Na G. Madaraka Nyerere
 
Mwishoni mwa mwezi uliopita nilihudhuria ufunguzi wa jengo jipya la kituo cha Dawati la Jinsia na Watoto kwa Wilaya ya Butiama. Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro.
Wengi walizungumza ingawa ni maneno ya Kamanda Sirro yanayokumbukwa zaidi. Mkoa wa Mara hauna sifa nzuri kwenye suala la mahusiano ya wanaume na wanawake. Wanaume wa Mkoa wa Mara, kwa ujumla wao, wanaonekana kuwa wakatili dhidi ya wanawake.
Imani hiyo haijajitokeza kwa ndoto pekee; ni matokeo ya mlolongo wa matukio mbalimbali ya kikatili dhidi ya wanawake yanayosikika kutoka maeneo kadhaa ya mkoa huo.
Ni tatizo la mfumo dume, ingawa mfumo huu haupo Mkoa wa Mara pekee. Upo duniani kote. Kinachoonekana Mkoa wa Mara ni tofauti tu za viwango vya ukandamizaji unaofanyika ndani ya jamii, hasa dhidi ya wanawake.
Chimbuko lake ni mila na desturi za tamaduni mbalimbali, na hata baadhi ya dini, ambazo zilimpa nafasi mwanaume kushika na kutawala nafasi za uongozi wa kisiasa, kuonekana anastahili kuwa na mamlaka ya kusimamia maadili, na ambaye alipata nafasi kubwa ya kunufaika na jamii yake.
Mwanamke hakuwa na sauti au nafasi ya kufanya uamuzi woyote wa msingi kwa sababu iliaminika kuwa ziko tofauti za kiasili kati ya mwanamke na mwanaume.
Wakati hatuwezi kupinga kuwa ziko tofauti kati ya wanawake na wanaume, tutakuwa wavivu wa kufikiri tukishikilia msimamo kuwa tofauti hizo zikiwekwa kwenye mizani ya ubinadamu, basi mwanaume atakuwa binadamu zaidi kuliko mwanamke. Utu wa mtu haupaswi kutokana na jinsia.
“Haupaswi” ni neno rahisi zaidi kuandika kuliko kulizingatia. Ubaguzi wa aina yoyote, wa rangi au wa kijinsia, ni masuala ambayo hatuzaliwi nayo; ni tabia ambazo tunajifunza kutokana na makuzi yetu.
Njia ya uhakika ya kubadilisha tabia hizi hasi kama ni kuelimisha jamii juu ya athari zake ingawa tunafahamu kuwa si rahisi kubadilisha mila na desturi, hata kama zinaonekana kuwa zinaleta madhara ya wazi kabisa ndani ya jamii.
Kwa muda mrefu nimeamini kuwa jitihada ya kuelimisha jamii zinazokeketa wasichana kwa kusema kuwa ni mila mbaya isingeweza kuzaa mafanikio bila kumuondoa msichana anayekeketwa kutoka jamii aliyokulia.
Na sababu ya kufanya hivi iko bayana: watu wazima ambao ndio ni muhimu kabisa katika kubadilisha desturi, wao hao hao ndio wanaosimamia utekelezaji wa hizo desturi zinazopaswa kuachwa.
Kumuondoa msichana, ambaye akishakeketwa anaozeshwa na aghalabu kwenye umri mdogo kabisa, kunazua tatizo la kumtenganisha binti huyo na familia na jamii yake.
Halitapatikana suluhisho la kuridhisha mpaka uzao wa watoto wanaokimbizwa au kutoroka kutoka kwenye jamii hizi wafikie utu uzima, wazae watoto wao, na kukuza rika ambalo halitaendeleza mila ya ukeketaji.
Wakati tukisubiri hao wasichana wa leo wawe watu wazima na wanaume kubadilisha mitazamo juu ya mahusiano yao na wanawake ndani ya jamii hizi, tunahitaji ulinzi wa wanajamii ambao wanaendelea kuathiriwa na mila na desturi zinazowakandamiza. Na ndiyo mantiki mojawapo ya kufungua madawati ya jinsia na watoto ili kusogeza karibu kinga ya sheria kwa waathirika.
Kwenye uzinduzi wa Butiama, alipopata nafasi ya kuongea na baadhi ya wakazi wa Butiama waliojumuika, IGP Sirro alishauri na kukemea.
Alisema: “Kuendelea kutembea na mapanga na mishale kwa sasa huo ni ushamba.”
Akaendelea:  “Somesheni watoto wa kike, maana kwa sasa ndio wakombozi katika familia zetu.”
Akaongeza: “Kumpiga mwanamke kumepitwa na wakati, yeyote atakayeendelea na tabia hizo mbaya ninakuagiza OCD utumie nguvu za kadiri ili kukomesha hilo.”
Kwa msisitizo akatukumbusha kuwa hata kama mume anamfumania mke, haruhusiwi kumpiga. Anaweza kuongea naye ili wamalizane kwa kumsamehe. Kama hilo litamshinda afuate utaratibu wa kisheria wa kumpa mke wake talaka.
Baadhi ya wanawake waliokuwa pale walipiga vigelegele vya nguvu. Baadhi ya wanaume waliguna, kimya kimya.

Mwisho