Na Mwandishi Wetu, JamhiriMedia, Iringa
MKUU wa wilaya ya Iringa, Herry James, amesema kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia itasaidia kuondoa migogoro iliyopo ya uelewa mdogo wa haki za binadamu, mila na desturi kandamizi, vitendo vya ukatili wa kijinsia, pamoja na imani za kishirikina zinazoawakabili wananchi wa mkoa huo.
Alitoa kauli hiyo juzi alipomwakilisha mkuu wa mkoa wa Iringa kufungua mafunzo ya wajumne wa kamati ya usalama ya elimu ya uraia na utawala bora inayoratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria.
Alisema mkoa huo wa Iringia ni miongoni mwa ambayo imepata fursa ya kufikiwa na Kampeni hiyo ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayofanyika kwa siku 10 katika mikoa minne na kwamba inapaswa kutumika vizuri kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwapo kwa muda mrefu.
Alisema, mafunzo kwa wajumbe hao yatasaidia kuwajengea uwezo viongozi katika ngazi mbalimbali za utawala ili kuhakikisha wunazingatia misingi ya utawala bora, haki za binadamu, na demokrasia kwa vitendo wakati wanatoa huduma kwa wananchi hususani namna ya kupata haki katika mambo yao.
James alisema mafunzo hayo yanahusisha wajumbe wa Kamati za Usalama za Mkoa na Wilaya, baadhi ya wataalam wa Halmashauri, na Watendaji wa Kata zote za Mkoa wa Iringa.
“Kwa hiyo binafsi kwa mkoa wetu huu wa Iringa, kampeni hii pamoja na mafunzo vimekuja kwa wakati muafaka na tunaamini yatakuwa ni msaada mkubwa kwetu kwenye shida ambazo zimetusumbua kwa muda mrefu, tuitumie kwa manufaa,”alisema James.
Alitoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kushirikiana kutatua changamoto hizo kwa kushirikisha maarifa watakayopata huku akiwataka viongozi na watendaji wa mkoa huo wa Iringa kushiriki kikamilifu kuhamasisha wananchi kutumia huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa bure kupitia kampeni yake inayoendelea.
James aliwahimiza washiriki kuhakikisha kuwa maarifa yatakayotolewa yanakuwa chachu ya mabadiliko katika utendaji wao wa kila siku.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa elimu hii inasambazwa kuanzia ngazi ya familia hadi sehemu za kazi ili kujenga jamii yenye haki, amani, na utawala bora,” alisema James.
“Ni vema mkatumia mafunzo haya kuleta tija na mafanikio kwenye jamii yetu na tutumie vema kampeni hii ya msaada wa kisheria kutatua matatizo yaliyopo kwenye jamii yetu.”