Oktoba 17 mwaka huu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete atapokea tuzo nchini Uholanzi, barani Ulaya. Ni tuzo inayotokana na kuiwezesha nchi yake kushika nafasi ya kwanza barani Afrika  kwa kushamiri demokrasia. Hiyo nchi yake ni Tanzania.

Kwamba Tanzania ni nchi ya kwanza kwa kushamiri demokrasia barani Afrika hakuna anayeweza kuhoji. Na hakuna anayeweza kudai kwa haki kwamba Wazungu wametumia upendeleo katika kumpa tuzo hiyo. Sisi sote ni mashahidi. Tanzania  ni nchi ya demokrasia halisi.

Leo, Oktoba 7, ni bathdei (ukumbusho wa siku ya kuzaliwa) ya Rais Kikwete. Hapana shaka Watanzania wenye mapenzi mema kwa nchi hii wataungana  katika kumtakia heri Rais Kikwete. Wataungana pia katika kumpongeza kwa msimamo wake katika masuala mbalimbali, ulioleta heshima kubwa Tanzania.  Mwaka 2012 Tanzania ilikuwa  miongoni mwa kumi bora katika nchi  zilizoongoza kwa Utawala Bora barani Afrika. Na sasa Tanzania inaongoza bara zima kwa demokrasia.

Haya ni mafanikio makubwa ambayo Tanzania ina kila sababu ya kujivunia. Kama tujuavyo, dhana ya demokrasia ilichimbuka barani Ulaya katika nchi ya Ugiriki katika Vijiji vya Athens na Sparta.

Wanavijiji wa vijiji hivyo walijadiliana, wakapitisha uamuzi uliohusu maisha yao, na wakatekeleza walichoamua. Hizo ni kanuni tatu za demokrasia: majadiliano, uamuzi na utekelezaji.

Shuleni tulifundishwa kwamba neno “demokrasia”asili yake ni Kigiriki. Ni maneno mawili, demo na krasia, ambayo yana maana ya “utawala wa watu” Ni utawala uliowekwa na watu wenyewe. Kwa ujumla demokrasia ni uwezo na uhuru  wa watu kujiamulia mambo yao.

Demokrasia huendana na uhuru wa kusema na uhuru wa kuandika. Tuanzie hapo katika kuzungumzia nchi yetu mahali ilipofikia katika suala zima la demokrasia. Kwa upande wa uhuru wa kusema tujiulize. Ni nchi ipi nyingine barani Afrika  watu wana uhuru mkubwa wa kusema kama Tanzania?

Nchini Tanzania mtu anaweza  kusimama hadharani na kuutangazia ulimwengu kwamba anaitisha maandamano nchi nzima yasiyo na kikomo ambayo  yatashirikisha wafanyakazi wote. Katika nchi nyingine za Afrika mtu huyo asingepona. Angetiwa ndani tu. Angeonekana kuwa tayari amechochea machafuko nchi nzima lakini Tanzania  haina ubabe huo.

Na kwa upande wa magazeti mimi sikumbuki Rais mwingine nchini Tanzania  aliyeendelea kusemwa vibaya magazetini kama Rais Kikwete. Naye ameendelea kukaa kimya. Utadhani hayupo nchini Tanzania. Kumbe kuiwezesha nchi yako kuwa ya kidemokrasia yataka uwe na uvumilivu wa hali ya juu. Bila ya  uvumilivu utaendesha  nchi yako kidikteta. Na hiyo ndiyo hali halisi ya Afrika ya leo. Nchi nyingi zinaendeshwa kidikteta. Demokrasia imeshindikana.

Wakati tunakubali umuhimu wa nchi kuendeshwa kidemokrasia tunalazimika kukubali kwamba katika Tanzania ya leo demokrasia imepanuka na sasa imevuka mipaka  yake. Imevuka mipaka ya usalama. Iko ukanda wa hatari. Ukweli ni kwamba katika Tanzania ya leo demokrasia inavuruga umoja wetu, mshikamano wetu na heshima yetu. Demokrasia inatumika vibaya, tena vibaya sana.

Kwa kuwa kila mtu ana  uhuru wa kusema kila mtu anajifanya ni mjuaji. Hakubali hata kidogo analosema mwenzake. Kumebaki kulumbana, kukashifiana na kutukanana kwa mdomo, kwa simu na mitandaoni.  Demokrasia inapoteza umoja wetu na heshima yetu mmoja mmoja  na heshima ya viongozi na Taifa zima.

Tunawasema viongozi vibaya  kana kwamba si viongozi wetu. Leo si jambo baya tena  kuwasema vibaya viongozi wakati wote. Limekuwa jambo analofanya mtu kwa lengo la kujitafutia sifa. Na kweli anasifiwa. Leo gazeti  lisilowasema vibaya  viongozi wa nchi haliuziki. Kwa hiyo magazeti  yanashindana katika kuwaandika vibaya viongozi.  Gazeti linalojaribu kuwasifu au kuwapongeza viongozi wakuu wa Serikali pale  wanapofanya vizuri,  linaonekana gazeti lisilo na faida kwa umma. Tumefikia hapo.

Demokrasia imepanuka na imevuka mipaka yake. Kwa sasa, badala ya viongozi kuwa madikteta ni wananchi walio madikteta. Wanailazimisha Serikali ifanye wanavyotaka wao. Serikali, kupitia Jeshi lake la Polisi, wanapotumia nguvu zaidi ikipambana na waasi na wakaidi, watu hulalamika kwamba polisi wanatumia nguvu zaidi. Inakubalika kwamba kulalamika  ni sehemu ya demokrasia. Lakini pia tunalazimika  kujiuliza; hivi ni nguvu ya kiwango kipi tunachotaka polisi watumie wanapopambana na waasi na wakaidi?

Ukweli ni kwamba  wale wanaolalamika wakati polisi wanapochukua hatua dhidi ya wahalifu na wakaidi, wanawaunga mkono wahalifu na wakaidi. Wanashabikia uhalifu na ukaidi. Demokrasia nchini  Tanzania imefika huko.  Demokrasia katika Tanzania ya leo  imefika mahali ambapo wahalifu na wakaidi wana wafuasi wasio na idadi kuliko wakati wowote katika historia ya Tanzania.

Watanzania wanaoitakia  mema Tanzania wamefika mahali ambapo sasa   wanasema kwamba rais ajae lazima awe dikteta. Tumetumia vibaya demokrasia iliyoimarishwa na Rais Kikwete na sasa watu wanaomba nchi iwe ya kidikteta. Huko nyuma halikuwa jambo la kawaida viongozi kusemana vibaya. Lakini  leo ni jambo la kawaida. Demokrasia imepanuka na imevuka mipaka yake. Viongozi wanatumia demokrasia kwa kuvunjiana heshima.

Kwa  upande wa asasi (mashirika) za kiraia malengo ya kuanzishwa  kwake yalikuwa kusaidia Serikali katika kuhudumia wananchi kiuchumi na kijamii. Leo, karibu asasi zote za kiraia ni mwiba. Zinaongoza mapambano dhidi ya Serikali  na chama tawala. Zimeacha kutimiza majukumu yake. Ni matokeo mengine ya kupanuka demokrasia hata imevuka mipaka yake.

Ukipita mitaani kwenye meza za magazeti, majarida na  vitabu  ndiyo utakubali kwamba demokrasia  nchini Tanzania  imepanuka na sasa imevuka mipaka  yake. Majarida na vitabu vingi tu vinaandika kwa wazi kabisa matusi na mambo yasiyoendana na maadili. Ni matokeo ya kupanuka demokrasia. Hata wizara  inayosimamia utamaduni  inaacha mambo yaende yanavyokwenda.

Ukisikiliza nyimbo za taarab na za bongo fleva  utakubali pia demokrasia imepanuka  na sasa imevuka mipaka yake. Nyimbo zimekosa maadili.  Ukiangalia mavazi ya vijana wetu — wa kiume na wa kike — utakubali demokrasia  ilivyochangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa maadili na kudhoofika kwa utamaduni wa Mtanzania. Vijana wanatumia vibaya uhuru wao.

Lakini  tayari Tanzania  imetumia fedha nyingi katika kutafuta vazi la Taifa. Nani  atavaa vazi la Taifa katikati ya Taifa ambalo tayari limepoteza utamaduni wake wa Taifa? Kwa kifupi, hatutafuti vazi la Taifa. Tunatafuta vazi la viongozi. Tumechelewa kutafuta vazi la Taifa.

Kuna wakati Tanzania ilifuta mashindano ya uzuri  ambayo miaka hii yanaitwa “Mashindano ya urembo ” ama “Miss Tanzania” au “Miss Utalii.” Ulikuwa utawala wa  Rais Julius  Nyerere uliofuta mashindano hayo  baada ya kuonekana kwamba hayaendani  na maadili ya Watanzania.

Azimio  la Arusha, hata kama limekufa, lilitaka jambo la maana sana. Liliwataka Watanzania waishi  kama Watanzania. Kwa hiyo, kuanzia wakati huo Watanzania waliheshimu mambo yao ya asili. Likawa jambo la kawaida  kukuta ngoma za Watanzania kwenye kumbi za burudani.  Leo ngoma za Watanzania  hazionekani tena mijini. Labda utaziona uwanja wa ndege katika mapokezi ya mgeni. Nafasi ya ngoma za Watanzania  imechukuliwa na bongo fleva.

Kampuni za bia  na za  simu za wageni  hazikupoteza wakati. Zinatumia  fedha nyingi kuzungusha vijana wa bongo fleva nchi nzima  katika kuhakikisha kwamba ngoma  za asili  za Watanzania zinafutika kabisa katika uso wa Tanzania.

Kuna hili Tamasha la Sanaa (na ngoma za asili) linalofanyika Bagamoyo kila mwaka. Kwa kuwa lengo la wageni ni kufuta kabisa  utamaduni wa Mtanzania,  wanatumia fedha nyingi kufadhili bongo fleva. Lakini hawatumii hata shilingi moja  kufadhili Tamasha la Bagamoyo. Hiyo ni demokrasia.

Lakini kinachotakiwa sasa  ni Serikali  kuwashtukia hawa wageni  waliokazana kufuta utamaduni wetu. Tumepanua mno demokrasia na sasa imevuka  mipaka hata ukoloni  mamboleo umepata nafasi  ya kuvuruga utamaduni wetu  kama ulivyofanya  ukoloni mkongwe.

Wakati umefika kwa Serikali kuthamini  chake. Itenge fedha kwa ajili ya kufadhili  Tamasha la Sanaa la kila mwaka la Bagamoyo.

Na kwa upande wa mashindano  ya urembo hapa pia wageni  wanashirikiana na wananchi  waliokosa uzalendo katika kudhoofisha maadili ya Mtanzania. Wageni wanatumia fedha nyingi kupeleka wasichana wetu Hifadhi za Taifa  huku wasichana hao wakiwa wamevaa sketi fupi (vimini).

Demokrasia imegeuza matakwa  ya Azimio la Arusha lililotutaka Watanzania tuishi  kama Watanzania. Sasa tunaishi kama Wazungu. Lakini hatuwezi kuwa Wazungu.

Katika haya yote  hatuwezi kumlaumu Rais Kikwete  kwa kuimarisha demokrasia katika nchi yetu. Rais aliamua kuimarisha demokrasia kama chombo cha kuharakisha maendeleo yetu. Badala yake tumetumia vibaya uhuru wetu wa kusema na uhuru wetu  wa kutenda. Ndiyo maana  hata Bunge la Katiba limeleta aibu kwa Taifa letu ambapo  wajumbe walitumia wakati mwingi kukashifiana.

Na sasa Bunge Maalum la Katiba limepitisha Katiba. Lakini wale wasiokubali kushindwa wanatumia demokrasia kusema maneno mbalimbali. Wanasema kwamba Bunge la Katiba limehonga baadhi ya wajumbe. Lakini hawasemi majina ya waliohongwa. Wanadai kura zimechakachuliwa. Lakini hawatoi ushahidi. Wanasema kupitishwa kwa Katiba kutasababisha machafuko Tanzania. Wanatumia demokrasia kutuweka roho juu.

Hakika demokrasia imepanuka  na sasa imevuka mipaka yake. Tujisahihishe.