Na Prisca Libaga, JamhuriMedia,Arusha
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wilayani Arumeru pamoja na Taasisi muhimu zinazohusika wakati wa zoezi la uteketezaji wa vielelezo vya dawa za kulevya kwa mujibu wa sheria imeteketeza gunia 21 za bangi kavu katika dampo la maji ya chai lililopo wilayani Arumeru katika Mkoa wa Arusha.
Gunia hizo 21 za bangi kavu zilizoteketezwa zilikamatwa pamoja pia na uteketezaji wa ekari 81 za bangi zilizokuwa zimepandwa katika mashamba ya nafaka ya maharage na mahindi ambapo watuhumiwa wanne waliohusika na gunia hizo walikamatwa wakati wa operesheni hiyo iliyotekelezwa tarehe Mei 11, 2024 na DCEA Kanda ya Kaskazini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya ya Arumeru katika Kijiji cha Engutoto Kata ya Mwandet iliyopo wilayani Arumeru katika Mkoa wa Arusha.
Wakati wa uteketezaji wa vielelezo hivyo kwa mujibu wa sheria, Afisa Sheria wa DCEA Kanda ya Kaskazini Benson Mwaitenda kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa DCEA alitoa rai kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha kuachana na matumizi, usafirishaji na kilimo haramu cha bangi sababu sheria zipo na ni kali kwa watuhumiwa watakaojihusisha na dawa za kulevya kwani wanaweza kufungwa hadi kifungo cha maisha jela.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi wa DCEA Kanda ya Kaskazini Bi. Sara Ndaba wakati wa uteketezaji wa vielelezo hivyo alieleza kuwa DCEA Kanda ya Kaskazini itaendelea kutoa elimu kwa umma juu ya madhara ya tatizo la dawa za kulevya na kuhakikisha makundi yote yanafikiwa katika maeneo yote ya ukanda wa Mikoa ya Kaskazini.