Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) imesema inaendelea na mchakato wa manunuzi ya pampu zitakazosaidia kuongeza ufanisi katika mtambo wa uzalishaji maji Ruvu Juu ambao husambaza maji katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la Mbezi katika Wilaya ya Ubungo.

Hayo yamesemwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire alipokutana na wananchi na wakazi wa mtaa wa Mshikamano, Kata ya Mbezi, Wilaya ya Ubungo kujadiliana juu ya mipango ya uboreshaji wa huduma ya maji katika eneo hilo na maeneo jirani.

“Tunatambua eneo la Mshikamano ni moja ya maeneo yenye changamoto ya upatikanaji maji ambayo DAWASA tunalazimika kuyapatia maji kwa awamu. Kama DAWASA tunaahidi kufikisha maji kwa Wananchi kwa siku tulizokubaliana ili kupunguza changamoto za kihuduma ,” amesema Mhandisi Bwire.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mshikamano, Henry Madenge ametoa rai kwa DAWASA kuweka utaratibu nzuri wa upatikanaji wa huduma na kuusimamia ili wananchi wapate huduma.

“Tunashukuru DAWASA kwa kuitikia wito wa kukutana na kutusikiliza na Wananchi hawa na kutupa majibu ya hoja zetu za maji, tunategemea maji yatatufikia mapema ili wananchi tuepukane na shida ya maji katika mtaa wetu,” amesema.

DAWASA inaendelea na juhudi za kuhakikisha inaboresha huduma ya maji katika eneo lake la kihuduma.