Wazungu walipoasisi demokrasia wakaweka na misingi mitatu ya kanuni za demokrasia ambazo ni uhuru wa majadiliano, uhuru wa walio wengi kufikia uamuzi na uhuru wa utii wa uamuzi uliokubaliwa katika kikao.
Kadhalika walipotoa tangazo la haki za binadamu wakaweka vifungu vipatavyo thelathini vinavyoweka wazi haki za binadamu. Mathalani, haki ya kuishi katika uhuru, haki ya kulindwa na sheria, haki ya utaifa (uraia), haki ya kutoa mawazo na kujitetea mbele ya mahakama.
Si hivyo tu, wakasema iko haki ya kushiriki katika serikali ya nchi, haki ya kufanya kazi na kupata mahitaji muhimu, haki ya kupata elimu na huduma nyingine katika jamii, na kadhalika.
Tangazo hilo linataja pia wajibu alionao binadamu mmoja kwa binadamu wenzake katika jamii anamoishi ili kuleta maendeleo kamili na hali bora ya maisha yao wote. Hii ina maana kwamba binadamu hawezi kudai haki katika jamii bila kuwa na wajibu. Yaani wajibu kwanza, haki inafuata.
Katika lugha iliyo fasaha, uwe kiongozi, mtawala, mwanasiasa au mtetezi wa haki, kwanza timiza wajibu. Uwe umetabahari katika demokrasia, au uwe umetajiriba katika uongozi na utawala, au umetajididi katika utetezi wa haki ya mtu yeyote. Katika haya, upendeleo au uonevu hauna nafasi.
Baadhi ya wanasiasa na watetezi wa haki za binadamu katika Afrika hujikomba kwa Wazangu wasaidiwe kupata au kuwekwa madarakani katika nchi zao. Au kuwa na kinyongo na kufanya hiyana kwa viongozi waliopo madarakani. Katika mazingira kama haya ndiko kunakowapa wivu, hamaki na kiburi kufanya maasi na kusahau: “Achezaye na tope humrukia.”
Maasi hayo huvishwa vazi la mageuzi, au mabadiliko au mapinduzi baada ya kushonwa na kitambaa demokrasia, kudariziwa na nyuzi utawala wa sheria na kuwekwa vifungo haki za binadamu. Vazi ambalo linapendeza machoni na mwilini na kuwavuta vijana wa Afrika kulivaa kwa mikogo.
Wanasiasa wakongwe (vingunge) barani Afrika wanatambua athari ya vazi hili. Lakini baadhi yao kwa kukosa saburi, huwasukuma na kuwashawishi vijana kulivaa vazi hili, kwa maelezo kwenda na wakati na kutaka mapinduzi (mabadiliko). Ama kweli uzuzu hauna mwenyewe.
Katika lugha ya sayansi ya siasa, mapinduzi ni mabadiliko ya haraka katika jamii, mabadiliko ambayo yanawanyang’anya wachache madaraka waliyokuwa wakiyatumia kwa manufaa yao, na kuyaweka madaraka hayo mikononi mwa walio wengi.
Maasi ni kupinga mapinduzi. Ni mabadiliko ya haraka yanayowanyang’anya madaraka wananchi walio wengi, na kuwapa wachache, kwa madhumuni ya kuzuia maendeleo ya umma.
Hebu tuangalie ni kweli tawala za nchi za Afrika hazitekelezi utawala wa sheria na haki za binadamu: kama inavyoelezwa na baadhi ya wanasiasa, wanaharakati wa siasa na watetezi wa haki za binadamu ? Badala yake wanaminya kanuni hizo na kuzia. (kuwa na chuki na mtu au jambo fulani).
Iwapo jibu ndiyo, hawatekelezi. Ni sababu zipi au jeuri ipi zinazowapa nguvu na ujasiri kuacha kufuata misingi ya demokrasia na kanuni za haki za binadamu? Endapo jibu ni hapana, wanatekeleza. Ni sababu gani zinazowachochea wanasiasa hao na washirika wao kukejeli, kutoa matusi na kutaka kuleta maasi katika nchi?
Ni vema na ni busara pia kukumbuka nasaha isemayo: “Mchuma janga hula na wa kwao.” Mama Afrika anasema: “Kupanda mchongoma (si kazi), kushuka ndiyo ngoma.” Viongozi na vijana wa Afrika tunababaishwa na nini?
Kipi kinatusibu watoto wa mama Afrika hata kudiriki kwenda kwa Wazungu mikono nyuma au kifuani na kujidhalilisha na kilio shuu! Kuomba msaada watusaidie kuangusha tawala zetu na waje tena mchana kweupe kukomba mali zetu, kutunyanyasa na kutudharau utu wetu. Utu ni bora kuliko madaraka. Tutafakari.