“Samahani daktari, asubuhi ya siku tatu zilizopita kaka yangu alikutwa amekufa chumbani
kwenye nyumba ya wageni alipokwenda kupumzika na mpenzi wake…”
“Lakini baada ya kumhoji huyo mpenzi wake, alisema wakati wameingia chumbani alikunywa
vidonge kadhaa ambavyo baadaye, wataalamu waligundua vilikuwa vya kuongeza nguvu za
kiume. Je, ni kweli dawa za kuongeza nguvu za kiume zinaweza kusababisha kifo?”
Hilo ni swali nililoulizwa wiki iliyopita na mmoja wa wasomaji wa safu hii. Nami ninachukua fursa
hii kulitolea ufafanuzi.
Kwanza kabisa naomba ieleweke kuwa dawa yoyote ile ikitumika kinyume au pasipo kufuata
ushauri wa mtaalamu wa afya, inaweza kuwa hatari kwa afya na hata kusababisha kifo.
Na tunapokuja kwenye suala la dawa za kuongeza nguvu za kiume, dhana hii huthibitika zaidi.
Tatizo la kukosa nguvu za kiume kwa ujumla wake linakuja na sura tofauti, lakini sura
iliyozoeleka ya tatizo hili ni pale mwanaume anaposhindwa kushiriki tendo la ndoa kikamilifu.
Anashindwa kudumu kwa muda mrefu na hatimaye kusinyaa kabla ya kumaliza tendo la ndoa.
Jambo hili husababishwa na vihatarishi na matatizo mbalimbali ya kiafya kwa ujumla wake,
lakini kusinyaa au kutosimama kikamilifu wakati wa kushiriki tendo la ndoa kunatokana hasa na
msukumo hafifu wa damu kwenye via vya uzazi.
Hivyo, naomba ieleweke kuwa dawa hizi hazileti tiba ya kudumu wanavyodhani, bali zinafanya
kazi ya kuongeza kasi ya msukumo wa damu kwenye mishipa ya damu iliyopo kwenye sehemu
za siri za mwanaume.
Hiyo inatokea ili mwanaume aweze kushiriki tendo la ndoa kwa wakati ule na utendaji kazi wa
dawa hii huwa ni wa muda mfupi tu. Hivyo, mtumiaji atalazimika kutumia dawa kila anapohitaji
kushiriki tendo la ndoa.
Dawa hizo zimewekewa kiambata chenye kemikali inayoitwa sildenafil na hiki kina kiwango
maalumu kinachotakiwa kuingia mwilini kutokana na hali ya kiafya ya mtumiaji husika, na
madhara ya kiafya ya dawa hii ndipo yanapoanza.
Kama nilivyoeleza awali, dawa hii inafanya kazi kwa kuongeza kasi ya msukumo wa damu
mwilini ili kulazimisha damu ifike kwenye sehemu za siri za mwanaume, hatimaye aweze
kusimama.
Na kama tunavyofahamu, kazi ya kusukuma damu mwilini inafanywa na moyo, hivyo dawa hii
huulazimisha moyo kufanya kazi ya ziada na hivyo kuupa (moyo) hatari ya kupata matatizo
kama vile kwenda kasi na hata kusababisha moyo kusimama.
Na kwa mtu mwenye matatizo mengine ya kiafya kama vile shinikizo la damu, mtumiaji
anakuwa hatarini zaidi ya dawa hizi kumsababishia kifo.
Watu wengi wamekuwa wakitumia dawa hizo holela bila kupata ushauri wa wataalamu wa afya,
na hii ni hatari sana kwa sababu wengi wamekuwa wakizitumia kiasi kikubwa kuliko afya zao
zinavyoweza kuhimili.
Ni vyema kwanza kupatiwa vipimo vya afya kama vile kupima kazi ya mapigo ya moyo na
shinikizo la damu, ili kushauriwa kiwango stahiki cha dawa hii kulingana na hali ya kiafya.
Ninashauri pia kama una tatizo la kukosa nguvu za kushiriki tendo la ndoa, ni vyema kuwaona
kwanza wahudumu wa afya na kupata msaada wa utatuzi wa tatizo kuliko kuvamia dawa hizi
bila ushauri wa daktari. Ni hatari.