Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka amelazimika kutembea zaidi ya kilometa 5 ndani ya maji baada kuzungukwa wakiwa katika harakati za kusaidia kuokoa wananchi waliopata mafuriko kufuatia kujaa mto Miombo baada kupokea maji mengi kutoka milimani.
Awali Mkuu wa Wilaya na Wajumbe wa kamati ya Usalama walifika eneo ambalo daraja linalounganisha vijiji vitatu katika Kata ya Nyameni Zombo ambalo limechukuliwa na maji na kusababisha huduma za usafiri na usafirishaji kusimama.
Hata hivyo wakati wakitoka eneo hilo wakajikuta wamezungukwa na maji na kulazimika kuanza kutembea kujinusuru sambamba na kuwasaidia wananchi wengine ambao bado walikuwa katika makaazi yao.
Mafuriko hayo yaliyosabibishwa na mvua kubwa zilizonyesha milimani,hakuna athari za kibinadamu zilizotokea zaidi ya kuharibu miundo mbinu ya madaraja, barabara na makazi ya wananchi ambapo zaidi ya kaya 120 zimeingiliwa na maji.