DAR ES SALAAM
NA CATHERINE LUCAS
Ofisa Mipango Msaidizi, Masoko na Haki za Binadamu wa Kituo cha Haki za Binadamu na Msaada wa Kisheria (LHRC), Tito Magoti, amesema Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa matukio ya ajali za barabarani.
Akizungumza na JAMHURI, Magoti amesema licha ya takwimu kuonyesha jiji hilo linaongoza kwa ajali na wingi wa askari wa usalama barabarani, bado tatizo la ajali halijapatiwa ufumbuzi. Amesema ukaguzi wa magari unaofanyika mara kwa mara si mwarobaini wa tatizo la ajali za barabarani.
Kwa upande mwingine ameutaja Mkoa wa Tabora kuwa ni kinara wa matukio ya mauaji yanayoambatana na imani za kishirikina na watu kujichukulia sheria mikononi.
Amesema kuwa wanatumia njia za kishirikina kuwatishia watu kuwa watawaua, hivyo watu wanakosa uhuru na amani ya kuishi katika maeneo ya mkoa huo.
Amesema kutokuwa na elimu ya kutosha ni miongoni mwa sababu zinazochangia watu kuendelea na vitendo vya ushirikina.
“Kuwatisha watu kuwa watawaua kunasababisha uvunjifu wa haki na si sayansi kama wanavyodai wahusika wa vitendo hivyo,” amesema Magoti.
Hata hivyo amesema kuna mtazamo potofu kutoka kwa baadhi ya watu serikalini wakiamini kuwa taasisi hiyo imejiingiza katika siasa na kuwashawishi wananchi waache kutekeleza sheria za nchi na kupingana na uongozi uliopo madarakani.
Amesema LHRC imejikita katika haki za kijamii ikiwemo haki ya kuishi, haki ya kumiliki mali, haki ya kuabudu mahali popote na haki ya kifamilia.
Pia alisisitiza kuwa kazi yao ni kuwatembelea wananchi waishio vijijini ili kutoa msaada wa kisheria na kuwapa elimu kuhusu haki zao bila kubughudhiwa na mtu yeyote.
Magoti amesema licha ya LHRC kutetea haki za binadamu kwa kuwapa mwongozo wa kisheria kuna changamoto mbalimbali zinazokikumba kituo hicho.
Amesema kwa sasa wanakabiliwa na ukosefu wa fedha na vyombo vya usafiri kwa ajili ya kuwawezesha kufanya ziara zao vijijini ili kuonana na watu waliokosa haki zao na wanaohitaji mwongozo wa kisheria.
Amesema kuwa ili waweze kutatua changamoto hizo wanakusudia kushirikiana na vyombo vya habari kuwaelimisha wananchi kuhusu kazi zote zinazoendeshwa na kituo hicho.
Naye Hussein Shafii (23), mkazi wa Mwenge jijini Dar es Salaam akizungumza na Gazeti la JAMHURI amesema serikali inanufaika kwa namna moja ama nyingine na kituo hicho.
Shafii amesema LHRC inaisaidia serikali kulinda, kutetea haki za binadamu na kuwadhibiti wale wanaovunja haki hizo.
“Kwa hiyo serikali inasaidiwa na kituo hiki ingawa ni shirika lisilo la kiserikali, hivyo inapaswa kukisaidia badala ya kukituhumu kuwa kinajihusisha na siasa,” amesema.
Kituo hicho kilianzishwa mwaka 1995 kwa dhumuni la kutetea na kulinda haki za binadamu kwa mujibu wa sheria za nchi.
- Mwisho