DAR ES SALAAM
Na Regina Goyayi
Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Dayna Nyange, yupo nchini Nigeria akiandaa nyimbo kadhaa zitakazokuwa kwenye EP (extended playlist) yake mpya.
Akizungumza na JAMHURI, msanii huyo wa kike ambaye yupo kwenye mikakati ya kurejesha heshima yake kwenye fani ya muziki, anasema amewashirikisha wasanii kadhaa wa Nigeria katika nyimbo anazoziandaa.
Tayari moja ya nyimbo hizo mpya inayofahamika kwa jina la ‘Elo’ ipo mtaani akiwa amemshirikisha msanii mkubwa nchini humo, David Adeleke, a.k.a Davido, na imekwishazua gumzo la aina yake, wengi wakishangazwa amewezaje kumpata nyota huyo wa Afrika.
“Kwanza, ninamshukuru Mungu kwa kunifikisha hapa, pia ninapenda kumshukuru sana Davido. Nilimpelekea kazi yangu, akaisikiliza, ikamgusa na akaipenda ndiyo maana akakubali kushiriki na mimi katika wimbo huu.
“Hii inaonyesha uwepo wa Mungu na kwamba wakati ukifika, umefika na itakuwa hivyo,” anasema Dayna.
Anaishukuru menejimenti yake kwa juhudi kubwa wanazofanya kutangaza kazi zake ndani na nje ya Tanzania.
“Ni hawa ndio wamenisaidia sana kwa upande wa kazi zangu, na kwa hakika zinakwenda vizuri. Naweza kusema kila kitu kimekuwa rahisi kwa sababu yao.
“Juhudi na uvumilivu wao umelipa. Huwezi kuwasahau mashabiki katika mafanikio ya msanii. Hawa ni muhumu sana na ninawaomba waendelee kuniunga mkono na kutazama ngoma yangu mpya ya Elo, Dayna Nyange Ft Davido,” anasema.
EP hiyo ya mwanadada wa Kitanzania imekamilika na kutimiza ndoto yake ya muda mrefu ambayo pia ni ndoto ya kila msanii wa muziki duniani.
“Ni furaha kwangu na washirika wangu kwa kukamilisha hii EP inayokwenda kwa jina la ELO. Tumefanikiwa, tena si kufanikiwa tu, ila ni kwa kiwango kikubwa!
“Ukiitazama utakubaliana nami kwamba ni kazi ambayo nimetumia nguvu kubwa, akili nyingi sana. Haikuwa kazi rahisi hata kidogo,” anasema.
Katika EP hiyo Dayna amewashirikisha wasanii kadhaa tofauti na anasema: “Uzinduzi wa EP hii unakaribia sana na utafanyika wakati wowote.”