Kumbe wananchi 7,565,330 hawakujitokeza kutumia hiyo haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi wao. Je, hawa wasiopiga kura kweli wote walikuwa na sababu za msingi kutokupiga kura zao? Tunajua kati ya hao watu 7,565,330 wapo waliotangulia mbele ya haki, wapo waliokuwa wagonjwa mahututi na wasingeweza kupiga kura lakini tuamini kuwa watu 7,565,330 walikuwa na sababu za msingi za kutokupiga kura? Siyo kweli. Hapo ndipo mimi nasema Rais Obama alikuwa sahihi alipowahimiza wapiga kura wa Marekani kwa kuwaambia…”if you are serious about democracy, you can’t afford to stay home just because she (Clinton) might not align with you on every issue” (Rais Obama Philadelphia tarehe 22 Julai, 2016). Kama watu wote hawa zaidi ya milioni 7 na nusu hawakuridhika na uteuzi wa vyama ndipo wakasusa kupiga kura, haikuwa sahihi.
Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi hapo nasema wale wote wasiopiga kura zao Oktoba 2015 kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani eti kwa kuwa mtu wao hakuteuliwa na chama, kwa kutokuridhika kwao na kama wamesigana kimtazamo na mgombea huyo, siyo sababu ya kutosha kwao kutokupiga kura. Demokrasia inadai kila aliyejiandikisha, mradi haumwi au hana sababu ya msingi anapaswa kwenda kupiga kura yake. Je,hawa wenzetu millioni 7 na nusu waliielewa demokrasia kweli?
Uchaguzi wa Marekani kidemokrasia yao, unachukua miezi kama 5 hivi ya kampeni mpaka kuifikia tarehe ya kupiga kura. Katika muda huo wote wagombea wanajinadi katika majimbo. Ni kazi ngumu kweli kweli. Hatimaye ifikapo Novemba wananchi wanakwenda kupiga kura zao. Muda wote wa kampeni kuna vituko, kuna midahalo, kuna ulimi kutereza na hata kuna kupakana matope ili mradi mbinu zitumike ili kumnufaisha mwomba kura.
Sote tumesikia malalamiko ya Donald Trump kabla ya uchaguzi ule hata akafikia kutamka kama hatashinda yeye hatakuwa tayari kuyapokea matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu. Amekuwa na “confidence” sana juu yake mwenyewe. Amediriki kutamka wazi wazi atalishughulikia vilivyo suala zima la wahamiaji na wazamiaji hasa wa kutoka Mexico na nchi za waarabu. Ametamka wazi kuwa waafrika ni wavivu, wanasura mbaya, wanakimbia makwao kwa vile watawala wa nchi za kiafrika sio waaminifu ni wanyonyaji. Ametishia kujenga ukuta kutenganisha nchi yake na nchi ya Mexico. Anamsujudu Rais Putin wa Urusi kama mfano wa ushupavu na utawala bora.
Ni ajabu sana demokrasia ya Marekani. Bwana Donald Trump hakuwahi kuwa katika Serikali au niseme utawala yaani hakuwa Gavana wa Jimbo hivi au kuwa mwanasiasa na kufikia Useneta katika Congress. Ni utamaduni uliozoeleka kule Marekani, ili mgombea Urais akubalike angalau atokee katika kazi za kiserikali na pia awe amelitumikia taifa kwa kujitolea jeshini National service akaenda kupigana kule Vietnam au Korea au Vita Kuu ya II ile. Yote hayo hayumo. Yeye ni mjasilia mali tu na mfanyabiashara mashuhuri. Ana mapesa na anaitwa bilionea. Huruka kwa madege yake tu. Kacheza karata zake vizuri na leo ni Rais mteule wa Marekani.
Kutokana na utajiri wake huo bwana Donald Trump anayo jeuri ya fedha na ndiyo maana kasema wazi yeye siyo Rais NJAA, hivyo hatapokea MSHAHARA wa Urais. Hapo anatengeneza historia katika taifa lile. Anakuwa Rais wa kwanza Marekani mfanyabiashara. Na tena anakuwa Rais wa 3 nchini Marekani kutokupokea mshahara. Wengine waliomtangulia kukataa mshahara ni Rais wa 31 Herbert Clark Hoover 1929 – 1933) Rais wa 35, John Fitzgerald Kennedy (1960 – 1963) na huyu atakayekuwa Rais wa 45 Donald Trump 2017 – .
Mama Hilary Clinton, mwanamke wa kwana Marekani kugombea Urais alipatwa na mikasa. Kwanza ni yale matumizi ya barua pepe zake binafsi katika mambo ya Serikali – huu siyo utaratibu wa kiserikali popote duniani. Pili afya yake, tangu siku ile alipopatwa na kizunguzungu ikabidi asaidiwe kuingizwa katika gari na akahitaji mapumziko ya siku kadhaa kwa binti yake. Jambo lile la utete wa afya lilimpunguzia mvuto. Tatu kile kitendo cha FBI kutangaza wanazo barua pepe za mfanyikazi wa bibi Clinton kilimsulubu sana mama Clinton siku za mwisho mwisho za kampeni yake. Mpinzani wake alitumia taarifa ile kuonesha ukosefu wa utawala bora wa mama huyu katika kutunza siri za Serikali kiasi kwamba hata watumishi wake wanaweza kutumia barua pepe zao binafsi katika mambo ya kiofisi. Laiti huko mbele FBI wangemwona ana hatia basi angeweza kuondolewa katika madaraka yale ya Urais kwa kile kinachoitwa “IMPEACHMENT” By Congress kama ilivyotokea kwa Rais yule Richard M Nixon miaka ile ya nyuma.
Waamerika kadhaa wakabadili mawazo kwa kuhofia mama Clinton kweli anaweza kutenguliwa Urais wake. Hayo pamoja na nafikiri ile jinsia yake vilitosha kumpunguzia mama Clinton chati na akaukosa Urais. Imeonekana kitakwimu ni wanawake wachache sana walimpigia kura bibi Clinton.
Tarehe ya kura ilipofika 08 Novemba 2016 kila mtu alikuwa roho juu na kuwa na wasiwasi mkubwa. Wangoni tunasema “mitima nyenyema” kusubiria kuona nani ataibuka kidedea. Sina shaka wazo lile la Rais Obama kuwaomba wananchi wote wapenda demokrasia wajitokeze kwenda kutumia kura yao kumchagua wampendaye halikusikilizwa. Alisema hivi, namnukuu, “you’ve got to get into the area….. because democracy isn’t a spectator sport”. Kwa tafsiri yangu “hamna budi kuingia ulingoni maana demokrasia siyo mchezo wa kutazamwa”.
Maneno ya kuhimiza namna hii laiti yangefuatwa na wapiga kura wote, si ajabu matokeo yangalikuwa tofauti. Hebu tazameni kule Marekani, wananchi waliojiandikisha kupiga kura walikuwa watu milioni 231.5. lakini waliojitokeza kupiga kura zao walikuwa watu 128.8. Ndiyo kusema watu milioni 102. 7 hawakujitokeza kupiga kura zao. Hawa wote tuseme wangempigia kura mama Clinton mambo yangalikuwaje? Sijui hilo. Kule Marekanii pamoja na kuendelea kwao kidemokrasia lakini watu asilimia 55.6 tu ndio waliopiga kura tarehe 08/11/2016. Watu hawakuhamasika vya kutosha kujitokeza kupiga kura.
Kumbe tukilinganisha na uchaguzi wetu ule wa mwaka jana mwezi Oktoba 2015 hapa kwetu tunaona mwamko ni mkubwa wa walioitikia kujitokeza kupiga kura. Katika waliojiandikisha kupiga kura watu 23,161,440 wakajitokeza watu 15,596,110 basi hiyo ni asilimia 67.34 ni juu sana kulinganisha na waliojitokeza Marekani ambao walikuwa ni asilimia 55.6 tu. Hapo bwana tunaweza kujivunia hamasa yetu ya kujitokeza kupiga kura ilikuwa kubwa.
Lakini kule Marekani Rais hachaguliwi kama hapa kwetu kwa wingi wa kura tunaita “popular votes”. Utaratibu wa kule ni kwamba Rais huchaguliwa na kikundi maalum katika kila Jimbo. Hicho kikundi kinaitwa “Electoral College” hawa ni wawakilishi toka kila jimbo. Kuna idadi maalum iliyokubalika kikatiba yao. Basi hiyo Electoral College ina wajumbe 538 tu. Kikundi hiki wapo watu 435 wawakilishi kutoka majimboni, wapo watu 100 MASENETA na kuna wajumbe 3 wanatoka Wilaya ya Columbia. Ili uwe Rais Katiba inasema lazima mgombea apate kura 270 toka kundi hilo – hiyo ni zaidi ya nusu. Demokrasia namna hiyo iko Marekani tu ambako kuna kikundi maalumu cha wenye uwezo wa kumchagua Rais wa nchi ile.
Basi katika uchaguzi wa Novemba tarehe 8, 2016 hii bwana Donald Trump alijizolea kura 276 za hao Electoral College wakati mama Clinton alipata kura 232 tu ndiyo kusema baadhi ya hao wajumbe wa Electoral College hawakupiga hata kura sivyo? Hao ni wajumbe 508 tu wa hiyo Electroral College ndiyo walipiga kura. Je, wale wajumbe 30 mbona hawakupiga kura? Hata hao wajumbe 30 wote wangempigia bibi Clinton angepata kura 262 tu nazo zisingetosha kumpa urais mama huyu. Asiye na bahati habatishi.
Pamoja na mama Clinton kupata popular votes 60,274,974 wakati Trump alipata kura 59,937,338 na kwa kidemokrasia ya Marekani popular votes hazimweki Rais Madarakani, ndiyo sababu Mama Clinton akashindwa kuukwaa Urais wa Marekani.
Kutokana na hilo wazo la popular votes na kule kutokujitokeza kwa wengi kupiga kura ndiyo tunayoyaona matokeo ya watu eti kuandamana kumpinga mteuliwa. Jambo hilo halisaidii chochote.
Mambo muhimu ya kujifunza kutokana na uchaguzi ule wa Marekani ni kama haya: Chaguo la chama kule linaheshimika sana katika kuunganisha umoja na mshikamano wao kichama. Wote mademokrats na Mari publicans mgombea akishateuliwa kinachofuata ni NIDHAMU ya chama. Wote wanaunga mkono uteuzi na kumfanyia kazi huyo aliyeteuliwa na Chama.
Pili baada ya uchguzi kumalizika, Taifa zima linajumuika kujenga nchi yao. Hakuna suala la mikutano ya kampeni majimboni wala hakuna makundi au lugha za sijui kutokutambua matokeo ya uchaguzi. Hii ni nidhamu ya hali ya juu na ni uelewa mkubwa wa utawala wa sheria.
Katika kuteua mgombea kule hawana kitu “MWENZETU” tumetoka naye mbali katika siasa yaani hakuna KUBEBANA. Wale jamaa ni mastahili, uwezo na fedha vinakuwezesha kuwa kiongozi. Bwana Donald Trump hakuwa mmoja wa Magavana wala mmoja wa Maseneta kama ilivyozoeleka. Huyu ni mfanyabiashara na mtu wa nje ya Serikali (an outsider). Hili linataka uelewa mkubwa sana na demokrasia iliyopevuka.
Tujiulize haya maandaano tunayosikia katika miji na majimbo mbalimbali yanafaida kweli? Yanaweza kubadilisha matokeo ya uchaguzi? Kama wangalijitokeza kumpigia kura huyo waliyemkusudia sidhani kama sasa wangeweza kujitokeza kuandamana. Waingereza wana usemi huu. “What can’t be cured must be endured”! Yaani lisiloponyeka livumiliwe. Na waswahili tunasema, “majuto ni mjukuu”. Basi kuandamana kule kamwe hakutabadili Urais wa Marekani.
Sisi katika nchi zinazoendelea hapo tungesikia wanaharakati na Tume ya HAKI ZA BINADAMU wakilalama – waandamanaji wanakosewa haki zao za kibinadamu. Polisi wanatumia nguvu kupita kiasi. Je, kule Marekani mmesikia hayo yakidaiwa? Kwanini tusijiulize, Umoja wa Mataifa na haki zake za binadamu mbona wapo kimyaa kule? Kwa wakubwa suala la haki za binadamu halisemwi, lakini nchi za ulimwengu wa 3 au zinazoendelea, wazungu hao hao wanachochea tulaumu Serikali zetu.
Weupe wale wale huku wangetushauri kutuonesha namna haki za binadamu zinavyokiukwa na Serikali zetu. Je, kule Marekani Serikali za majimbo husika au Serikali ya Rais Obama mnasikia ikisemwa? Wananchi tuamke na tuone unafiki wa demokrasia ya Magharibi. Hakuna upuuzi huo wa wanaharakati au tume ya HAKI ZA BINADAMU kule Marekani.
Tujifunze maana ya demokrasia hapa duniani. Kama bibi Clinton alipata popular votes 60,274,974 wakati Trump alipata popular votes 59,932,338 kwa vigezo na mitazamo ya huku kwetu, bibi Clinton angelalamika kaonewa na Trump kabebwa. Hiyo ndiyo hali ya uafrika. Kumbe kule nchi za Magharibi Katiba ndiyo inatoa mwongozo Rais anapatikanaje na wala hatusikii malalamiko ya dhulma.
Wale wote waliokimdhania SIYE katika uchaguzi ule wa Marekani wameona kuwa ni NDIYE na yule wengi waliyemfikiria kuwa NDIYE kawa SIYE huko Marekani. Kwa hiyo kuandamana, kulia, kuotea mageuzi huwa ni KAZI BURE, Rais mteule Donald Trump ndiye sasa kesha ula. Wewe, mimi na mwingine yeyote yule duniani tupokee matokeo haya. Ndiyo uamuzi wa demokrasia ya Marekani huo.
Nchi za ulimwengu wa tatu hatuna utamaduni wa KUPOKEA matokeo na kuyakubali kwa kiingereza tunasema “to CONCEDE DEFEAT” na hivyo kuwa na ustaarabu na ushupavu wa kumpongeza mshindi alivyofanya bibi Clinton kule Marekani.
Kila uchaguzi katika nchi huwa ni funzo kwa wengine kujipima namna ya kuepa mapungufu. Laiti viongozi wa vyama, vya siasa wangebahatika kwenda Marekani wakashuhudia uchaguzi ule, ninaamini viongozi wetu wangekuja na mawazo ni badala ili tuboreshe chaguzi katika nchi zetu.
Demokrasia siyo mchezo wa kutazama tu bali ni utekelezaji unaomdai kila mtu kutenda. Sote tukipiga kura zetu, matokeo yanaweza kuwa tofauti sana na hivi inavyokuwa kama mamilioni ya waliojiandikisha wanashindwa kujitokeza kutumia haki yao. Kususa kupiga kura siyo demokrasia na ni kilele cha udikteta tu. Wala siyo njia sahihi ya kupata haki yao.
Niliwahi kuandika makala huko nyuma ikielezea je, Tanzania kuna demokrasia ya aina gani? (Tazama Jamhuri toleo 268 – 270 ya Novemba 2016) watanzania tusidanganyike na wale wanaotuambia tunabinywa na Serikali na Tanzania hakuna demokrasia. Tuwaulize tu ni wapi huko kwenye demokrasia safi isiyo na kasoro? Basi demokrasia ni mchezo wa wote kupiga kura kutoa kauli na wala siyo kusikiliza au kutazamia na kungojea wengine wanafanyaje.
Baada ya matokeo ya kura kunazuka madai ya kuonewa au kudhulumiwa. Ni kuingia ulingoni kupiga KURA mambo kwisha na demokrasia itafanya kazi yake. Wale wa maRSM Jeshi zamani katika makambi wakitunanga katika makambi kwa kusema “AKILI MUKICHWA” yaani tumia akili zako za kuzaliwa. Watanzania baada ya kuona uchaguzi wa Marekani, maandamano yanayofanyika kumpinga Rais Mteule Trump – hatusikii mataifa yakilaumu haki za binadamu kukiukwa basi tutumie AKILI zetu kujifanyia demokrasia yetu ya kitanzania.
Hao wanaharakati na wale wanaodai kuminywa kwa demokrasia hapa nchini, na wanasiasa uchwara sasa watambue uongo wa neno demokrasia. Ni wakati mwafrika awe “Liberated” kimawazo asiwe “His Master’s Voice” katika kuinanga demokrasia katika nchi yake. Magharibi hawathubutu kuichezea Serikali yao wala kuibeua. Donald Trump pamoja na vioja vyake vyote, kebehi zake zote watu matajiri na weupe wamemkubali. Ni demokrasia yao sisi tufuate yetu na wala tusiige ya Magharibi. Tuwe waafrika na hasa wazalendo wa Tanzania.
Mungu ibariki Tanzania. Dumisha uhuru na umoja.