Kampuni ya Novo Nordisk imezindua dawa yake ya kupunguza uzito ya Wegovy nchini China baada ya kuidhinishwa na mamlaka ya afya mwezi Juni.

Zaidi ya watu milioni 180 wanaishi na uzito wa kupindukia nchini China, ambayo ina idadi ya watu bilioni 1.4.

Kulingana na tovuti ya habari ya biashara ya China, Yicai, dozi ya sindano nne za Wegovy itagharimu yuan 1,400 sawa na dola za Kimarekani 153 ($194).

Ripoti ya Yicai inasema watu wanene nchini China watalazimika kulipia bei kamili ya dawa hiyo, kwani haijajumuishwa katika bima ya kitaifa ya afya.

Utafiti unaonyesha kuwa watu wanene wanaotumia Wegovy wanaweza kupoteza zaidi ya 10% ya uzito wa mwili wao.

Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa China wa WeChat, Novo Nordisk inasema “dawa yake itatoa matibabu salama na bora ya kupunguza uzito kwa walio na uzito kupita kiasi na watu wanene nchini China.”

Wegovy ni dawa ambayo husaidia kudhibiti sukari, kupunguza hamu ya kula, na kuwafanya watu kujisikia kushiba.

Hata hivyo, inaweza kuleta kichefuchefu na kutapika kwa baadhi ya watumiaji, na utafiti unaonyesha kwamba watumiaji wanaweza kurudi katika uzito wao baada ya kuacha matibabu na kuendelea na ulaji.

Wegovy ilianza kuuzwa nchini Marekani mwaka 2021. Ilizua gumzo mtandaoni na tangu wakati huo dawa hiyo imekuwa kwenye rafu za maduka ya dawa kote ulimwenguni.