Wakati wizara na taasisi za serikali zikiendelea kupambana kukamilisha matarajio ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 – 2020, katika kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa, Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) inatekeleza miradi mitano mikubwa ambayo imelenga kuwaondolea kero ya maji wakazi wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na Mkoa wa Pwani.
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, anasema pamoja na miradi ya Dawasa, serikali imeandaa mradi mkubwa wa kupeleka maji katika miji 28 nchini utakaogharimu zaidi ya Sh trilioni 1.2.
Akizungumzia miradi sita iliyotiwa saini chini ya Dawasa, Profesa Mbarawa anasema lazima ianze kutekelezwa bila kuchelewa na wananchi waendelee kupatiwa maji kila eneo bila kusubiri kuzinduliwa kwa mradi.
Anasema katika miradi hiyo sita inayogharimu Sh bilioni 114.5, mmoja unatekelezwa kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia (WB) na mingine mitano inatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.
Prof. Mbarawa anasema awamu ya pili ya mradi wa usambazaji maji kuanzia matenki ya maji Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi Bagamoyo uliolenga kuhudumia wateja 750,000 utaunganisha wateja wapya 64,000 na utagharamiwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya Sh bilioni 77.2, ukitarajiwa kukamilika miezi 18 kuanzia sasa.
Miradi mingine inayogharamiwa kwa fedha za ndani itagharimu Sh bilioni 40 zinazotokana na vyanzo vya ndani ya Dawasa na uwezeshaji wa serikali.
Miradi mingine ni bomba la kusafirisha maji kutoka Jet hadi Buza, visima 20 Kimbiji na Mpera wilayani Kigamboni, usambazaji wa maji Kisarawe – Pugu, mradi wa maji katika mji wa Mkuranga na bomba la kusafirisha maji kutoka Mlandizi hadi Kijiji cha Mboga (Chalinze).
Prof. Mbarawa anaeleza kukerwa kwake na kuanza kwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka Chuo Kikuu hadi Bagamoyo, ambao usanifu wake ulikamilika mwaka 2014 na makubaliano ya kifedha yalifikiwa wakati wa utiaji saini wa mradi wa daraja la Ubungo ambao kwa sasa uko karibu asilimia 40 ya utekelezaji.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja, anasema utiaji saini huo wa mikataba sita yenye thamani ya Sh bilioni 114 ni sehemu ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 Dar es Salaam inakuwa na uhakika wa maji kwa asilimia 95 ya wakazi wake, kutoka asilimia 85 iliyopo sasa.
Mhandisi Luhemeja anasema Dawasa imeimarisha utendaji na upatikanaji wa huduma za maji kutoka asilimia 68 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 85 mwaka huu, na kutoka makusanyo ya Sh bilioni 3.2 hadi Sh bilioni 11.2 kwa mwezi mwaka huu.
“Mwaka 2015 maunganisho ya maji yalikuwa kwa wateja 123,000 lakini kutokana na juhudi zinazoendelea tumeweza kuunganisha wateja 326,000, lakini pia kiwango cha upotevu wa maji kimepungua kutoka asilimia 53 mwaka 2015 hadi asilimia 41 mwaka huu.
“Kiwango hicho cha upotevu wa maji bado ni kikubwa, kwa hiyo tunaendelea na juhudi za kukipunguza zaidi ili maji yanayozalishwa yaweze kusaidia watu wengi zaidi,” anasema Mhandisi Luhemeja.
Miaka minne iliyopita Dawasa imeboresha ulipaji wa ankara kwa kuhakikisha hawapandishi malipo ya ankara hizo za maji na kwa sasa bado haina mpango wa kupandisha malipo hayo, kwa kuwa nia ni kutoa huduma za maji kwa wananchi wengi zaidi.
Mhandisi Luhemeja anasema Dawasa inaendelea kuunganisha wateja kwa mkopo kwa wale wanaounganishiwa maji kwa maunganisho ya awali, hivyo hakuna mteja mpya atakayelipishwa gharama za kuunganishiwa maji.
Luhemeja anasema kutokana na wingi wa visima binafsi katika maeneo yanayohudumiwa na Dawasa, wameunda kamati maalumu kwa ajili ya kufuatilia na kuhakikisha visima hivyo ambavyo kwa sasa vipo zaidi ya 6,000, vinapatiwa huduma za kitaalamu, ikiwamo kuwekwa dawa.
“Tumechukua uamuzi huu kwa kuwa kuna changamoto nyingi za kitaalamu, hasa yanapotokea magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, ambayo yanaenea kwa kasi kutokana na maji ya visima vingi kutokuwa na dawa, kwa hiyo hii itasaidia kupunguza madhara,” anasema Mhandisi Luhemeja.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa anasema ndani ya muda wa miezi 12 kamati hiyo itahakikisha inakuja na tathmini halisi ya nini kifanyike kwa ajili ya kumaliza matatizo yote yaliyoainishwa katika utumiaji wa visima binafsi, ambapo tayari hatua zimeshaanza kuchukuliwa kufukia visima vifupi na vingine vilivyokuwa wazi kufunikwa.
Anasema pamoja na miradi sita mikubwa iliyotiwa saini, ipo miradi maalumu mitatu inayohusika na maji taka ambayo iko kwenye eneo la Jangwani, ambapo tayari mkandarasi yuko eneo la mradi. Mingine ni ya Mbezi Beach na Mtoni Mtongani kwa ajili ya kusaidia wakazi wa maeneo hayo wasiokuwa na mfumo unaofaa wa majitaka, utakaokamilika ndani ya miezi 12 ijayo.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Asumpta Mshama, anasema mkoa wake bado unahitaji zaidi huduma za Dawasa kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa wakazi na ujenzi wa viwanda.
Anasema pamoja na ujenzi wa machinjio yenye uwezo wa kuchinja ngombe 1,000 na mbuzi 3,000 kwa siku na ujenzi wa viwanda zaidi ya 50 katika eneo la Zegereni, maeneo hayo bado hayana uhakika wa maji safi na salama, hivyo ni vema kuangaliwa upya namna ya kuyafikia kwa haraka.
“Mkoa wa Pwani kwa sasa ni wa viwanda, ambapo vinaongezeka kwa kasi lakini kuna uhaba mkubwa wa maji, kwa hiyo ni vema Dawasa iweke mkakati maalumu wa kuyafikia maeneo haya na kusambaza huduma zake,” anasema Asumpta.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, anasema miradi hii mikubwa ya maji ikikamilika kwa wakati itasaidia usafi kwa wananchi na kupunguza kasi ya magonjwa ya tumbo na ya milipuko, ukiwamo kipindupindu.
“Tumebaini kuwa kutokuwapo kwa uhakika wa maji kunawasukuma watu kuchimba visima vifupi ambavyo ni kichocheo cha magonjwa ya mlipuko. Tumeagiza wataalamu wa afya vifukiwe, lakini miradi hii ya Dawasa ikikamilika itasaidia kupunguza matatizo kama haya,” anasema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Dawasa, Jenerali mstaafu Davis Mwamunyange, anasema miradi hii ni hatua nzuri ya utekelezaji kwa vitendo kaulimbiu ya kumtua mama ndoo kichwani, akitoa shukrani kwa Benki ya Dunia na Wizara ya Maji kwa juhudi zinazoendelea.
Jenerali Mwamunyange anasema Dawasa bado ina safari ndefu kwa kuwa mahitaji ya maji bado ni makubwa katika maeneo ya pembezoni ikiwamo Kibaha, ambako mji unakua kwa kasi, hivyo ni wakati mwafaka sasa kuangalia namna ya kutatua changamoto za wakazi wa maeneo hayo.
“Lakini tukubaliane, bado kuna malalamiko ya wananchi kuhusu kupelekewa ankara zisizokuwa sahihi bado ni makubwa. Hapa bado kuna tatizo, hivyo ni vema mchukue hatua za haraka kuhakikisha malalamiko haya yanakoma, ni lazima tupate suluhisho endelevu,” anasema.