Na Manka Damian, Jamhuri Media,Mbeya

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa amewataka vijana wasomi kutumia elimu walizopata katika vyuo mbalimbali hapa nchini kubuni miradi na kuifanya bila ya kuwa na ulazima wa uwepo wa fedha ilimradi kama watakuwa waaminifu.

Malisa amesema kuwa vijana ni nguzo muhimu katika maendeleo hivyo elimu walizopata ziende zikawe msaada kwao katika kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja na kujenga uaminifu na kujiamini ili kuendesha maisha yao kupitia fursa mbalimbali kutoka serikalini .

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa

Malisa amesema hayo April 28,2025 wakati wakati akifungua kongamano la vijana wasomi kutoka kata mbili za Nsalala na Utengule Usongwe mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi wilayani Mbeya waliokutana katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya kwa mwito wa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Erica Yegella.

“Na hapa kuna tatizo kubwa kwenye eneo hili (la vijana) kwa sasa suala la uaminifu kwa vijana wengi ni tatizo kubwa yaani ukifika getini kwa mtu ukiingia tu unaanza kuangalia hivi hii nondo haiwezi kutoka hapa! Ndio maana mtu akija hapa kutoka Kenya anafungua Hotel yake anaona bora achukue wa-Kenya au achukue watu wa nchi anayotoka kwasababu vijana wengi wamekosa uaminifu”, amesema Malisa.

Erica Yegella ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mbeya amesema ameamua kuwaita vijana hao wasomi wa ngazi na tasnia mbalimbali ili kuwaonyesha namna ambavyo Halmashauri yake ya Mbeya ina fursa mbalimbali kwao (vijana) ikiwemo mikopo ya asilimia nne kwa kundi hilo ili kujiimarisha kiuchumi kupitia miradi wanayoifanya kwa mtu mmoja mmoja au kwa kundi la vijana.

“Nimewaita vijana hapa ili muweze kuona fursa mbalimbali zilizopo katika Halmashauri yetu ili muweze kuzitumia nyie vijana tunaamini ni nguzo kuu katika maendeleo hivyo tumieni fursa tulizonazo katika Halmashauri yetu “amesema mkurugenzi huyo.

Mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii Halmashauri ya wilaya ya Mbeya Agness Elkunda, amesisitiza suala la uaminifu kwa vijana kwa kurudisha mikopo yao kwa wakati na kwa uaminifu ili kunufaisha wakopaji wengine.

Baadhi ya vijana wamesema wamenufaika na kongamano hilo na kuushukuru uongozi wa Halmashauri ya Mbeya kwa kuwaonyesha fursa mbalimbali hasa za kiuchumi ambazo wanaweza kuzitumia vyema katika kujiletea maendeleo.

“Tunashukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hii Erica Yegella kwa kutufumbua macho yetu ,sisi ni vijana wasomi lakini fursa nyingi tulikuwa hatuzijui katika Halmashauri yetu hii lakini Sasa tumeamka tutafanya kwa kuaminifu mkubwa.