Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam
(DAWASA) DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amesema kuwa uwezo wa uzalishaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam umeongezeka kutoka lita 520,000,000 kwa siku hadi lita 534,600,000 kwa siku, sawa na ongezeko la lita 14,600,000 kwa siku. Hayo yameelezwa leo, Machi 11, 2025, Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Mhandisi Bwire ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 11, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.

Amefafanua kuwa uwezo wa kuhifadhi maji umeongezeka kutoka lita 153,649,000 hadi lita 198,965,000, sawa na ongezeko la lita 45,316,000. Alisema mafanikio haya ni matokeo ya juhudi kubwa za Serikali na Mamlaka katika kuboresha huduma za maji kwa wananchi.

“Tofauti na zamani, kwa sasa tuna mafanikio makubwa. Mtandao wa usafirishaji na usambazaji wa maji umeongezeka kutoka kilomita 4,690.7 hadi kilomita 7,206, sawa na ongezeko la kilomita 2,513.4. Mtandao wa majitaka umeongezeka kutoka kilomita 450 hadi kilomita 519.4, sawa na ongezeko la kilomita 69.4,” amesema Mhandisi Bwire.

Amesema kutokana na juhudi za Serikali, idadi ya maunganisho ya wateja wa majisafi imeongezeka kutoka 343,019 hadi 455,720, sawa na ongezeko la wateja 112,701, na kuongeza kuwa upatikanaji wa huduma ya majisafi umeongezeka kutoka wastani wa asilimia 89.

Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji yenye uhakika, Mhandisi Bwire alieleza kuwa DAWASA imeanza utekelezaji wa mradi wa bwawa la Kidunda lenye mkataba wenye thamani ya Shilingi bilioni 335.9. Hadi sasa, Shilingi bilioni 85.4 zimetolewa na mradi umefikia asilimia 28 ya utekelezaji.

Aidha, Mhandisi Bwire alitaja mafanikio mengine kuwa ni kutolewa kwa kibali cha kuanza maandalizi ya mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji, utakaohakikisha upatikanaji wa maji kwa mahitaji ya jiji hadi mwaka 2050. Hivi sasa, kazi ya kuandaa michoro ya mwisho ya mradi huo inaendelea.