Thamani ya dhahabu na almasi zilizozalishwa nchini mwaka jana na kampuni kubwa zinazochimba madini hayo nchini iliongezeka kwa dola milioni 55.5 za Marekani ukilinganisha na kiasi kilichopatikana mwaka 2018.
Kwa mujibu wa takwimu mpya za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ongezeko hilo la takriban asilimia 3.8 lilitokana kwa kiasi kikubwa na thamani ya dhahabu iliyozalishwa na wachimbaji wakubwa.
BoT inasema kuongezeka kwa thamani ya dhahabu kulichangiwa sana na kupanda kwa bei yake kwenye soko la dunia ambayo sasa hivi ni zaidi ya dola 1,600 za Marekani kwa kila wakia kutokana na mlipuko wa kirusi cha corona duniani.
Taarifa za hali ya uchumi za Benki Kuu zinaonyesha kuwa thamani ya dhahabu na almasi zilizozalishwa mwaka 2019 ilikuwa dola milioni 1,534.5 za Marekani wakati thamani ya madini hayo mwaka uliotangulia ilikuwa dola milioni 1,479.1 za Marekani.
Katika robo ya nne ya mwaka jana, thamani ya madini hayo ilikuwa dola milioni 441.2 za Marekani, kiasi ambacho ndicho kilichokuwa kikubwa zaidi kwa mwaka mzima. Kati ya Julai na Septemba, dhahabu na almasi zilizozalishwa zilikuwa na thamani ya dola milioni 388.9 za Marekani, wakati thamani kwenye robo ya pili na ya kwanza ilikuwa dola milioni 378.5 za Marekani na dola milioni 325.9 za Marekani mtawalia.
“Dhahabu na almasi zenye thamani ya dola milioni 441.1 za Marekani zilizalishwa na wachimbaji wakubwa kwenye robo ya mwaka iliyoishia mwezi Disemba mwaka 2019, hili likiwa ongezeko la asilimia 7.8 ulikiganisha na kipindi kama hicho mwaka 2018,” BoT inasema kwenye taarifa ya hali ya uchumi katika robo ya nne ya mwaka jana.
Dhahabu ni moja ya vyanzo vikubwa vya fedha za kigeni nchini, ikiwa ya pili nyuma ya utalii, ikiongoza bidhaa zote zinazouzwa nje ya nchi kwa mapato. Mauzo ya madini hayo mwaka jana yaliongezeka kwa asilimia 45.5 hadi dola milioni 2,217.1 za Marekani kutokana na kuongezeka kiasi kilichouzwa na bei yake kwenye soko la dunia.
Mwaka 2018, fedha za kigeni zilizotokana na mauzo ya dhahabu nje ya nchi zilikuwa na thamani ya dola milioni 1,524 za Marekani, ikilinganishwa na dola milioni 1,541.1 za Marekani. Kuongezeka kwa mapato ya dhahabu mwaka jana ni moja ya matokeo ya mageuzi makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwenye sekta ya madini.
Mageuzi hayo ni pamoja na kuanzishwa kwa vituo maalumu vya kuuzia madini ili kudhibiti magendo ya rasilimali hiyo na kuiwezesha serikali na taifa kwa ujumla kupata mapato stahiki kutokana na biashara hiyo.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji Sekta ya Madini jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema mageuzi kwenye sekta hiyo pia yanalenga kuongeza mchango wa madini kwenye pato la taifa.
“Kwa sasa hivi mchango wa madini ni asilimia 3.5 lakini ifikapo mwaka 2025 utakuwa umeongezeka hadi asilimia 10,” waziri mkuu aliwaambia washiriki wa mkutano.