Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Chato
MKUU wa Wilaya ya Chato mkoani Geita kwa kushirikiana na Taasisi ya Mtetezi wa Mama wilaya hiyo,wametembelea gereza na kutoa msaada wa sabuni,mafuta na taulo za kike kwa wafungwa na mahabusu waliopo kwenye gereza la wilaya hiyo,ikiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali za kuhudumia jamii.
Mbali na msaada wamechangia damu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato ili kusaidia matibabu ya wagonjwa wenye uhitaji wa huduma hiyo muhimu.
Akikabidi msaada kwa magereza hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhandisi Deusdedith Katwale, amesema msaada huo umetokana na michango ya wananchama wa taasisi ya mtetezi wa mama ambao wameguswa na mahitaji ya wafungwa na mahabusu ili kuwapa matumaini ya kuwa bado wao ni sehemu ya jamii.
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwataka wadau wengine wa maendeleo kuguswa na uhitaji wa makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo wafungwa na mahabusu ambao baada ya adhabu zao wanatarajiwa kurejea uraiani wakiwa watu wema na wazalendo kwa taifa lako.
Mbali na kuipongeza taasisi hiyo,ameitaka kupanua wigo wa kuendelea kuyaeleza mazuri yote yanayotekelezwa na serikali chini ya rais Samia Suluhu Hassan, na kwamba hatamvumilia mtu yoyote atakaye taka kukwamisha jitihada za taasisi hiyo.
“Taasisi yenu ni halali kwa sababu imesajiliwa kisheria na ninawapongeza kwa kujipambanua kumtetea mheshiwa rais Samia na kuyaeleza wazi mambo mengi mema anayowatendea watanzania, niwahakikishie kuwa ofisi yangu itaendelea kuwapeni ushirikiano mkubwa na milango ipo wazi wakati wote” amesema Katwale.
Kadhalika amewataka kutokatishwa tamaa na na wote wenye nia ya kubeza kazi nzuri zinazotekelezwa na serikali ya awamu ya sita huku akidai baadhi ya madiwani wamekuwa wakimpigia simu kutaka kujua uhalali wa shughuli za taasisi hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa taasisi hiyo,Monica Magadula, amesema kuwa msaada huo umelenga kuonyesha upendo na mshikamano kwa wahitaji wakiwemo wafungwa na mahabusu wa kike ambao wanahitaji kuwa na hedhi salama licha ya uwepo wao gerezani.
“Sisi kama taasisi ya Mtetezi wa mama tumeona ipo haja kwetu kuunga mkono jitihada za serikali kwa kutoa damu kwa ajili ya wagonjwa pamoja na kutoa misaada hii kwa wafungwa na mahabusu lakini jambo kubwa zaidi ni pale tulipogundua wafungwa wa kike hawapati taulo za kike wawapo gerezani ili kuwa na hedhi salama.
Kaimu mkuu wa Magereza hiyo, SP. Antony Michael,ameshukuru kwa msaada huo huku akiahidi kuufikisha kwa walengwa kama ilivyokusudiwa na kwamba jamii haina budi kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali ikiwa ni pamoja na kuonyesha upendo kwa wafungwa na mahabusu.