Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songwe
MKUU wa Wilaya ya Ileje, Mkoani Songwe, Farida Mgomi, amewaasa wananchi wa Wilaya hiyo kuungana, na kushirikiana kwa pamoja kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia, kwa kukemea na kushirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha jamii inabaki salama dhidi ya vitendo hivyo.
Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya Kampeni ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia wilayani hapo, ambapo alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, DC Mgomi ametoa wito kwa Wananchi kubadilika na kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwani vinarudisha nyuma ustawi wa jamii na kuzorotesha uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Aidha amewasihi wazazi kuwalinda Watoto kwa kuwapa malezi stahiki yanayozingatia maadili ya Kitanzania ili kuwaepusha watoto kuiga Tamaduni za nje ambazo zinakiuka miiko ya maadili ya Nchi yetu.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ameziasa familia kudumisha Upendo na kuepuka Migogoro sambamba na kutumia fursa zilizopo katika wilaya hiyo ili kujiongezea kipato kitakachowasaidia kutunza na kulea familia.
Pia DC Mgomi ametoa rai kwa jeshi la Polisi kupitia dawati la jinsia kuendelea kushirikiana na wananchi kwa kutoa elimu kuhusu Ukatili wa kijinsia na kuchukua hatua stahiki kwa wale wole watakaokutwa na hatia ya kujihusisha na vitendo vya ukatili wa Kijinsia.