Busara na hekima ni maneno mafupi na mepesi kutamkwa na mtu yeyote. Lakini ni mapana na mazito katika kuyatambua, kuyahifadhi na kuyatumia kama nyenzo ya kumfikisha mtu kwenye malengo na makusudio yake kwa jamii.
Maneno haya, kila moja lina herufi sita na yanashabihiana katika maana na matumizi; na yanabeba neno akili. Upacha na uhusiano wao unaunganishwa na neno falsafa, lenye maana ya elimu ya akili, maana na sababu za mambo au vitu.
Ndani ya busara na hekima kuna dhana nyingi kama vile maarifa, werevu, ujuzi, ujanja, fikira, mtazamo, adili n.k. Nafikiri kwa mantiki hii ndiyo maana viongozi wawe wa siasa, wa dola, wa dini au wa michezo na kadhaa hawana budi kubeba busara na hekima.
Mtu mwenye mwono na uzingatio wa falsafa anapozungumza na mtu au watu, huchukua hadhari kabla ya kutamka kusudio, lengo au madhumuni yake. Hufanya hivyo akiwa na shabaha ya kutaka kueleweka, kukubalika na kufuatwa.
Busara au hekima huonekana pale lugha itumikapo katika kuelezea, kunasihi au kuhimiza jambo Fulani, husaidia mno kujenga uelewano na uhusiano kati ya kiongozi na kiongozi na kati ya kiongozi na wanaoongozwa.
Kiongozi hupata sifa nzuri na kuheshimika anapotumia busara katika uamuzi wa vitendo vyake; na anatumia hekima katika mazungumzo yake. Asipofanya hivyo, ukweli, hushusha na hupoteza sifa za uongozi wake.
Busara na hekima hazipatikani kama nguo za kununuliwa dukani. Ni dhana adhimu zilizomo ndani ya silika ya mwanadamu. Huchomoza pale mtu atumiapo akili na fahamu zake kwa uadilifu katika kuunganisha tabia za watu kufanya mema na kuacha mabaya.
Dhana hizo pia hupimwa na hutolewa maana na tafsiri na watu mbalimbali wanaopokea lugha inayozungumzwa na mtu au kiongozi yeyote aliyekusudia ujumbe wake kuwafikia walengwa. Mapokezi yake huwa chanya au hasi.
Hasi au chanya hutokea mzungumzaji anapotumia lugha ya hamaki na chuki kufikisha ujumbe wake kwa watu, ambao tayari wana hasira na kinyongo na wengine wenye kuangalia na kusikitika kutokana na madhila yaliyokwisha au yanayoendelea kutokea.
Mara kadhaa, Watanzania tumeshuhudia kuona na kusikia baadhi ya viongozi wetu katika vyama vya siasa, serikalini na hata katika michezo wakitoa lugha zenye ukakasi na kutia mzizimo wa hofu katika mioyo yetu huku tukijikaza kama vile hakuna jambo.
Ni vyema viongozi wetu mkatumia lugha za kujenga siyo za kubomoa hata kama tunaona kiongozi au mtu fulani ameikosea jamii ya Watanzania, ni busara na hekima mtu au kikundi fulani kuitwa kwenye meza ya mazungumzo.
Hakuna jambo jema lolote lililofaulu duniani kwa kutumia ukaidi, ufedhuli au ubabe. Ila ufaulu wake huwa mbaya na hasara. Kukiri udhaifu na ujinga si ubwege; ni utu na uungwana. Ni busara hapa kuzingatia methali ya Kiswahili ‘Kwa mwoga huenda kicheko, kwa shujaa huenda kilio’.
Dua za kumwombea mtu zina thamani kubwa iwapo mtu anayeombewa anafanya ibada ya kuomba mema mwenyewe kwanza na kutofanya mabaya. Waislamu wanasema ‘sali kabla ya kujasaliwa upate rehema na pepo ya Allah, huku ukisimamisha sala.’
Namalizia makala hii kwa kuwaomba viongozi wangu nchini, katika vyama vya siasa, serikalini na taasisi za utetezi wa haki za binadamu watumie busara na hekima, wanapotoa kauli (lugha) zao zisiwe za ushabiki na mlolongo wa chuki na inda.
Narejea, Padri Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Pugu, tarehe 22/3/1955 akamwita Mwalimu Julius Nyerere na kumwambia, “Mwanangu Julius, ualimu na siasa havipatani hata kidogo, fuata oni langu, uache kabisa mambo ya siasa na uzingatie kazi yako ya ualimu.” (Kitabu ‘Uamuzi wa Busara’).
Mwalimu alikwenda nyumbani akayafikiri maneno hayo na akajiuliza afanye nini sasa. Akapiga konde moyo, akampa padre barua ya KUJIUZULU. Mwalimu akafanya uamuzi wa busara wa kuacha kazi. Leo Watanzania tuko huru. Narudia kusema BUSARA na HEKIMA ni muhimu.