Kuna taarifa iliyoripotiwa na Gazeti la JAMHURI toleo la Machi 22, 2015 ikiwa na kichwa cha habari: “Barua ya wazi kwako Rais John Magufuli (1)”.
Barua hiyo ilikuwa na mambo kadha wa kadha yaliyoutuhumu uongozi wa Wilaya ya Ngorongoro na Mkoa wa Arusha, hususani Kamati za Ulinzi na Usalama na kuhusishwa na mgogoro wa mipaka kati ya kijiji cha Naan na Kisangiro.
Katika barua/taarifa hiyo niliyoisoma nimebaini kuna hoja kubwa nne ambazo ni:-
*Serikali ya Wilaya ya Ngorongoro inawalinda wahamiaji haramu kutoka Kenya wakishirikiana na asasi zisizo za kiserikali (NGO’s) na hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahamiaji haramu hao wanaoishi Wilaya ya Ngorongoro.
*Kutokuheshimiwa kwa mipaka iliyowekwa na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka mwaka 2013.
*Rushwa inavyosababisha kupuuza kuondolewa kwa wavamizi (wahamiaji haramu).
*Mkuu wa Wilaya kuwaambia wananchi wa Kisangiro kuwa hawawezi kupata haki hata waende wapi.
Hivyo, mimi kama Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya nimeona ni busara kutoa ufafanuzi wa hoja hizo kwa umma ili kuepusha upotoshwaji wa taarifa.
Ikumbukwe kuwa Februari, 2015 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Jakaya Kikwete alifanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya sanjari na uteuzi wa wakuu wa wilaya wapya. Hivyo wilaya ya Ngorongoro ilikumbwa na mabadiliko hayo na hivyo kupata mkuu wa wilaya mpya.
Mimi Hashim Mgandilwa nilipata uteuzi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro mnamo Februari 18, 2015 na kuapishwa Machi 2, 2015 nikimpokea aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hii, Mheshimiwa Elias Wawa Lali.
Baada ya kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wangu (DC Mstafu Mhe. Wawa Lali) nilienda Dodoma kwa ajili ya semina elekezi na wiki ya mwisho ya Machi nilirudi kuanza kazi rasmi.
Katika taarifa iliyoandikwa kwenye Gazeti la Jamhuri ilitoa tuhuma hizo na kutoa mifano mbalimbali ya mambo yaliyofanywa na Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa wakati huo.
Yaliyoripotiwa ni kipindi ambacho mimi Hashim Mgandilwa- Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa sasa nilikuwa bado sijateuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya hii.
Kwa mfano, zimezungumzwa tuhuma za mwaka 2013 pamoja na Januari 14, Januari 16 na Januari 28, 2015. Vilevile hata wajumbe wa kamati yangu ya ulinzi na usalama walibadilishwa kipindi hicho hicho (mfano OCD, DSO na DIO). Lakini taarifa hizo zimeripotiwa kama uongozi ni ule ule na hakuna mabadiliko yoyote kwenye uongozi huo.
Hata hivyo, baada ya kuanza kazi rasmi nikishirikiana na Kamati yangu ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kipaumbele changu kilikuwa kwenye mambo makubwa matatu ambayo ni wahamiaji haramu, kuimalisha usalama pamoja na kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi.
JITIHADA TULIZOCHUKUA
Wahamiaji haramu
Machi 31, 2015 niliongoza operesheni ya kuwasaka wahamiaji haramu nikishirikiana na wajumbe wangu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na kikosi cha kupambana na ujangili.
Operesheni hii ilikuwa ya siku 12. Jumla ya wahamiaji haramu 17 walikamatwa kutoka Kenya wakiwa na mifugo zaidi ya 3,500. Kati yao walikuwapo watatu waliokuwa na umri chini ya miaka 18 ambao walikabidhiwa kwa wazazi wao. Watuhumiwa wengine walifikishwa mahakamani- kati yao; sita walikiri makosa mahakamani na walitumikia kifungo cha miezi sita kila mmoja. Wanane walitozwa faini.
Habari hii ilichapishwa katika Gazeti la Jamhuri la Aprili 22, 2015 na kurudiwa Februari 24, 2016.
Hata hivyo, ikumbukwe Aprili 2015 Kamati ya Ulinzi na Usalama ilifunga mnada wa Kalkamoro uliokuwa umeanzishwa kienyeji kwa lengo kuingiza mifugo na baadaye kuitafutia malisho sanjari na watu hao kuweka makazi yao hapa nchini kinyume cha sheria.
Septemba 12 hadi Oktoba 3, 2015 tulifanya tena operesheni nyingine ya kuwasaka na kuwaondoa wahamiaji haramu. Kazi hii haikufanikiwa kama tulivyotarajia kutokana na kuwa kipindi hicho kilikuwa cha kampeni za Uchaguzi Mkuu hivyo tulikosa msaada kutoka kwa viongozi wa kisiasa. Tukiwakamata watuhumuwa watano wakiishi nchini kinyume cha sheria. Wote walifikishwa mahakamani na kutozwa faini kati ya Sh 50,000 na Sh 300,000 kwa mujibu wa sheria za nchi.
Jitihada za Kamati ya Ulinzi na Usalama hazikuishia hapo. Kuhusu uwepo wa matrekta mengi kutoka Kenya yanayoingia kufanya kazi za kulima bila kufuata taratibu za nchi yetu, hatua zimechukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa.
Novemba 26, 2015 tulifanya operesheni na kuyakamatwa matrekta matano yaliyoingizwa nchini bila kibali na watuhumiwa wote walifikishwa mahakamani. Wawili walitozwa faini ya Sh 500,000 kila mmoja na watatu walitozwa faini ya Sh 700,000 kila mmoja.
Hatua hizi zinadhihirisha kuwa serikali ya wilaya na kamati yangu ya ulinzi na usalama imekuwa ikichukua hatua zinazostahili dhidi ya wahamiaji haramu na si kama inavyoelezwa kuonekana kama tunawalinda watu wanaoingia nchini bila kufuata taratibu.
Kuimarisha amani na usalama
Katika hili, mimi kama Mkuu wa Wilaya nikishirikiana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama katika kipindi cha Aprili 2015 tulifanya mkutano wa hadhara kwenye vijiji vya Kisangiro na Naan ambako miongoni mwa ajenda ilikuwa kujadili masuala ya usalama katika maeneo yenye migogoro ya ardhi, hususani eneo la Gibladi.
Tuliwaasa wawe na utulivu wakati serikali inalishughulikia na tukaahidi kuzikutanisha serikali za vijiji vyote viwili ili tukubaliane kwa pamoja. Baada ya hapo nilifanya juhudi za kuwatafuta na kuwakutanisha wenyeviti wa vijiji kabla ya kuzikutanisha halmashauri za vijiji. Kati ya vijiji hivyo, mwenyekiti wa kijiji kimoja hakuwa tayari kwa kukaa na kujadiliana kuhusu na mgogoro huo.
Hata hivyo, Wilaya ya Ngorongoro ina changamoto ya kuwa na silaha nyingi zinazosababisha kuwa na matukio ya mauaji ya mara kwa mara. Silaha hizi inasadikika zinatolewa Kenya. Kupambana na hili, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ikishirikiana na mkoa Februari 24, 2016 iliagiza silaha zote zisalimishwe kituo cha polisi.
Hadi sasa tumefanikiwa kukusanya silaha 96 na kazi inaendelea. Kati ya hizo silaha; 90 zilizokuwa zinamilikiwa kihalali zimepokewa Kituo cha Polisi Wilaya ya Ngorongoro ila matumizi yake hayakuwa sahihi. Silaha sita za kivita zilizokuwa mikononi mwa watu kinyume cha sheria zilitelekezwa. Miongoni mwa silaha hizo ni SMG (2), AK47 (1), SAR (1), G3 (1) na Mark 4 (1).
Haya yote yanafanywa na Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro wanaishi kwa amani na usalama, lakini pia kutimiza azma ya Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhakikisha Ngorongoro inatawalika na kuwa na amani kama ilivyo maeneo mengine ya Tanzania.
Ufumbuzi wa migogoro ya ardhi
Ikumbukwe Februari 10, 2016 tulifanya kikao cha wadau wote kutafuta suluhu ya migogoro eneo la Loliondo. Kikao kingine kilifanyika Februari 20, 2016 katika Ofisi ya Tarafa ya Sale iliyopo Kata ya Digodigo. Kilihusisha viongozi wa kimila, wenyeviti wa vijiji, madiwani na watu maarufu- lengo likiwa wananchi kuheshimu mipaka iliyowekwa kwenye vijiji.
Lakini pia kubainisha na kuweka mpaka unaonekana wazi kati ya tarafa za Sale na Loliondo.
Februari 21, mwaka huu kulitokea sintofahamu ya kuripotiwa kwa matukio mawili ya kujeruhiwa kwa mkazi wa Kijiji cha Naan na mauaji ya watu watatu wa jamii Kisonjo katika Kijiji cha Kisangiro. Kamati ya Ulinzi na Usalama ilienda kwenye vijiji hivyo na kutuliza hali iliyokuwapo na kuimarisha ulinzi ili kusitokee ulipaji kisasa.
Hitimisho
Kwa maelezo haya machache yaliyotolewa hapo juu naomba kupingana na hoja zilizotolewa na mwandishi wa barua hiyo kwani kamati yangu ya ulinzi na usalama iliyopo sasa imekuwa makini na ikitenda shughuli zake kwa weledi wa hali ya juu pasipo kuonea mtu na kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake kama mtanzania na anafurahia kuishi na kuwa raia mwema wa Tanzania.
Mwisho naomba kutoa mwito kwa jamii ya Ngorongoro, tuitunze amani na tuendelee kuwafichua wale wote wanaomiliki silaha kinyume cha taratibu ili kupunguza na kuondoa kabisa matatizo ya utekaji na utumiaji wa silaha katika matukio ya kihalifu.
Pia nashauri vyombo vya habari kujiridhisha kabla ya kuchapisha habari zao kwa kuzungumza na mamlaka husika ili kuepusha kutoa taarifa zisizojitosheleza kwa jamii na kusababisha kuchochea migogoro zaidi.
Imetayarishwa na:
Hashim Mgandilwa
Mkuu wa wilaya
Ngorongoro