Imetimu miaka 27 sasa tangu Watanzania waamue kurejesha mfumo wa demokrasia wa vyama vingi vya siasa nchini (1992 -2019).
Katika harakati za kurejesha mfumo huu, kuna hotuba nyingi. Miongoni mwao viongozi waliotoa hotuba za namna hiyo ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, baada ya kukubali mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kuhusu kurejeshwa mfumo wa demokrasia wa vyama vingi vya siasa nchini, alihutubia katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa wa CCM uliofanyika Februari 18, 1992 jijini Dar es Salaam. Ifuatayo ni sehemu ya hotuba hiyo kuhusu mageuzi.“Ili mageuzi haya tunayoyazungumza yaweze kufana katika hali ya utulivu na amani, yanahitaji yaongozwe na CCM yenye umoja, nguvu na mshikamano.
“CCM si chombo kinachozama, ambacho baadhi ya watu waliomo wanataka kukimbia wasizame nacho. CCM ni chama chenye nguvu, na kama TUME ya Rais ilivyobainisha. Wananchi wengi wangependa tuendelee na utaratibu huu wa chama kimoja chini ya CCM.
Ndiyo maana, mimi kwa upande wangu napenda mageuzi haya yafanyike hivi sasa. Maana kila mageuzi makubwa huhitaji kiongozi mwenye uwezo na anayeaminiwa na wananchi. CCM ni kiongozi mwenye uwezo huo na anaaminiwa na wananchi.
“Mageuzi haya hayana budi kusimamiwa na kuongozwa na Chama Cha Mapinduzi chenye umoja, nguvu na mshikamano. Ndugu wananchi, ndugu wajumbe, naomba mniamini katika hilo. Nalisema na kuliamini kwa dhati ya moyo wangu. Lakini naomba mniamini pia katika hili lifuatalo.
“Historia ni sehemu ya historia ya chama chetu na nchi yetu. Ni matokeo halali kabisa ya kuwa na chama kimoja chenye nguvu na kinachopendwa na wananchi kwa muda mrefu. Lakini sasa tunazungumzia uwezekano wa kuruhusu mfumo wa vyama vingi.
“Mimi sitashangaa hata kidogo ikiwa baada ya sheria kubadilika, baadhi ya wanachama wa CCM wataona kuwa mawazo yao hayawezi tena kuwa na manufaa au kueleweka kiasi ya kutosha ikiwa watabaki ndani ya CCM. Wakiamua kutoka katika CCM na kuanzisha chama kingine, kwa maoni yangu tutafanya makosa makubwa sana kuwaona kuwa ni wasaliti.
“Kama tutaanzisha utaratibu wa vyama vingi kwa moyo mmoja, basi tunataka vyama ambavyo vinaweza kuchaguliwa na wananchi wa Tanzania kuunda serikali ya nchi yetu.
“Halmashauri Kuu ya Taifa haituombi tutoe ruhusa ya kuanzisha utitiri wa vyama vya ovyo ovyo. Nani anavitaka? Nani anavitaka vyama vya utitiri? Vya ovyo ovyo! La sivyo baadhi ya wanachama wa CCM watasema potelea mbali, na wataanzisha chama au vyama na kukabili kutukanwa na wenzao watakaobaki ndani ya CCM.
“Matokeo ni kutukanana na tutakuwa tumeweka msingi wa vyama vya uhasama. Nani anataka vyama vya uhasama?
“Najua wapo watu wanaodhani kuwa vyama vya siasa ni vyama vya uhasama. Matumaini yangu ni kwamba watu hawa hawamo ndani ya CCM. Basi, tufanye kitendo ambacho kitawasaidia au kitatufanya sisi tusifanane nao.
“Leo tunajadiliana juu ya tofauti zetu ndani ya chama kimoja. Wakati mwingine kama nilivyosema tunazivungavunga tofauti zetu kwa sababu ya kuoneana haya. Lakini hatugombani na tofauti zetu zinabaki palepale.
“Kesho bila ya kubadili mawazo yetu na kwa kuamini kwa dhati kabisa kwamba tunaweza kuendeleza mawazo hayo vizuri zaidi. Tunaweza tukajikuta katika vyama viwili mbalimbali.
“Kwa nini tugombane! Na tutukanane! Ni kweli kwamba sasa tutalazimika kuzielewa tofauti zetu waziwazi zaidi na hadharani ili wananchi waweze kuzielewa. Hilo ni jambo la kawaida katika mfumo wa demokrasia wa vyama vingi. Lakini si sababu ya kutugombanisha,” mwisho wa kunukuu.
Watanzania wenzangu kwa kiasi gani tumepokea nasaha hizi na kuzitekeleza kwa heri na amani, katika kipindi chote tangu tuingie tena katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi? Kumbuka, muungwana ni kitendo.