Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata watu watano wakiwa na kilogramu 1,815 za dawa za kulevya aina ya Skanka.

Watu hao wamekamatwa maeneo ya Luguruni Mbezi na Magomeni jijini Dar es Salaam katika operesheni iliyofanyika Agosti 28 hadi Septemba 2, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi na habari leo Septemba 10 jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amewataja watuhumiwa hao ni Richard Mwanri (47) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Makonde na Felista Mwanri (70) mkulima na mkazi wa Luguruni Mbezi ambaye ni mmiliki wa nyumba zilipokutwa dawa hizo za kulevya.

“Watuhumiwa wengine ni Athumani Mohamed (58) mfanyabiashara na mkazi wa Tanga, Omary Mohamed (32) dereva bajaji na mkazi wa Buza na Juma Chapa (36) mkazi wa Kiwalani.

“Richard Mwanri ni mhalifu ambaye amekuwa akipokea dawa za kulevya kutoka nchi mbalimbali na kuziingiza nchini kwa usafiri wa magari zikiwa zimefichwa kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine kisha kusambazwa kwa wauzaji wengine katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema.

Amebainisha kuwa katika opesheni hiyo, gari aina ya Mitsubishi Pajero yenye namba za usajili T 551 CAB na bajaji yenye namba za usajili MC 844 CZV vilikamatwa.

Aidha amesema Mamlaka hiyo itaendelea kuwa macho na kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya wote wanaoharibu nguvu kazi taifa kwa kujihusisha na dawa za kulevya kwa namna yoyote ile.

Vilevile, Kamishna Lyimo ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.

“Watumishi wanaofanya kazi katika vituo vya forodha vya mipakani husussani wanaohusika na ukaguzi wa magari na bidhaa zinazoingia kutoka nchini, waendelee kuwa makini wanapotekeleza majukumu yao kwani wahalifu wa dawa za kulevya hubuni mbinu za kuficha ili kusafirisha dawa za kulevya,” amesisitiza

Please follow and like us:
Pin Share