Na Mwandishi Maalum, JamhuriMedia, Katavi
Mkuu wa wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi Bw. Onesmo Mpuya Buswelu tarehe 4 Juni, 2024 amefikishwa mbele ya Baraza la Maadili kwa tuhuma za ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Bw. Buswelu anatuhumiwa kwa makosa mawili ambayo ni matumizi ya lugha chafu dhidi ya watumishi wa umma na kukamata watu na kuwaweka ndani kinyume cha sheria.
Kikao cha kusikiliza tuhuma dhidi ya kiongozi huyo kimefanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Jaji (Mst.) Rose Teemba na mjumbe wa Baraza hilo Bw. Peter Ilomo.
Wakili wa Serikali Bw. Hassan Mayunga emelieleza Baraza kuwa mlalamikiwa wakati akitekeleza majukumu yake ya kikazi amekuwa akitumia lugha chafu na matusi kwa watumishi na watendaji wa serikali wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika kinyume na kifungu cha 6(1)(a) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Bw. Mayunga alisema, “Mhe. Mwenyekiti mlalamikiwa wakati akiteleza majukumu yake ya kikazi amekuwa akiwakamata na kuwaweka mahabusu wananchi, watumishi wa umma na watendaji wa serikali wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika kinyume na kifungu cha 6(1) (c) cha Sheria iya Maadili ya Viongozi wa Umma.”
“Kushindwa kutimiza wajibu huo wa kisheria ni ukiukwaji wa maadili ya viongozii wa umma kwa mujibu wa kifungu cha 6 (2) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma,” alisema.
Upande wa mlalamikaji uliwaleta mashahidi watatu ambao ni Bw. Leonard Kansimba, Afisa Uchunguzi wa Sekretarieti ya Maadili, Bw. Raymond Bernard, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kakoso, wilayani Tanganyika anayedai kutolewa lugha ya matusi na mkuu huyo wa wilaya na Bw. Primo Amadeo Kampamba, fundi ujenzi kutoka Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika aliyelieleza Baraza kuwa Mkuu huyo wa Wilaya alimuweka mahabusu bila kufuata taratibu.
Mlalamikiwa ambaye ni mkuu wa wilaya ya Tanganyika ameyakana mashtaka yote mawili na kudai mbele ya Baraza kuwa tuhuma zote anazotuhumiwa nazo ni za kutengeneza kwasababu amekuwa akisimamia vizuri utekelezaji wa miradi ya maendeleo wiyani humo kwa kuhakikisha fedha za miradi zinatumika ipasavyo bila ubadhilifu wa aina yoyote.
“Katika kutenda kwangu kazi kama mkuu wa wilaya ya Tanganyika sijatumia lugha chafu na za matusi kwa watumishi na watendaji wa wilaya.” Alisema na kuongeza kuwa, kazi hizi za ukaguzi wa miradi sijazifanya peke yangu, nilikuwa na viongozi wengine wa Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.
“Kwa ukaribu na udhibiti huo, imepelekea wanaodhibitiwa kutofurahi,” aliliambia Baraza huku akitokwa na machozi.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Mwenyekiti wa Baraza alimueleza mlalamikiwa kuwa, “tumesikiliza pande zote, sasa liachieni Baraza lifanye upekuzi na tathmini kama kutakuwa na chochote mamlaka yako itakujulisha.”