Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Kamshna Jenerali wa Mamlka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA),Aretas Lyimo amesema, mamlaka hiyo imedhamiria kutoa elimu zaidi kwa Watanzania kuhusiana na dawa za kulevya ili wawe na uelewa wa pamoja kuhusu aina ya dawa za kulevya, athari zake na hatua za kisheria zinazowakabili wanaojihusisha na matumizi au biashara ya dawa hizo nchini.
Ameyabainisha hayo Julai 6, 2023 katika banda la DCEA, mamlaka hiyo inashiriki Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba kuanzia Juni 28, 2023 hadi Julai 13, 2023 ndani ya viwanja vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (SabaSaba) vilivyopo Barabara ya Kilwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
“Tupo hapa Sabasaba na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ina banda lake katika viwanja hivi vya Sabasaba.
“Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwa wananchi juu ya athari ya dawa za kulevya, aina ya dawa za kulevya, lakini pia sheria zinazoongoza mamlaka na sheria pia zinazoongoza wale ambao wanakamatwa na dawa za kulevya.
“Hukumu zake zikoje, ili sasa kuwafanya wananchi waweze kuelewa sheria zetu zipoje, lakini pia waweze kupata elimu ya kutosha kuhusiana na dawa za kulevya.
“Lengo ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa wa kutosha, ili kuhakikisha na wao wanakuwa walimu wetu mitaani huko, kwa ajili ya kufundisha wenzao na watu waweze kujiepusha na dawa za kulevya.
“Lakini tuweze kupiga vita kwa pamoja dhidi ya dawa za kulevya nchini, kwa sababu dawa za kulevya zinaathari kubwa sana nchi,ikiwemo zinaharibu uchumi wetu, zinaharibu jamii, lakini pia zinaharibu myororo mzima wa uchumi.
“Kwa sababu pia nguvu kazi ya vijana ndiyo wajenzi wa Taifa, lakini sasa unakuta wengi ndiyo wanangukia kwenye dawa za kulevya.
“Lakini pia, sasa hivi wanafunzi walio wengi wa shule za msingi, sekondari na vyuo ndiyo wanaoangukia kwenye matumizi ya dawa za kulevya, kwa hiyo unakuta zinaharibu pia Taifa letu kwa kutokua na elimu ya kutosha,kwa kuwa na watu ambao wengi wanaishia kuharibu afya zao kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.
“Lakini pia, wananchi watusaidie kuhakikisha tunafanya operesheni kwa pamoja, kwa lengo la kuhakikisha watu wanaepukana na dawa za kulevya, lakini pia sisi mamlaka tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba tunatokomeza dawa za kulevya nchini ili kuweza kujenga uchumi wetu imara na tutaendelea kufanya operesheni mbalimbali nchi nzima.
“Vile vile si Sabasaba peke yake, lakini pia kwenye matukio mengine yakiwemo matamasha mbalimbali ambayo yanafanyika nchini, tutaendelea kutoa elimu ili wananchi nchi nzima waendelee kupata elimu kuhusiana na dawa za kulevya.
“Ipo mikoa ambayo imekithiri kwa kilimo cha bangi, mfano Arusha, Mara, Morogoro na Ruvuma, Ruvuma huko kuna maeneo wanalima sana bangi, lakini ukienda pia Iringa, lakini pia kuna mikoa ambayo imekithiri kwa kilimo cha mirungi, mfano ukienda Tanga na Kilimanjaro ambako kote huko tunaenda kutoa elimu.
“Lakini pia kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo tunakwenda kufanya utafiti ili kuja na mazao mbadala ya kulima katika maeneo hayo, umeona pia Arusha na Mheshimiwa Rais (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan) ametoa ahadi kwamba atahakikisha Wizara ya Kilimo inafanya utafiti kuewezesha mazao mbadala ili waepukane na kilimo cha bangi.
“Lakini pia Serikali itajenga miundombinu ya barabara, watapelekewa maji, lakini pia mmemsikia Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi ile asilimia 10 ya mikopo kutoka halmashauri, pia wataona namna ya kuitumia ili wale vijana ambao wameingia kwenye dawa za kulevya na wameamua sasa kuacha, na wameshapata nafuu waipate sasa ili waangalie cha kufanya.
“Ka sababu wengi baada ya kuacha dawa za kjulevya na kupata dawa na kurudi katika hali ya kawaida, wengi hawana kitu cha kufanya kwa hiyo mwisho wa siku wanarudi tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya, lakini ile asilimia 10 ya halmashauri sasa hivi itatumika kwao, unaangaliwa utaratibu mzuri wa namna ya kuwakopesha wale vijaa ili iwe kama mitaji yao.
“Ya kuunda kuunda vikundi na kuweza kuzalisha mali, ili wasirudi tena kwenye dawa za kulevya, changamoto kubwa ambayo tunakutana nayo ni kwamba jamii kama jamii ya Watanzania bado hawajachukua jukumu lao kmuweza kuelimisha watu kuhusiana na athari na ubaya wa dawa za kulevya.
“Kwa hiyo, wazazi wengi hawachukui jukumu lao hilo la kuwaelimisha na kuwalinda watoto wao, kwa hiyo bora wazazi na walezi wote wangechukua jukumu lao la kuwaelimisha watoto wao na kuhakikisha hawaingii kwenye dawa za kulevya ili tatizo lisingekuwepo.
“Lakini pia wale viongozi ambao wapo katika jamii husika, viongozi wa kimila, viongozi wale wa chini kuanzia ngazi ya vijiji, vitongoji, na kupanda juu kila mtu kwa nafasi yake, viongozi wa dini, jamii kwa ujumla na viongozi wote kila mtu kwa nafasi angekuwa anakemea ili tatizo na kuhakikisha kwamba ili tatizo linapotokea mahali wanachukua hatua.
“Hili tatizo lisingekuwa kubwa hivyo, kwa sababu unakuta kwenye mtaa kuna kijiwe cha wauzaji wa dawa za kulevya, na jamii inawajua, lakini pale watu hawachukui hatua na hawatoi taarifa ili wale watu ambao wanajihusisha na dawa za kulevya waweze kukamatawa na kuchukuliwa hatua.
“Kwa hiyo jamii kutojihusisha na kukemea dawa za kulevya, ndilo linalokuza tatizo kubwa la dawa za kulevya nchini, kwa hiyo niwaombe watu wote kila mtu kwa nafasi yake ahakikishe anakemea dawa za kulevya nchini,”amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Ustawi wa Jamii
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) katika Divisheni ya Kinga na Tiba, Bi.Sarah Ndaba amesema, lengo la wao kuwa katika maonesho hayo ni kuifikia jamii ili iweze kutambua majukumu yao.
“Tupo hapa viwanja vya Sabasaba kupeleka ujumbe kwa jamii juu ya kazi zetu tunazozifanya yaani kazi kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA). Sisi kama maafisa wa jamii tuliopo hapa DCEA Divisheni ya Kinga na Tiba kazi yetu ni kuziratibu asasi za kiraia zinazofanya kazi ya udhibiti wa dawa za kulevya.
“Lakini, pia tunazisimamia nyumba za upataji nafuu ambazo kwa sasa zipo 50 Tanzania bara, tunaziratibu katika kuhakikisha kwamba, kama wanafuata Mwongozo wa Uanzishaji na Uendelezaji wa Nyumba za Upataji Nafuu Tanzania Bara.
“Kwa sababu ni lazima wafuate mwongozo wa kuendesha nyumba za upataji nafuu, lakini pia hizi asasi za kiraia zinatusaidia kupeleka ujumbe kwa jamii,pamoja na kutoa elimu kutoka kwenye shule za msingi mpaka kwenye jamii kupitia Mwongozo wa Utoaji Elimu juu ya Dawa za Kulevya.
“Mbali na hilo tuna MAT Kliniki (Medically Assisted Therapy-MAT au vituo vya tiba saidizi kwa waraibu kwa kutumia dawa), tuna takribani MAT Kliniki 15, kati ya hizo 11 zikiwa ni MAT Kliniki kubwa na nne zikiwa ni MAT Kliniki ndogo.
“Zipo katika mikoa kadhaa Tanzania Bara na hizi MAT Kliniki zinawasaidia waraibu kupata methadone, tuna asasi za kiraia ambazo zinasaidia kuwaratibu hawa waraibu na kuwapeleka MAT Kiliniki kupata hizo hudum,”amebainisha Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) katika Divisheni ya Kinga na Tiba, Bi.Sarah Ndaba.