMHURI.

“Nilipata taarifa za kukereka kwa Waziri Kigwangalla kutoka kwa…(jina tunalo), akiniambia waziri amelalamika kwake, hata hivyo nilimwandikia ujumbe mfupi Waziri Kigwangalla ambao hadi hivi sasa [Januari 11] hajanijibu, sijui alikasirika au ni nini,” anasema Tale.

Naye, msanii mwingine, Steve Nyerere, amezungumza na JAMHURI na kusema haoni sababu ya wasanii kuingizwa kwenye ‘ugomvi binafsi’.

“Mimi ninashangaa, kazi ya kutangaza utalii ni kazi ya kizalendo sana na tunamsaidia Rais Dk. John Magufuli, sasa ninyi mlitaka waje wasanii kutoka nje ndio watangaze vivutio vyetu?

 “Tulikaa kikao cha watu saba kabla ya kuanza shughuli hiyo, kikao hicho kiliwahusisha mimi (Steve Nyerere), Diamond, Babu Tale na wengine wanne. Kwenye kikao hicho ninakumbuka tulihoji tutautangaza utalii bila bajeti? (kula, kunywa na kulala) na si kuwalipa wasanii.

 “Utalii wetu ulikuwa unatangazwa na kina Van Damme na Check Norris, unataka hao waendelee kutangaza? Umeona Rwanda leo wanapiga hatua kuliko sisi wakati sisi tunaweza kuisaidia nchi yetu kutangaza utalii,” anasema.

Akijibu swali kuhusu matokeo ya wasanii kushirikishwa kutangaza utalii wa ndani, Steve anasema wamefanikiwa.

“Kuhusu matokeo ya kazi ile ndugu yangu, mimi nimefanikiwa kwa asilimia 150, maana wananchi wote wanajua kwamba nilishindwa kupanda Mlima Kilimanjaro, hivyo watu wengi wanatamani kwenda kuona mlima ulionishinda kukwea,” anasema.

Millard Ayo asubiriwa kwa saa nane

Mwandishi na mmiliki wa Ayo TV, Millard Ayo, pamoja na msanii Mrisho Mpoto ni miongoni mwa wanufaika wa fedha zinazopatikana kwa maelekezo ya Dk. Kigwangalla kutoka katika taasisi kuu nne zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Ayo ndiye aliyetumiwa ndege ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kutoka Arusha na ikamsubiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere [Terminal One] kwa saa nane.

Gharama za kukodi ndege ya abiria 12 (kama zilivyo ndege za Wizara ya Maliasili na Utalii), ni dola 4,500 za Marekani kwa safari ya Dar es Salaam –Arusha. Kwa kiwango cha ubadilishaji fedha cha sasa, kiasi hicho ni wastani wa Sh milioni 10.2. Hii ina maana kwa safari ya Dar es Salaam-Arusha-Dar es Salaam kiasi cha fedha kilichotumika ni wastani wa Sh milioni 20.4. 

Kama Kigwangalla angeamua utumike usafiri wa ndege za biashara, gharama kwa safari hiyo, kwa maana ya tiketi ya kwenda na kurudi ingekuwa wastani wa Sh 600,000 wakati huu wa msimu wa utalii.

JAMHURI limemtafuta Ayo, lakini hakupatikana ofisini kwake wala kwenye njia nyingine zote za mawasiliano kwa siku tano.

 “Ni rahisi sana kuomba miadi ya kumuona bilionea Bakhresa kuliko kukutana na Millard Ayo, kaka nakuambia hautamwona Millard hata tuki-bet [kucheza kamari],” kimesema chanzo chetu.

JAMHURI limezungumza na msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) ambaye ndiye msanii aliyetumiwa ndege Kigoma ambako alikwenda kufanya shughuli zake na kupelekwa Arusha.

Kama ilivyo kwa Ayo, wastani wa gharama za ndege zilizotumika kukodi ndege kutoka Arusha-Kigoma-Arusha ni Sh milioni 10.2 kwa safari moja.

Mpoto alipatikana, lakini baada ya kuelezwa lengo la kumtafuta, hasa kutumiwa ndege Kigoma, aliomba apigiwe simu baadaye.

“Nina kazi kidogo zimenitinga ila kama ni jambo mahususi tunaweza kuongea…nitakupigia tuongee vizuri sana kuhusu mimi kufuatwa na ndege Kigoma pamoja na kampuni ambayo ninafanya nayo kazi, mimi ninafanya kipindi cha televisheni kinaitwa ‘Kaa Hapa’,” anasema Mpoto.

Usuli

Chanzo cha ugomvi kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda, kimebainika ni hatua ya katibu huyo kupinga uchotwaji fedha unaofanywa na Dk. Kigwangalla kupitia kivuli cha kutangaza utalii.

Desemba 31, mwaka jana Rais John Magufuli akiwa mapumzikoni katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo mkoani Geita aliwapa siku tano viongozi hao kupatana, vinginevyo angetengua uteuzi wao.

Pamoja na uchotwaji fedha taslimu, waziri huyo analalamikiwa pia kwa matumizi yasiyo sahihi ya mali zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, zikiwamo ndege.

Katika matukio mawili ya karibuni, aliagiza ndege ya TANAPA imfuate msanii Kigoma ili ashiriki tamasha jijini Arusha.

Katika tukio la pili, Dk. Kigwangalla aliamuru ndege ya TANAPA imfuate mwanahabari jijini Dar es Salaam na kumpeleka Arusha, Rubondo, Katavi na baadaye akarejeshwa Arusha.

Wageni wake, wakiwamo wasanii wakiwa katika majiji kama Arusha hulazwa katika hoteli za kifahari za kuanzia hadhi ya nyota nne.

Chanzo cha habari kinasema Profesa Mkenda amekuwa haridhishwi na matumizi ya fedha hizo, na amekuwa akitaka taratibu zifuatwe ili kunusuru fedha za umma, lakini na yeye mwenyewe kama mtendaji mkuu na ofisa masuuli wa wizara abaki salama.

Dk. Kigwangalla, kama alivyowahi kufanya aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wa mwisho katika Awamu ya Nne, Lazaro Nyalandu, amekuwa akiagiza apewe fedha nyingi ili kuwalipa wasanii kwa kigezo cha kuwatumia kuhamasisha utalii ndani na nje ya nchi.

Kwa kigezo hicho amekuwa akitumia makundi ya wasanii kuzunguka huku na kule nchini kufanya shughuli hiyo. Wasanii hao huzuru hifadhi za taifa, pia hushiriki matamasha mbalimbali.

Hivi karibuni alipeleka kundi la wasanii kukwea Mlima Kilimanjaro, lakini ni mmoja tu aliyefanikiwa kufika kileleni. Wengine, licha ya kushindwa, waliendelea kulipwa fedha kwa muda wote uliopangwa.

Imeelezwa kwamba Waziri Kigwangalla amekuwa akiagiza apewe fedha kutoka katika taasisi kuu zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Taasisi hizo ni TANAPA, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

“Kuna makundi ya wasanii yanapelekwa kwenye maeneo mbalimbali ya hifadhi, gharama zake ni kubwa. Waziri anaagiza gharama zibebwe na wizara, sawa; lakini kuwe na utaratibu, yeye hataki. Unakuta anaagiza zitolewe Sh milioni 170, zitolewe Sh milioni 80; mara zitolewe Sh milioni 100 na kadhalika. Hizi fedha ni nyingi, na kwa maana hiyo lazima kuwe na utaratibu wa kifedha wa kuziomba na kuzitoa.

 “Mbaya zaidi, fedha hizo hutakiwa zilipwe na wakuu wa taasisi kwa maelekezo ya waziri. Huo si utaratibu. Kule kwenye taasisi wakisema hawana mamlaka ya kufanya malipo bila maelekezo ya katibu mkuu, mgogoro huanzia hapo.

 “Katibu Mkuu anapoambiwa anang’aka na kutaka fedha zisitolewe bila kufuata mfumo wa malipo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Waziri akishajua katibu mkuu amekwamisha malipo kwa sababu hizo, basi ugomvi unalipuka,” kinasema chanzo chetu.

JAMHURI limeelezwa kuwa baada ya Waziri Kigwangalla kuona anakwamishwa na katibu mkuu, alianza kutumia utaratibu wa kumwagiza msaidizi wake kuwasiliana moja kwa moja na wakuu wa taasisi hizo ili wafanye malipo.

 “Hilo nalo lilionekana kuwa ni ukiukwaji wa taratibu, kwa sababu msaidizi wa katibu hana mamlaka ya kuwasilisha maelekezo ya kufanyika malipo. Utoaji fedha za umma una taratibu zake,” kinasema chanzo chetu. 

Fedha zinazochotwa kutoka kwenye taasisi hizo zinatumika kugharimia usafiri, malazi na posho za wasanii.

Hata hivyo, baadhi ya waliozungumza na JAMHURI wanasema kinachofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuwatumia wasanii kinavuka mipaka ya ‘utangazaji utalii’, badala yake kuna mkakati wa kisiasa kwa ajili ya siku zijazo.

“Ninachoweza kukuhakikishia ni kuwa kuna mpango wa watu kuwania nafasi kubwa zaidi mwaka 2025, kwa hiyo kinachofanyika sasa ni kuwavuta wasanii ili wawe karibu nao kwa ajili ya mwaka 2025. Hili halina ubishi kwa sababu tumo humu tunajua mengi.

“Kinachofanywa sasa ni kujenga mtandao wa kuungwa mkono na ndiyo maana unaona wanaotumika hapa ni wasanii na watu wa online,” kinasema chanzo chetu na kuongeza:

“Angalia hata wajumbe wa bodi, baadhi yao wanateuliwa kwa sababu ni marafiki wa wakubwa wizarani.”

Mwanzoni mwa Desemba, mwaka jana wasanii saba walifanya ziara katika baadhi ya hifadhi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sehemu ya kujionea vivutio ili kuvitangaza, hivyo kuhamasisha wageni na wenyeji kutalii.

Ziara hiyo ilianzia katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato na kuendelea hadi hifadhi za taifa za Ibanda – Kyerwa na Rumanyika – Karagwe. Kiongozi mkuu wa msafara alikuwa Dk. Kigwangalla mwenyewe.

Wasanii wa muziki na maigizo (Bongo Movie) walioshiriki ni Steve Nyerere, Dude, Richie, Shilole, Ebitoke, Shetta na mwakilishi kutoka Muziki AT (Zanzibar). Baadaye walizuru Hifadhi ya Taifa ya Rubondo.

Rais Magufuli akizungumza na wahifadhi wa Rubondo, alisema: “Ninafahamu, watendaji wenu wa juu, Katibu Mkuu na Waziri kila siku wanagombana, ninawatazama taratibu na nilishampa kazi Katibu Mkuu Kiongozi awaite na awaeleze, lakini wasipobadilika nitawaondoa…Siwezi kuwa na watendaji ambao nimewateua mwenyewe halafu wanagombana, na kuna mambo mengi hayaendi. Katibu Mkuu hamheshimu waziri na waziri hataki kwenda na katibu mkuu, siwezi kuvumilia hilo.

“Leo nawaambia wajirekebishe na ikiwezekana wajirekebishe ndani ya siku tano, wawe wanasalimiana na wanazungumza, mimi ninafahamu, nina vyombo, ninajua nani hafai zaidi,” alisema Rais Magufuli.

Baada ya kauli ya Rais Magufuli, Waziri Kigwangalla kupitia akaunti yake ya Twitter aliandika: “Kazi ya urais ni ngumu sana. Tulioteuliwa na Mheshimiwa Rais kumsaidia utendaji/usimamizi wa maeneo mbalimbali hatupaswi kumuongezea Rais frustration nyingine zaidi. Sisi kwenye wizara yetu, baada ya kikao na Chief Secretary (Katibu Mkuu Kiongozi) tulimaliza tofauti zilizokuwepo na sasa hali ni shwari!”

Gazeti la JAMHURI limemtafuta Dk. Kigwangalla kwa njia zote za mawasiliano ili kupata maoni yake, lakini hakupokea simu wala kujibu maswali aliyoandikiwa. Katibu Mkuu, Profesa Mkenda, hakuwa tayari kuzungumza.

Wizara yenye vishawishi

Wizara ya Maliasili na Utalii inatajwa kuwa miongoni mwa wizara zenye vishawishi na fitina nyingi. Mara kadhaa viongozi wenye ‘roho nyepesi’ za kujipatia ukwasi wamekuwa hawadumu.

Lakini pia wale wanaokuwa na ‘mioyo migumu’ ya kukataa kushiriki magenge ya ufisadi wamekuwa wakiandamwa kwa kuundiwa fitina ambazo hatimaye huwaondoa madarakani.

Kuanzia mwaka 2006, Wizara ya Maliasili na Utalii imeongozwa na mawaziri saba kwa vipindi vinane. Alianza Anthony Diallo, akafuata Profesa Jumanne Maghembe, Shamsa Mwangunga, Ezekiel Maige, Balozi Khamis Kagasheki, Lazaro Nyalandu, Jumanne Maghembe (mara ya pili) na sasa ni Dk. Hamis Kigwangalla.

Kwa kipindi hicho makatibu wakuu waliopitia wizara hii ni Salehe Pamba, Blandina Nyoni, Dk. Ladslaus Komba, Dk. Adelhelm Meru, Maimuna Tarishi, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, na sasa ni Profesa Mkenda.

Idara ya Wanyamapori inayotajwa kuwa yenye vishawishi vya kila aina, haikuwa nyuma kwenye pangua pangua za wakurugenzi wake.

Kuanzia mwaka 2006 idara hiyo imeongozwa na Emmanuel Severe, Erasmus Tarimo, Obeid Mbangwa, Profesa Alexander Songorwa (mara mbili), Paul Sarakikya (Kaimu), Herman Keraryo na sasa ni Dk. Maurus Msuha.

Kigwangalla kama Nyalandu

Nyalandu anayetajwa kuwa miongoni mwa mawaziri walioifaidi vilivyo Wizara ya Maliasili na Utalii, alifikia hatua ya kuwa na vyumba maalumu katika hoteli za kitalii katika majiji ya Dar es Salaam na Arusha vilivyolipiwa na taasisi za NCAA na TANAPA. Malipo hayo hayakuzingatia kama amelala, au la.

Ofisini kwake kwenye Jengo la Mpingo, alionekana kwa nadra; na hata alipotaka kuzungumza na waandishi wa habari, alitumia hoteli za kitalii ambazo malipo yake huanzia Sh milioni 3 kwa saa kadhaa.

Alifanya hivyo ilhali wizarani kwake kukiwa na ukumbi wa kisasa wenye viyoyozi na huduma zote za kuendeshea mikutano.

Mara kadhaa alitumia ndege za taasisi zilizo chini ya wizara yake kwa ajili ya shughuli binafsi zisizokuwa na uhusiano na kazi zake za ofisi.

Kama Kigwangalla, Nyalandu pia aliwatumia wasanii kwenye shughuli mbalimbali, lakini nyuma ya mpango huo ikabainika kuwa kulikuwa na mkakati wa kuvuna fedha. Wakati fulani alilazimisha malipo ya Sh milioni 500 kutoka TANAPA kwa ajili ya kudhamini shindano la urembo.

Miaka ya mwisho ya uongozi wake alisafiri na msanii wa filamu za Tanzania, Aunty Ezekiel Grayson, nchini Marekani na kukaa huko kwa siku 14 kwa gharama za Wizara ya Maliasili na Utalii.

Walikwenda huko kwa kile kilichoelezwa kuwa ni mapumziko, na wakati huo huo kumtumia kutangaza vivutio vya utalii ili kuvutia watalii wengi kuja nchini Tanzania.