Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Halmashauri ya Mji Kibaha, mkoani Pwani imetoa muda wa lala salama kwa kaya zaidi ya 130 zilizovamia shamba namba 34 ambalo ni mali ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mitamba kata ya Pangani.

Halmashauri hiyo, imewataka waanze kutoa mali zao katika maendelezo ya makazi waliyojenga kinyume cha sheria na atakaekaidi bomoabomoa itamkumba.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kibaha Mshamu Munde, ametoa rai hiyo katika kikao maalum na waandishi wa habari,kilichofanyika Ofisini kwake, Kibaha ,mkoani Pwani.

“Tunatumia ustaarabu kwanza ,uungwana ,kuna watu walishapewa notisi ya siku saba 22,novemba mwaka 2022 ,waanze kutoa mali zao kwa hiari kabla ya kuondolewa kwa nguvu na kuharibiwa mali na kusababisha kupata hasara”.

“Kaya zaidi ya 130, maeneo yatakayovunjwa yapo mengi ambayo wamiliki hawajulikani ,Ila yapo maeneo yatakayobakia wazi na kuna taasisi za Serikali zitabakia ikiwemo Mitamba na zitakazonunua maeneo yaliyopangwa”ameeleza Munde.

Munde amefafanua, watakaobaki maeneo yao ya makazi yatarasimishwa na watalazimika kulipa bei ya soko.

“Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilipewa shamba la hekta 4,000 sawa na ekari 10,000 na Wizara ilikubali kuipatia Halmashauri ya Mji wa Kibaha kiasi cha hekta 2,963 bila malipo yeyote na Wizara ikabaki na hekta 1,037. “

“Jumla ya wananchi 1,556 walilipwa fidia yao kwa awamu kuu nne kati ya mwaka 1988-1991″alibainisha Munde.

Oktoba 13 mwaka 2023, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge alifika Mitamba kuzungumza na wananchi na kutoa maagizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na waliovamia shamba namba 34 waondoke mara moja.

Agizo jingine ilitoa muda kwa Jeshi la Polisi na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani, kufanya uchunguzi kwa vinara na viongozi 24 wakiwemo wa mitaa,watendaji wa mitaa na wataalamu wanaodaiwa kujinyakulia milioni 900 kwa kuuza kitapeli maeneo hayo, na atakaebainika achukuliwe hatua za kisheria.


Vilevile aliwaagiza wataalamu wa halmashauri ya Kibaha Mjini kupima na kuweka alama eneo hilo na wananchi walioendeleza maeneo yao kuondoa maendelezo yao .

Mpimaji Ardhi Halmashauri ya Mji Kibaha, Aron Shushu, ameeleza kiwanja hicho kimepimwa upya kwa kuzingatia sheria namba 8 ya mipango miji na mwaka 2021 kilifanyika kikao na wananchi hao kwa ajili ya kutoa katazo la kutovamia shamba hilo.