Na Cresensia Kapinga, Jamhuri, Songea
Katibu Tawala Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Mtela Mwampamba, ameitaka jamii kujitokeza kwa wingi katika zoezi la unyweshaji wa kinga tiba ya Usubi, magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele na yamekuwa yakiwaathiri sana jamii maskini.
Hayo ameyasema jana wakati akizindua shughuli za magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele na unyweshaji wa kinga tiba ya ugonjwa wa Usubi kwa wakazi wa Manispaa ya Songea kwa Agost 2023 iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo.
Amesema kuwa zoezi hilo la Kitaifa ambalo linafanyika kila mwaka chini ya Wizara ya Afya na Tamisemi kwa kushirikiana na Shirika la R.T.I (Research tringle Institute) chini ya ufadhili wa marekani bado kumekuwepo na mwamko mdogo kwa jamii kutokana na kipindi cha zamani wananchi walikuwa wanaamini kuwa magonjwa hayo ni laana ni magonjwa ya kurogwa jambo ambalo sio kweli.
Amesema kuwa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ni magonjwa ambayo yamo ndani ya jamii zetu na hasa jamii maskini na hata wataalam husika ama viongozi hawayapi umuhimu kulingana na madhara yake katika jamii na ndio maana serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele katika magonjwa hayo ili kuhakikisha kwanza wananchi wanapewa Elimu kuhusiana na magonjwa hayo kuwa hayahusiani na Imani potofu ni magonjwa kama magonjwa mengine ambayo yanaweza kupatiwa tiba na pia kupatiwa kinga.
Kwa upande wake Mratibu wa magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele Manispaa ya Songea Dkt. Bload Komba ameyataja magonjwa hayo kuwa ni matende,mabusha,Trakona (vikope) ,kichocho, minyoo ya tumbo na Usubi.
Amesema kuwa zoezi la unyweshaji wa kingatiba ya Usubi kwa jamii ndani ya Manispaa hiyo ni kufikisha zaidi ya asilimia 80 na wanategemea kuwafikia watu zaidi ya laki 2.2 lakini kunamakundi ya watu wasiostahili kunywa dawa hizo kama watoto chini ya miaka 5, wanawake wajawazito na wagonjwa mahututi.
Aidha amewatoa hofu wananchi juu ya dawa hizo kuwa ni salama na zinamanufaa mengi zikitumiwa kwa usahihi kama vile kupunguza maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine,kuwa vimelea vya magonjwa hayo,kuepusha upungufu wa dawa mwilini,kufanya watoto wakuwe vizuri na kuboresha nguvu kazi katika jamii.