DAWASA imejizatiti katika kuhakikisha inawapatia maji salama wakazi wote wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na wale wa maeneo ya Mkoa wa Pwani.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Cyprian Luhemeja, amekagua miradi ya maji inayoendelea kukamilishwa.
Akizungumza na Gazeti la JAMHURI kabla ya kuanza ziara hiyo, Mhandisi Luhemeja anasema ziara hiyo ni kufanya tathmini ya miezi sita ya utendaji kazi tangu kuanza kwa Dawasa mpya, ambapo kwa sasa Dar es Salaam asilimia 85 wanapata huduma ya maji safi na salama.
Anasema Dawasa imetenga asilimia 35 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji.
“Mpaka sasa Dawasa imekwishatumia Sh bilioni 12 katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ambapo jumla yake ni miradi 41 ikiwa kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji wake,” anasema Luhemeja.
Katika bajeti ya mwaka 2019/2020 wametenga Sh bilioni 64 kwa ajili ya kukamilisha miradi yote ili kufikia lengo la serikali la asilimia 95 ya wananchi kupata maji safi na salama.
Mhandisi Luhemeja anasema lengo la Dawasa ni kuifungua Dar es Salaam na Pwani kuhakikisha maji yanapatikana baada ya kukosekana kwa muda mrefu katika maeneo yaliyokuwa hayana mtandao wa maji.
Wakati mabadiliko makubwa yakiendelea ndani ya Dawasa, taasisi hiyo imetenga kiasi cha asilimia 35 ya mapato yake ya ndani kwa kila mwezi kuhakikisha wanaanzisha miradi ya maji jijini Dar es Salaam.
Hayo yamethibitishwa na Mhandisi Cyprian Luhemeja, wakati wa ziara ya kukagua miradi 42 ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na Bagomoyo na Pwani hivi karibuni.
“Kuna miradi 42 inayotekelezwa kwa fedha za ndani ambapo tumetenga asilimia 35 ya mapato yao ya kila mwezi kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali hasa pembezoni mwa mji ambapo mtandao haujafika,” anasema Luhemeja.
Anasema lengo kubwa la DAWASA ni kuwekeza kwenye mtandao wa maji kwa kutumia fedha za ndani na kila mwezi wamekuwa wanatumia Sh bilioni 3 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Gezaulole, Chalinze Mboga, Kisarawe, Kibamba, Kiwalani Phase 3 na miradi mingine.
Luhemeja anasema kuwa hatua za upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam umefikia asilimia 85 ambapo kwa siku yanazalishwa maji lita za ujazo milioni 502 kutoka kwenye mtambo wa Ruvu Juu, Ruvu Chini, Mto Kizinga na visima vilivyojengwa na jamii au watu binafsi.
Ziara ya Afisa Mtendaji Mkuu ililenga kukutana na wananchi na kuwaeleza nini Dawasa inafanya katika kuwahakikishia upatikanaji wa maji katika maeneo ya Mabwepande, Bunju na Kitunda ambapo mradi wao unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Katika hatua nyingine, Dawasa imewataka wamiliki na wasambazaji wa maji ya kisima kujitokeza ili wapewe leseni na cheti cha kusambaza baada ya kupimwa ubora wake.
Luhemeja anasema kwa mujibu wa sheria hairuhusiwi kusambaza maji katika eneo la huduma la mamlaka hiyo bila kuwa na leseni.
“Tumeanza kuvitambua visima vyote vinavyotoa huduma ya maji na kupima maji yake bure ili wakazi wapate maji safi na salama,” anasema Luhemeja.
Anasema kwa sasa watu 10,700 wanatumia maji ya visima na kwa kupima maji yake itasaidia kuondoa kabisa changamoto ya magonjwa ya mlipuko.
Mhandisi Luhemeja anasema ziara hiyo ni ya kufanya tathmini ya miezi sita ya utendaji kazi tangu kuanza kwa Dawasa mpya, ambapo kwa sasa Dar es Salaam asilimia 85 wanapata huduma ya maji safi na salama.
“Sehemu kubwa ya jiji inapata maji, maeneo ambayo hayakuwa na huduma sasa yamefikiwa, kwa mfano maeneo ya Segerea, Kinyerezi, Kipawa, Ukonga, Changanyikeni, Goba, Mivumoni, Salasala, Madale kwa Msuguri, kwa Mbonde, Misugusugu, Kiwalani, Miti Mirefu na baadhi ya maeneo ya Kigamboni,” anasema Mhandisi Luhemeja.
Mhandisi Luhemeja anasema kuwa, mafanikio hayo yanakuja baada ya ufanisi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyopelekea kuongezeka kwa maji yanayozalishwa pamoja na kuimarika kwa utendaji kazi kunakozingatia usimamizi mahiri wa utoaji huduma bora.
“Katika kuhakikisha kuwa maji yaliyoongezeka yanawafikia wananchi wengi zaidi hasa katika maeneo ambayo zamani hayakuwa na mtandao wa mabomba, miradi mbalimbali mikubwa na midogo imetekelezwa, miradi hiyo inahusisha ujenzi wa matenki ya maji matano yenye ujazo wa kati ya lita milioni 5.0 na 6.0 pamoja na ulazaji wa mtandao wa mabomba,” anasema.
Matenki hayo yamejengwa katika maeneo ya Changanyikeni, Salasala, Wazo, Mabwepande na Bagamoyo na katika maeneo yote ya miinuko ili kuwezesha maji kufika katika maeneo mengi zaidi kwa msukumo mzuri na mradi huo umetekelezwa na serikali kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya India na upo katika hatua za ukamilishwaji.
Mhandisi Luhemeja amesema kilometa 176 za mtandao chakavu wa maji zimebadilishwa, hivyo kuchangia kupunguza kiwango cha maji yanayopotea, kwa ujumla kiasi cha kilomita 500 za mabomba mapya zimelazwa mitaani ili kuweza kugawa maji kwa uwiano mzuri zaidi na kufanya mamlaka kuwa na mtandao wa kilomita 3,000 kutoka 2,500 zilizokuwepo mwaka 2015.
Ili kuboresha huduma na kufikia lengo la kufikishia asilimia 95 ya wananchi ndani ya eneo la huduma ya Dawasa maji safi, bora na ya gharama nafuu kuna miradi imendelea kutekelezwa ambapo kuna mradi wa Chalinze III, Kibamba-Kisarawe, Chalinze Mboga, Mlandizi – Manelomango, Kilindoni – Mafia, Mkuranga na miradi mipya inayolenga kufikia watu wenye kipato waishio katika maeneo yasiyo na huduma ya maji.
Miradi mitatu mikubwa ya kisasa ya uchakataji majitaka inatarajiwa kujengwa hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya kufikishwa asilimia 30 ya huduma ya majitaka. Pia miradi midogo ya uchakataji majitaka ipatayo 50 itajengwa kuhakikisha kuwa wananchi wa ngazi zote wanafikiwa na huduma bora ya majitaka.