Matumizi ya dawa za kulevya nchini yameongezeka katika kipindi cha miaka miwili kwa asilimia 75 katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Zaidi ya wahanga 3,000 wa dawa za kulevya wanaendelea kupatiwa dawa (Methadone) katika vituo vya afya vitatu hapa nchini yenye lengo la kuwasaidia ili washiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.

Katika mahojiano maalumu na JAMHURI, daktari bingwa wa magonjwa ya akili na dawa za kulevya kutoka Hospital ya Taifa ya Muhimbili, Dk Cassian Nyandindi, anasema tatizo la matumizi ya dawa za kulevya nchini ni kubwa tofauti na watu wanavyofikiri.

Anasema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai tu vituo vinavyotoa tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya nchini vinahudumia wahanga zaidi ya 3,151 wanaoendelea kupatiwa matibabu hapa nchini, jambo ambalo ni hatari kutokana na idadi hiyo kuongezeka kila mara.

Dk. Nyandindi anasema kuwa takwimu za mwaka  2014, zimebainisha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na watumiaji 25,000 wa madawa ya kulevya, idadi iliyoongezeka na kufikia 50,000 kwa mwaka huo huo, jambo ambalo si jema kwa Taifa.

“Kundi kubwa watumiaji wa dawa za kulevya ni vijana ambao ni nguvu kazi kwa Taifa katika kuhakikisha wanafanya kazi na kuleta maendeleo,’’ anasema Dk Nyandindi.

Vituo hivyo vya tiba kwa wahanga  wanaopata dawa Methadone vinapatika katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo kuna wahanga 1,001, Temeke 820, Mwananyamala 1,200 huku Zanzibar kukiwa wahanga 200 wanaopata matibabu hayo.

Dk Nyandindi anasema lengo la kuanzisha vituo hivyo ni kuhakikisha watumiaji wa dawa za kulevya wanaacha kabisa na pale inaposhindikana hushauriwa kuzitumia kwa njia salama na si kujidunga sindano.

Anasema kuwa 75 ya waathirika wa dawa za kulevya waliokuwa wameathirika mfumo wa ufahamu pamoja na ugonjwa wa akili, wamepatiwa matibabu na kuacha kabisa matumizi ya dawa hizo huku asilimia 25 wakishindwa kuacha na kuendelea na matumizi ya dawa hizo.

“Jambo la kusikitisha ni kwamba, watumiaji wa dawa za kulevya asilimia kubwa wanatoka katika familia masikini licha ya kuwapo idadi ndogo ya wahanga hao wanaotoka katika familia zenye kipato cha kati na juu, hali inayozidi kuziongezea umasikini familia hizo duni,’’ anasema Dk Nyandindi.

Pia anabainisha kuwa kutokana na ongezeko la matumizi makubwa ya dawa za kulevya nchini, vituo vya tiba havitoshelezi huku tiba hiyo ikitolewa zaidi jijini Dar es Salaam na Pwani tu.

Anasema hali inayofanya huduma ya tiba hiyo kuhitajika pia katika mikoa mingine nchini ili kuweza kuwasaidia kuondokana na matumizi ya dawa hizo.

“Mkoa wa Arusha kwa sasa ndiyo unaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wahanga wanaokuja kutibiwa. Mikoa ya Pwani, Morogoro, Mwanza, Mbeya pamoja nao ni muhimu kuwa na vituo hivi kutokana na hali ilivyo kuliko wote kutegemea kuja kutibiwa jijini Dar es Salaam.”

Anaendelea kwa kusema, “Vituo ni vichache, watoa huduma ni wachache pia, hivyo tunaiomba Serikali iweze kujenga vituo kama hivi katika mikoa yote ili kupunguza gharama na msongamano usio wa lazima,’’ anasema Dk Nyandindi.

Hata hivyo, anasema kuwa watumiaji wa dawa za kulevya wanapendelea kutumia aina mbalimbali za dawa bila kuangalia athari zake ikiwamo bangi pamoja na heroin, jambo ni hatari kwa maisha yao.

Akizungumzia kuhusu matumizi ya dawa za usingizi za piriton (valium) kwa watumiaji wa dawa za kulevya, Dk Nyandindi anasema idadi kubwa ya wahanga hao hupendelea kutumia dawa za usingizi baada ya kukosa fedha.

Anasema piriton ni aina ya dawa za kulevya ambapo asilimia kubwa  ya watumiaji hupendelea kuitumia ili kujiridhisha kwa kuongeza hamasha katika matumizi ya dawa.

Madhara yake

Dk Nyandindi anasema ugonjwa unaotokana na matumizi ya dawa za kulevya ni miongoni mwa magonjwa sugu kama yalivyo magonjwa mengine ikiwamo ukosefu wa kinga mwilini (UKIMWI), kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa muhusika, familia na Taifa kwa ujumla.

Kuna uwezekano mkubwa wahanga wa dawa za kulevya kupata ugonjwa wa kifafa, kuathirika kwa mfumo wa fahamu pamoja na kupata ugonjwa wa akili. Pia upo uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu.

Watumiaji wa dawa za kulevya

Baadhi ya watumiaji wa dawa za kulevya wanasema kuwa wakati wanatumia dawa walikuwa wakiishi katika mazingira magumu hasa pale wanapokosa fedha za kununua dawa.

Neema Mageta (35), mkazi wa Gongo la Mboto, Dar es Salaam, anasema baaada ya kupata vishawishi kutoka kwa marafiki wanaotumia dawa alijikuta anaingia katika majaribu na kuanza kutumia bila kujua ni hatari kwa afya yake.

Anasema mwaka 2012 alianza kutumia dawa kwa kuvuta bangi, kadri muda ulivyokuwa unazidi kwenda akaanza kutumia uga kwa kujiduga sindano, na kujikuta anafanya vitendo vya uhalifu.

Mgeta, ambaye ni mama wa mtoto mmoja, anasema mwaka jana alianza kutumia tiba na sasa hali yake imeimarika.

Amewataka Watanzania wanaotumia dawa za kulevya waende kuanza tiba ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.

Akizungumza na JAMHURI, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Augustino Lyatonga Mrema, anasema asilimia kubwa ya wahanga wa dawa ya kulevya ni vijana, na ndiyo nguvu kazi ya Taifa katika kuhakikisha wanaleta mabadiliko chanya na kupiga hatua katika masuala ya maendeleo.

Anasema utegemezi wa dawa za kulevya ‘drug addiction’ ni moja ya magonjwa sugu ambayo yanaisumbua jamii ya dunia ya sasa kwa afya na njanya zote.

Anasema vijana wengi wamekamatwa na kete moja au mbili na Jeshi la Polisi na kufunguliwa mashtaka mahakamani bila kujali kufanya hivyo sio jambo jema katika kuhakikisha tunadhibiti matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini.

Hata hivyo, anasema kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2015, kipengele cha 31 kinabainisha kuwa kuhusu adhabu, ambapo wahanga hao wanapelekwa gerezani, badala ya kupewa tiba.

Anasema kufanya hivyo kunaweza kupunguza gharama kwa Serikali kwani waathirika wa dawa wanapokuwa jela huwa wanatumia gharama za Serikali kwa kila kitu.

Mrema anasema kutokana ukubwa wa tatizo hilo, madaktari wamekuwa wakiwapatia matibabu ya aina tatu wahanga ikiwamo semina za kubadilisha fikra ‘Mind set’, dawa (methadone) pamoja na matibabu kwa njia ya kazi (Occupational Therapy).

Msimamizi wa Kituo cha Methadone, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Daktari Bingwa Idara ya Afya, Magonjwa ya akili, Dk Omary Ubuguyu, anasema kitaifa hakuna takwimu sahihi zinazoonesha idadi ya matumizi ya dawa ya kulevya ila taarifa ya makadirio inabainisha kuwapo na zaidi ya watumiaji 300,000 wa kulevya.

Anasema idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya inakadiriwa kuwapo Mkoa wa Dar es Salaam na waathirika wake hutumia dawa aina ya heroin ambayo ni hatari zaidi kwa afya zao.

Dk Ubuguyu anasema katika kituo cha Methadone cha Temeke kinahudumia wahanga 820 wa dawa ya kulevya ambao wanaendelea kupata tiba ya methadone kila siku. Wanawake wakiwa ni 56 na wanaume wakiwa ni 764.

“Baadhi ya wahanga wa dawa za kulevya wanaopata tiba ya Methadone katika kituo hiki, baada ya kuchukua vipimo vyao vya afya wamegundulika wana maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwamo ugonjwa wa Ukimwi, Homa ya Ini pamoja na ugonjwa wa kifua kikuu,’’ anasema Dk Ubuguyu.

Dk Ubuguyu anaeleza kuwapo na ongezeko kubwa la matumizi ya dawa za kulevya nchini tofauti na miaka mitatu iliyopita, huku wahanga wakubwa wakiwa ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 12-30 ambao ni nguvu kazi ya Taifa.

“Zaidi ya asilimia 90 wahanga wa dawa za kulevya ni vijana wenye kipato cha chini kwani wanafanya kazi ya kubeba mizigo, kupiga debe, na wengine hawana kazi zaidi ya kuwa ombaomba,’’ anasema Dk Ubuguyu.

Anasema katika vipimo wanavyofanyiwa kabla ya kuanza tiba wamegundua kuwapo matumizi ya dawa za kulevya za aina mbalimbali ikiwamo piriton ambazo wanashindwa kujua kwa nini wanatumia dawa hizo.

“Ukiona wanakuja kupata tiba ya methadone ujue tatizo limeshakuwa kubwa kutokana madhara yanayojitokeza ya kiafya ikiwamo kupata ugonjwa wa akili,’’ anasema Dk Ubuguyu.

Dk Ubuguyu anabainisha kuwa tiba yake huchukua muda wa miaka miwili kupona kabisa, jambo ambalo ni changamoto kwa watoa huduma kutokana na uchache wao kiasi cha kukosa muda wa kupumzika.

Kwa mujibu wa repoti ya Matumizi ya dawa ya kulevya iliyotolewa  na Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 2015, mwaka 2013 watu milioni 246 walikuwa wanatumia dawa za kulevya.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa idadi hiyo ni ongezeko la watu milioni tatu zaidi ya mwaka 2012 katika matumizi ya dawa za kulevya kwa wakazi wote duniani.

Taarifa hiyo inabainisha kuwa zaidi ya watu milioni 27 wanaotumia dawa za kulevya ni wakazi wa mataifa makubwa duniani, Malaysia pamoja na wafanyabiashara.

Hata hivyo, imeeleza kuwa wastani wa watu milioni 1.65 wanaotumia dawa za kulevya wanaishi na virusi vya UKIMWI kwa mwaka 2013.

Pamoja na kupatiwa matibabu, idadi ya vifo vilivyotokana na dawa za kulevya kwa mwaka 2013 inakadiriwa kuwa ni 187,100.

Dawa aina ya heroin imeonekana kuwa ndiyo imekuwa ikitumiwa kwa wingi barani Ulaya na Amerika. Huku ripoti hiyo ikibainisha ongezeko kubwa la matumizi ya dawa za kulevya mwaka hadi mwaka.

Mwaka 2006 watumiaji wa dawa za kulevya walikuwa milioni 208 huku wahanga wakiwa milioni 26, mwaka 2007 watumiaji milioni 211, wahanga milioni 28.