Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia Kilombero

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya amesema Serikali haitawafumbia macho watu watakaohusika kudhoofisha jitihada za kulinda na kuhifadhi Pori la Akiba Kilombero ambalo ni mahsusi kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vya maji, misitu na wanyamapori hususani upatikanaji wa maji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme katika mradi wa kimkakati wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Akizungumzia umuhimu wa kuhifadhi Hifadhi hiyo Januari 3, 2024 wilayani humo, Wakili Kyobya amekemea vikali tabia ya watu wachache wanaowalaghai wananchi kulima na kuchunga mifugo ndani ya hifadhi pamoja na kuwauzia maeneo kwa ajili ya kilimo.

“Imetokea tabia ya watu kwenda kuwashawishi wananchi kwamba maeneo ya hifadhi yanaruhusiwa kulima na kuchunga mifugo, nasema maeneo ya hifadhi hayaruhusiwi kwa shughuli zozote za kibinadamu isipokuwa zile zinazoruhusiwa kisheria” amesema wakili Kyobya.

“Lakini kuna wengine wanawatapeli wananchi Kwa kuwauzia maeneo ndani ya Hifadhi, nimuombe OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) pamoja na Kamati ya usalama ya wilaya kuendelea kufuatilia kwa ukaribu na wale wote watakaobainika wanawadanganya wananchi, wanawalaghai, wanawatapeli Kwa njia moja ama nyingine tutachukua hatua” amesisitiza Mhe. Kyobya.

Aidha Wakili Kyobya ametoa wito kwa viongozi wa Wilaya yake kuongeza ulinzi katika Pori la Akiba Kilombero na kuweka utaratibu mzuri wa kuwapokea wananchi wanaohama kutoka ndani ya Hifadhi hiyo hasa katika maeneo yaliyo pembezoni mwa Hifadhi kama vile Mofu, Idete, Mawala, Chombe na Mgeta.

Maeneo mengine aliyoyataja ni pamoja na Chita, kalengakyelu, Chisano Ching’anda, Mlimba, Utengule na mengine yanayozunguka hifadhi huku akisisitiza kuwa imani na nia nzuri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan isiharibiwe na watu wachache.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba Jamal Idrisa Abdul amemshukuru Rais wa Dkt. Samia kwa kulipandisha hadhi Pori la Akiba Kilombero na kusisitiza kuwa kazi iliyobaki ni kuhakikisha Halmashauri kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) wanailinda na kuihifadhi Hifadhi hiyo sambamba na kurejesha uasili wake.

Mkurugenzi huyo amesema mpaka sasa kazi kubwa wanayoendelea nayo ni kuhakikisha wananchi hawaendelezi shughuli za kibinadamu katika hifadhi hiyo.

Kwa upande wake Kamanda wa Pori la Akiba Kilombero Bigilamungu Kagoma amesema tangu Hifadhi hiyo ipandishwe hadhi TAWA imeendelea na zoezi la uwekaji vigingi ili kuifanya mipaka ya Hifadhi kuonekana na kutambulika vizuri na wananchi ambapo mpaka sasa zaidi ya vigingi 1,100 tayari vimekwisha wekwa.