Wiki iliyopita makala hii iliishia pale ambapo ilionyesha kwamba Tanzania ni yetu, wa kuiua ni sisi wenyewe na wa kuijenga ni sisi wenyewe. Maisha yana ladha pale tu tunapotofautiana mitazamo, sasa endelea …

Maisha hayawezi kuwa na ladha kama mitazamo yetu itafanana. Tukifanana mitazamo tutakuwa kama wanyamapori wa mwituni wajulikanao kama ‘nyumbu’.

Kuna mafanikio makubwa katika kutofautiana kimtazamo. Maana yangu ni kwamba hauwezi kunilazimisha nikubaliane na mtazamo wako kama mtazamo wako hauna vigezo vya kunishawishi nikubaliane nao. Hali kadhalika, mimi pia siwezi kulazimisha ukubaliane na mtazamo wangu kama hauna vigezo vya kukushawishi ukubaliane nao.

Pamoja na ukweli kwamba binadamu wote ni sawa, lakini uwezo wa kufikiri na kufikia uhalisia wa mambo unatofautiana. Mawazo aliyonayo mtu huweza kumtofautisha na mtu mwingine.

Ili maisha yako yawe na ladha, lazima yapate mkosoaji, binadamu ni mkosoaji na mkosolewa. Kukosolewa ni kuambiwa ukweli mwingine tofauti na ule unaouamini. Kila binadamu anaishi na falsafa yake, awe anaijua au haijui, bado ni falsafa.

Ikitokea mtu kwa sababu ya ujinga wake asielewe anaishi falsafa gani ya maisha, hilo litakuwa ni tatizo lake binafsi na si tatizo la falsafa anayoishi…

Tukubaliane wote katika jambo hili: ‘Hakuna binadamu aliyekamilika’. Kama yupo binadamu aliyekamilika basi huyo atakuwa si binadamu aliyeumbwa na Mungu. Fahamu jambo hili, kila binadamu ana ujinga fulani.

Unapokosolewa ni kama unaonyeshwa ujinga ulionao, bahati mbaya si kila binadamu anaweza kuona ujinga alionao. Niruhusu niseme; demokrasia ni kutofautiana mawazo.

Kama nchi inafuata mfumo wa demokrasia, basi imekubali watu wake kutofautiana mawazo. Demokrasia ni kama mpira wa miguu, kila timu lazima icheze kwa bidii ili ishinde. Umewahi kuona wapi wachezaji wa timu moja wamefungwa miguu uwanjani huku wenzao wakicheza?

Mwalimu Nyerere anasema hivi: “Demokrasia ya kweli ni lazima ihitaji kila mtu aweze kusema kwa uhuru kabisa na mawazo ya kila mtu lazima yasikilizwe, hata kama mawazo ya mtu huyo hayapendwi kiasi gani au walio wengi wanadhani amepotea kiasi gani, si kitu.”

Misingi ya demokrasia inafundisha kwamba; kiongozi aliyeingia madarakani kidemokrasia hawezi kutaka kuongoza bila kufuata demokrasia iliyomweka madarakani. Nje ya demokrasia, uongozi wake hauwezi kuwa salama na mihimili mingine haiwezi pia.

Ningeulizwa leo kama Tanzania kuna demokrasia au hakuna, ningejibu: “Tanzania hakuna demokrasia, kuna kivuli cha demokrasia.”

Taswira ya kisiasa katika taifa letu sasa hivi haiko salama, hilo liko wazi. Sihitaji kuyasimulia mateso wanayopata viongozi wa upinzani.

Watanzania wote tunayaona, dunia inayaona. Vyama shindani sasa hivi wanapitishwa kwenye tanuri la moto. Wengine wanaungua kwa kuuguza majeraha ya risasi. Wengine wanatoweka katika mazingira tatanishi. Waandishi wa habari wengine wametoweka.

Wengine sasa hivi wameamua kuwa waandishi wa kuisifia serikali tu. Hapana, hii si Tanzania tunayotakiwa kuijenga. Nchi ya waoga wa kuthubutu, nchi ya wanafiki, nchi ya kujipendekeza kwa watawala.