Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Rufiji
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Michael Gwimile ametaka kamati za ujenzi kuwalipa kwa wakati mafundi wa miradi mbalimbali ya maendeleo .
Ameyasema hayo wakati akikagua miradi inayotekelezwa na Serikali ikiwemo majengo ya shule ,katika kata ya Utete,Mgomba, Chemchem na Umwe.
“Kitu ambacho sisi hatutaki ni kwamba tusianze kutengeneza madeni mapya ,kama hela imekuja kwa ajili ya mradi na hawa watu wapo site wawe wanalipwa kwa wakati:'” Hakuna haja ya kuwakopa unakuta jengo linaisha tunaanza kufuatana Halmashauri, haiwezekani” amesitiza Gwimile.
“Nyie wakuu wa idara ni na usimamizi wa kamati , Injinia, Mtu wa Elimu, Manunuzi ni kuishauri kamati ndo kazi yenu, tusiiiamulie tuishauri” ameongeza.
Wakizungumza baada ya ukaguzi huo Wananchi wanaoishi maeneo hayo wamesema wameridhishwa na namna wanavyoshirikishwa katika kamati za Ujenzi .
Suna Idd Mtulia Mkazi wa Kata ya Mgomba ambae pia ni mjumbe wa kamati ya Ujenzi wa shule mpya ya msingi Mgomba,aliishukuru Serikali kuwajengea shule hiyo ambayo kukamilika kwake kutaondoa adha ya watoto kusafiri umbali mrefu.
Alieleza changamoto kubwa ilikuwa wanaoishi Kijiji Cha Mpima ambapo wanatembea kilometa 3 na wengine wanaotoka Mapwegele wanatembea kilomita 6 kwenda Shule.
Mtulia ameieleza,kwasasa wanashukuru Mpima kuwa na Shule kwani watakuwa wamepata shule yao ,kadhalika na wanaotoka Mapwegele pia kuna Shule inajengwa kwahiyo changamoto itapungua na kubaki historia.
Akielezea fursa zinazopatikana kutokana na Ujenzi wa shule hizo Abdallah Makongora, Mkazi wa Chemchem alisema uwepo wa miradi hiyo unachangia kutoa fursa za ajira na uwepo wa shughuli na kujipatia kipato.
“Sasa hivi wageni wapo wengi, Dada zetu wamejenga migahawa hapa, vijana nao pia tunapata visenti na ajira, unakuja kufanya kazi hapa unapata chochote kitu” amesema Makongora.
Ali Kisongo alibainisha, wameridhishwa na ushirikishwaji”sisi tunaotoka kwenye jamii ya kawaida tupo kama wanne tukishirikiana na viongozi wengine kutoka idara mbalimbali za Kiserikali, kwahiyo tafsiri yake ni kwamba tuligawanywa kwenye kamati kuu mbili mimi mwenyewe nikiwa kwenye kamati ya mapokezi”