Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kisarawe

BAADHI ya maeneo kata ya Kiluvya wilayani Kisarawe, mkoani Pwani ikiwemo Makurunge, Majumba Sita wamelalamikia ukosefu wa maji hali inayosababisha kutumia maji ya bwawani na wanafunzi kubeba kupeleka shule ili kukabiliana na kero hiyo.

Akizungumzia kero hiyo, katika mkutano wa hadhara ulioitishwa eneo la Kiluvya Madukani na mkuu wa Wilaya ya Kisarawe,Petro Magoti ,mkazi wa Makurunge,Meri Charles alieleza, hawana maji kabisa kwenye eneo hilo.

“Ukosefu wa maji unatupa shida,tunatumia maji yasiyo salama kifua,tunachota maji bwawani, wanafunzi nao wanapata tabu kubebelea maji lita tano kupeleka shule ili kutumia kwa ajili ya usafi na matumizi mengine ya shule”alifafanua Meri.

Kutokana na malalamiko hayo ,Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Magoti aliwasiliana kwa njia ya simu na Waziri wa Maji Juma Aweso ambapo aliahidi kupeleka wataalamu Kata ya Kiluvya ili kufanya tathmini ya maeneo yenye changamoto ya maji.

Alielezea ,atatuma timu itakayofanya kazi hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata maji na kuondokana na changamoto za ukosefu wa maji.

“Ombi lenu nimelisikia natuma timu itakuja kufanya tathmini kwa yale maeneo ambayo yana changamoto hivyo msiwe na wasiwasi tutatatua shida hiyo,”alisema Aweso.

Magoti aliwaasa wananchi ,wawe na uvumilivu kwani Serikali imewasikia na kwa kushirikiana kero hiyo itapatiwa ufumbuzi.

“Suala la maji ni jambo muhimu hivyo lazima lishughulikiwe kwa uharaka ili kuondoa changamoto ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kumtua mama ndoo kichwani.

Nae Meneja wa DAWASA Emanuel Mbwambo alieleza ,mpango uliopo ni kuhakikisha mwezi wa Agosti baadhi ya maeneo yenye changamoto yanafikiwa na huduma ya upatikanaji wa maji.