Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kupitia wataalam wake kwenda kubomoa kitaalamu majengo ya madarasa matano ya shule ya Msingi Kalemane iliyopo kwenye Kata ya Maore baada ya kuezuliwa na upepo ulioambatana na mvua.
Hivyo kuhatarisha usalama wa wanafunzi na ajengo mengine endapo hatua za haraka hazita chukuliwa katika shule hiyo iliyojengwa tangu mwaka 1975 ambapo kuta zake zimeonekana kukosa uimara na uwezo wa kupauliwa upya hali inahatarisha usalama wa wanafunzi walio katika shule hiyo.
Akizungumza mbele ya watalaamu mbalimbali wa Halmashauri hiyo MKuu wa Wilaya Kasilda Mgeni amesema mvua zinazo endelea kunyesha huenda zikasababisha majengo hayo kuanguka kabisa na kwa hali ilivyo majengo hayawezi kutumika tena.
“Niagize Mhandisi wa Halmashauri aje haraka kwa ajili ya kumalizia kubomoa kuta za Majengo haya matano kwa utaalam ili kuwe na Usalama wakati tukiendelea na mipango mingine ya kujenga majengo ya madarasa mapya,”amesema.
Aidha amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kuchukua tahadhari, kwa kuhama kwa muda katika maeneo yenye historia ya kujaa maji unapofika msimu wa Mvua kuepuka madhara zaidi yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha wilayani humo.