Na Alex Kazenga, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewasihi watumishi wa forodha kuzifanyia ukaguzi wa kina bidhaa zinazoingizwa na kutoka nchini, ikidaiwa wahalifu wa dawa za kulevya huzitumia kuvusha skanka; JAMHURI linaripoti.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam Septemba 10, 2024 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, ambapo pamoja na mambo mengine amesema operesheni waliyoifanya Agosti 28, 2024 hadi Septemba 02, 2024 imefanikiwa kunasa kilo 1,815 za skanka zikihusisha mtandao wa watu watano.

“Tunawasihi wananchi washiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara hii haramu.

“Aidha, watumishi wanaofanyakazi katika vituo vya forodha vya mipakani hususani wanaohusika na ukaguzi wa magari na bidhaa zinazoingia na kutoka nchini waendelee kuwa makini wanapotekeleza majukumu yao kwani wahalifu wa dawa za kulevya hubuni mbinu za kuficha kwenye bidhaa ili kuzisafirisha,” amesema Lyimo.

Ni kwa mkatadha huo, Lyimo amesema operesheni waliyoiendesha Magomeni na Mbezi Luguruni jijini Dar es Salaam, imewasaidia kumkamata wakala wa kupokea na kusambaza skanka nchini ikiwa ni pamoja na kuibaini nyumba ya kikongwe ulimo kuwa umefichwa mzigo wa skanka.

Wakala wa skanka aliyekamatwa na DCEA ni Richard Henry Mwanri (47) mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Mkonde wilayani Kinondoni na Felista Henry Mwanri (70), mkulima na mkazi wa Mbezi Luguruni, aliyekutwa na mzigo.

Wahusika wengine wa mzigo huo ni Athumani Koja Mohamed (58), mfanyabiashara na mkazi wa Tanga, Omary Chande Mohamed (32) dereva bajaji na mkazi wa Buza pamoja na JumaAbdallah Chapa (36) mkazi wa Kiwalani jijini Dar es Salaam.

“Katika operesheni hii tumefanikiwa kukamata pia gari aina ya Mitsubishi Pajer lenye namba za usajili T 551 CAB na bajaji yenye namba za usajili MC 844 CZV.

“Huyu Richard Mwanri amekuwa akipokea dawa za kulevya kutoka nchi mbalimbali na kuziingiza nchini kwa usafiri wa magari zikiwa zimefichwa kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine kisha kusambazwa kwa wauzaji wengine katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema Lyimo.

Katika siku za hivi karibuni amesema dawa za kulevya ina ya skanka zimekuwa zikikamatwa mara kwa mara akiitaja kuwa aina ya bangi ya kusindika yenye kiwango kikubwa cha kemikali yenye sumu aina ya Tetrahydrocannabinol (THC).

Kemikali hiyo anasema inaouwezo wa kuharibu mfumo wa fahamu, akili na kusababisha magonjwa yasiyoambukiza kama vile moyo, figo n aini.

“Matumizi ya skanka kwa wajawazito yanaweza kusababisha madhara kwa mtoto aliyetumboni ikiwemo kuathiri maendeleo ya ubongo wa mtoto na kuzaliwa na uzito mdogo,” amesema Lyimo.

Anaongeza kuwa kwa mujibu wa ripoti ya hali ya dawa za kulevya ya dunia iliyotolewa Vienna nchini Australia Juni 26, 2024 maeneo yaliyohalalisha matumizi ya bangi, uzalishaji wa bidhaa zenye bangi, kiwango kikubwa cha kemikali ya sumu ya THC kimeongezeka kwa watumiaji wa bangi katika nchi hizo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo katika mataifa hiyo pia kumekuwa na ongezeko la watu wanaohitaji tiba, kuongezeka kwa idadi ya watu wenye matatizo ya akili pamoja na wanaojaribu kujiua.

Please follow and like us:
Pin Share