Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Nyasa

MKUU wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Peres Magiri amesema kuwa ,usimamizi mbovu wa vyanzo vya mapato kutoka kwa baadhi ya wataalam na watendaji wa vijiji na kata umesababisha Halmashauri hiyo kushindwa kufikia malengo ya makusanyo ya ndani jambo ambako linasababisha kutoka lipa madeni kwa wakati kutoka kwa wazabuni na watumishi.

Mkuu huyo wa Wilaya Magiri, amesema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na watumishi na madiwani kwenye kikao cha robo ya nne cha Baraza la madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo.

Amesema kuwa, kutokana na Halmashauri hiyo kuwa na hali mbaya katika ukusanyaji na usimamizi wa vyanzo vya mapato ni jukumu la kila mmoja kusimamia kwenye eneo lake badala ya kutumia muda mwingi kukaa maofisini na amewaagiza kuwa lazima wawe na kumbukumbu nzuri ambazo zitakuwa zinaelezea nini halmashauri hiyo inafanya na si vinginevyo.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Peres Magiri akizungumza kwenye kikao Cha Baraza la madiwani kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.

Magiri amesema kuwa,Wilaya ya Nyasa ina vyanzo vingi vya mapato ikiwemo zao maarufu la kahawa lakini kuna watendaji waliopo maeneo mbalimbali kuto wajibika ipasavyo kwa madai kwamba wao hayawahusu na rasimu ni Moja ya taratibu zilizopo ili kukwamisha mambo yasiende kwenye halmashauri hiyo.

“Kwa hili la ukusanyaji wa mapato katika katika halmashauri yetu kuwa na hali mbaya mmenisikitisha sana nawaagiza viongozi wenzangu pamoja na madiwani ,Mkurugenzi ,watalaamu na watendaji tuchukuweni hatua za pamoja kusimamia makusanyo ya mapato na kwa wale watakaobainika kwenda kinyume na maagizo haya wachukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kuwasimamisha kazi bila kuwaonea haya’’ amesema Magiri.

Aidha amewaagiza wataalam hao kujitathimini namna ya utendaji wao wa kazi lakini pia wanatakiwa kufanya mapitio ya kodi ,tozo ushuru na utunzaji wa kumbukumbu sambamba nakuimarisha mfumo wa ukusanyaji na kuhakikisha makusanyo yote yanakusanywa kwa kupitia mfumo wa kielektroniki ili kudhibiti upotevu wa mapato.

Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa wakiwa kwenye kikao cha Baraza.