Serikali imekamata madini yenye thamani ya Sh bilioni 13.12 yaliyokuwa yakisafirishwa nje ya nchi kinyume cha sheria kwa kipindi cha kuanzia Oktoba, 2012 hadi Aprili, mwaka huu.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alitoa taarifa hiyo kwenye hotuba yake ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2013/2014 bungeni, jana.

Alisema wahusika wamechukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.

 

“Katika kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini nchini, Serikali kupitia Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) imeanzisha Madawati Maalum ya kukagua madini yanayosafirishwa nje ya nchi kupitia Viwanja vya Ndege vya Kimataifa vya Mwalimu Julius Nyerere ( Dar es Salaam ), Kilimanjaro na Mwanza.

 

“Madawati hayo yamesaidia katika kubaini na hatimaye kuwakamata watu wasio waaminifu wanaosafirisha madini nje ya nchi kinyume cha Sheria,” alisema.

 

Uharibifu, wizi waiumiza Serikali

Wizara ya Nishati na Madini imesema wizi na uharibifu wa miundombinu ya umeme nchini, umevuka kiwango.

 

Imesema katika kipindi cha Julai, mwaka jana na Aprili mwaka huu, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limepata hasara ya Sh milioni 966.

 

Alisema, “Kwa muda mrefu kumekuwa na tatizo sugu kutokana na wahusika kubuni njia mbalimbali za kufanya uharibifu huo na kusababishia TANESCO na nchi kwa ujumla hasara kubwa.

 

“Ili kukabiliana na tatizo hili, Wizara kupitia TANESCO imefanya juhudi mbalimbali zikiwemo za kuweka transfoma karibu na maeneo ya makazi ili kuimarisha ulinzi, kutumia transfoma zisizohitaji mafuta, kutumia nyaya za aluminiamu badala ya shaba; na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale wote wanaothibitika kujihusisha na wizi na uharibufu wa miundombinu ya umeme.

Ruzuku kwa TANESCO

 

Agosti, 2011 Serikali iliamua kuidhamini TANESCO ili ipate mkopo wa Sh bilioni 408.

 

 

 

Profesa Muhongo alisema kutokana na taratibu za mikopo za kibenki, TANESCO ilipata Sh bilioni 104 na hivyo kuifanya Serikali kulazimika kuingilia kati na kutoa Sh bilioni 402.23 kama ruzuku badala ya mkopo.

Muundo mpya wa TANESCO

Profesa Muhongo aliliambia Bunge kwamba Serikali imeamua kupitia upya muundo wa TANESCO ili kuongeza ufanisi na kuongeza ushindani katika sekta ndogo ya umeme kwa lengo la kuboresha huduma za umeme nchini.

Alisema Wizara imepokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali, wakiwamo wananchi na inatarajia kupokea mapendekezo ya muundo kutoka Menejimenti na Bodi ya TANESCO ifikapo Mei 31, mwaka huu.

“Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imetoa fedha za kumpata mshauri ambaye atatoa mapendekezo juu ya muundo mpya wa TANESCO unaofaa kufikiriwa na Serikali.

“Benki hiyo pia, imekubali kutoa fedha za kujenga uwezo wa watendaji wa Wizara, TANESCO na TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ). Baada ya kupokea mapendekezo kutoka vyanzo mbalimbali, Wizara itaandaa Mwongozo  wa namna bora ya kubadilisha muundo wa TANESCO na sekta ndogo ya umeme. Mwongozo umepangwa kukamilika Juni, mwaka kesho,” alisema.

Changamoto katika sekta ya nishati

Alisema pamoja na mafanikio hayo, Wizara katika Mwaka 2012/2013 ilikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kudhibiti upotevu wa umeme, kuwa na mbadala wa kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia nyumbani, kufikisha umeme vijijini, kukidhi ongezeko la mahitaji ya nishati nchini- hususan umeme, kuongeza wigo wa rasilimali au vyanzo vya kuzalisha umeme, kukidhi matarajio ya wananchi kuhusu manufaa yatokanayo na gesi asilia, kuvutia uwekezaji katika sekta ya nishati, mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yameathiri ufuaji wa umeme kutokana na maji; na uzalishaji wa umeme wa uhakika na wa kutosheleza ambao kwa kiasi kikubwa umetegemea zaidi mafuta mazito na dizeli ambayo ni ghali.

Mchango wa sekta ya madini kwenye pato la Taifa

Profesa Muhongo alisema katika Mwaka 2012/2013, Wizara imeendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya kukuza shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini nchini.

Alisema Wizara iliimarisha usimamizi wa sekta ya madini ili kuongeza mchango wake kwenye pato la Taifa.

“Kiwango cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi za uchimbaji madini kilifikia asilimia 7.8 katika mwaka 2012 ikilinganishwa na asilimia 2.2 Mwaka 2011. Aidha, mchango katika pato la Taifa ulifikia asilimia 3.5 ikilinganishwa na asilimia 3.3 kwa Mwaka 2011 kwa bei ya mwaka 2012.

“Thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi iliongezeka kutoka dola bilioni 1.98 za Marekani (Sh bilioni 3,168.32) mwaka 2011 hadi kufikia dola bilioni 2.3 (Sh bilioni 3,684.05) mwaka 2012. Ongezeko hili la asilimia 16.3 lilitokana na kupanda kwa bei ya dhahabu katika  soko la dunia kutoka wastani wa dola 1,571.28 za Marekani kwa wakia mwaka 2011 hadi kufikia wastani wa dola 1,668.63 za Marekani kwa wakia mwaka 2012.

“Thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi imeendelea kuchangiwa kwa kiwango kikubwa na madini ya dhahabu ambapo mchango wake kwa mwaka 2012 ni takriban asilimia 94,” alisema.

Elimu kwa umma kuhusu uchimbaji wa madini ya urani

Profesa Muhongo alisema Serikali iliendelea na jukumu la kutoa elimu kwa kupitia vyombo vya habari na ziara za mafunzo kuhusu faida na changamoto za uchimbaji wa madini ya urani, ili kuondoa hofu kwa umma juu ya madhara ya utafutaji na uchimbaji wa madini hayo.

“Napenda kutumia nafasi hii kusisitiza kuwa kitaalamu, urani ikiwa katika hali ya muunganiko na oksijeni (Triuranium Octoxide – U3O8) kama ilivyo ardhini ama baada ya kuchimbwa na kuchenjuliwa haina madhara kama inavyodaiwa na baadhi ya watu. Uchimbaji wa madini ya urani unatarajiwa kuanza katika eneo la Mkuju wilayani Namtumbo. Serikali itakuwa na hisa kwenye mgodi huu. Nawaomba wananchi waondoe hofu kuhusu madhara tarajiwa ya utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa Serikali yao ipo makini na itazingatia taratibu zote za kitaifa na kimataifa za kuchimba, kutunza, kusafirisha na kuendeleza madini hayo.

 

 

 

“Mradi wa Mkuju unaomilikiwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Ltd iliyosajiliwa na Msajili wa Kampuni chini ya Sheria za Tanzania uliuzwa Desemba 2010 kwa Kampuni ya ARMZ ya Urusi baada ya kununua hisa za Kampuni mama iitwayo Mantra Resources ya Australia kupitia Soko la Hisa la Australia kwa bei ya dola milioni 1,043.80 za Marekani (Sh. bilioni 1,670.08. Serikali kupitia TRA iliwapatia madai wahusika ya dola milioni 205.8 ambako dola milioni 196 zilitakiwa kulipwa kama Capital Gain Tax na dola milioni 9.8 ni Ushuru wa Stempu. Hata hivyo, Kampuni hiyo ilipinga madai hayo na shauri hilo lilifikishwa Mahakama ya Kodi,” alisema.