Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songwe
MKUU wa wilaya ya Ileje, mkoani Songwe Farid Mgomi, amewaasa watanzania kuendelea kudumisha na kuimarisha amani, upendo, umoja na mshikamano ikiwa ni Tunu ya msingi wa Maendeleo katika Taifa la Tanzania lililoasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Hayati Sheikh Abeid Aman Karume.
Akizungumza leo Desemba 9, 2024 katika Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara lililofanyika katika Ukumbi wa Coommunity Center wilayani hapo, DC Mgomi amehimiza wananchi kuendekea kuzienzi Tunu zilioachwa na Mwasisi wa Taifa hili ambapo kupitia upendo, amani, umoja na ushirikiano Taifa la Tanzania litazidi kusonga mbele katika Nyanja zote za maendeleo na kuwa mfano bora kwa Mataifa mengine.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ametoa pongezi kwa watumishi katika Wilaya hii kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidi na kuhakikisha Wilaya ya Ileje inasonga mbele kimaendeleo.
Aidha amewasisitiza watumishi kuendelea kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa kwa kila Mtu, hii ikiwa ni pamoja na kutoa huduma kwa wananchi pasipo kujali itikadi ya wananchi, dini, kabila au rangi.
Pia DC Mgomi amewasisitiza wananchi wa Wilaya hii kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania ili Amani, umoja na mshimano viendelee kudumu katika nchi yetu.