Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Bagamoyo
KATIKA kukabiliana na changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara, Serikali Wilayani Bagamoyo, imelielekeza uongozi wa shirika la umeme Tanesco Wilayani humo kuwa na siku moja ya kukata umeme kwa ajili ya matengenezo yasiyo ya dharura ili kuondoa kero kwa wateja.
Aidha Serikali ya Bagamoyo, imelitaka shirika hilo kuacha tabia ya kukata umeme mji mzima wakati wakifanya matengenezo na badala yake wakate katika eneo husika ili kuondoa usumbufu.
Halima Okash ambae ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,akitoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM kuanzia Julai -Desemba 2023 ,ameeleza wananchi wanatamani kufaidika na sekta ya nishati labda itokee dharura kubwa na Yale yaliyo ndani ya uwezo wa kushughulikiwa yafanyiwe kazi.
Okash amesema, endapo kunatokea hujuma zozote hawatavumilia watashughulikia kwa kufuata taratibu husika na tayari Meneja wa awali Tanesco wilayani hapo amebadilishwa.
Alieleza katika sekta ya nishati , Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya umeme na kutatua changamoto zinazojitokeza,ambapo katika kipindi hicho imetoa kiasi cha sh.milioni 519.2 kwa ajili ya usambazaji wa umeme Halmashauri ya Chalinze na Bagamoyo.
Hata hivyo inaendelea kumaliza mradi wa ujenzi wa kituo cha kupooza umeme Chalinze, mradi ambao umegharimu sh. bilioni 128 na umefikia asilimia 93.2.
“Kituo hiki kitapunguza changamoto ya ukosefu wa umeme kwenye maeneo ya wilaya ya Bagamoyo na nje ya wilaya “ameeleza Okash.
Katika viwanda , Okash alifafanua kwamba wilaya inaendelea kutoa fursa kwa wawekezaji kwenda kuwekeza na hadi sasa wilaya ina jumla ya viwanda 245 vikiwemo vikubwa 16 .
Kuhusu mifugo na uvuvi amesema , Halmashauri ya Bagamoyo imetenga milioni 31 kutoka vyanzo vya ndani kununua boti ambayo inakwenda kuwa mkombozi kwa uokoaji wakati wavuvi ama kukitokea majanga ya kuzama pamoja na kudhibiti uvuvi haramu na kufanya doria kuzuia njia za panya
Mkuu huyo wa wilaya alieleza sekta ya elimu , wilaya ilipokea bilioni 3.4 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa,matundu ya vyoo , mabweni ,majengo ya utawala na fedha bila malipo .
Sekta ya afya ilipokelewa bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya na ununuzi wa vifaa tiba ,ambapo zimejengwa hospital mbili na vituo 10 na zahanati.
Okash alieleza, sekta ya maji imetolewa bilioni 4.9 kwa ajili ya miundombinu ya maji ambapo kwasasa upatikanaji wa maji Safi na salama katika wilaya ni asilimia 84 na watu 439,520 wanapata maji.
Okash hakusita kuzungumza juu ya masuala ya migogoro ya ardhi,kama wilaya inaendelea kupambana na migogoro ya ardhi na wameshatatua asilimia 75 , asilimia 25 ya migogoro hiyo ipo kwenye mhimili wa mahakama.
Okash alitaja, changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni kutopata fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wakati, Mwamko mdogo Kwa wananchi kuchangia miradi ya maendeleo na kutopata mafundi wa uhakika kwa kufuata muongozo wa utekelezaji kuwa mingi kwa wakati mmoja.
Kadhalika, amezingumzia namna wilaya ilivyojipanga kwenye uchaguzi wa Serikali za vijiji vitongoji na mitaa na uchaguzi mkuu,na kusema utakuwa wa haki kwa kupata viongozi Bora na kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo.
Awali Mwenyekiti wa CCM Bagamoyo Alhaj Abdul Sharif, alihimiza wenye sifa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Alikemea makundi,chuki na rafu wakati wa kuelekea kwenye chaguzi hizo ,na amesisitiza Umoja na Mshikamano ili kuimarisha chama.