Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Dunia na vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Kipekee alituumba sisi wanadamu tumiliki na kuvitawala vyote: majini, nchi kavu na angani.
Ndiyo maana baadhi ya mataifa yenye nguvu kiuchumi yanathubutu kwenda kuchunguza nini kilichopo katika anga za mbali. Harakati zote hizo ni katika kutafuta kumiliki na kutawala: wamefika kwenye mwezi wakaona nini kinajiri huko. Bado wanakazana kufika kwenye sayari nyingine kama Mars na Jupiter.
Hakika Mungu ni mwenye nguvu na wa ajabu sana. Kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu alipomuumba binadamu na akamuweka duniani kuwa mmiliki na mtawala wa vyote vilivyomo; alihakikisha binadamu ataendelea kuishi kwa kuvuta gesi safi ya oksijeni (oxygen [O2]) na kutoa gesi ukaa (carbon dioxide-[CO2]). Huo ndio msingi wa uhai wetu kupitia kupumua na mengine yakifuata (chakula, mavazi, nyumba na kadhalika).
Kisayansi tunafahamu kuwa gesi aina ya nitrogen inachukua sehemu kubwa katika hewa kwa asilimia 78 wakati oksijeni ni karibu asilia 21 ya gesi zote angani. Vilevile, kuna gesi aina ya argon kwa asilimia 0.93 na gesiukaa (CO2) asilimia 0.04, lakini pia kuna vigesi vingine pamoja na unyevunyevu (water vapour) kwa asilimia 0.03.
Kadhalika, Mwenyezi Mungu aliweka misitu na mimea mbalimbali kwa makusudi ili tuendelee kupata oksijeni ya kutosha na wakati huo huo gesiukaa ikibakia kwenye viwango visivyoleta madhara kwa binadamu na wanyama wengine.
Hali hiyo inamaanisha nini kwetu sisi binadamu? Kiuhalisia misitu, miti na mimea mingine juu ya ardhi na ndani ya maji (aquatic plants and other living organisms) ndiyo mitambo asilia ya kutengeneza oksijeni na kufyonza gesiukaa kuitoa angani na kuihifadhi kwa usalama wetu.
Misitu, miti na mimea huota na kukua na katika kufanya hivyo kunahitajika maji na virutubisho vinavyopatikana kwenye udongo, lakini pia kuwapo gesiukaa na nguvu ya jua. Katika mchakato huo ndipo gesiukaa, ambayo ikiachiwa ikaongezeka sana kwenye mfumo mzima wa hewa angani, inasababisha madhara kwetu sisi binadamu, lakini pia kwa viumbehai wengine kutokana na kuongezeka joto duniani na hivyo kusababisha mabadiliko ya tabianchi (temperature rise and climate change). Kimsingi, gesiukaa inatumiwa na mimea katika mchakato wa kutayarisha chakula kwa mchanganyiko wa maji na virutumisho vingine (kutoka kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha) na kwa msaada wa nguvu ya jua hutengeneza chakula kinachohitajika kwa miti na mimea kukua. Ni katika utaratibu huo unaowezesha misitu, miti na mimea kutoa (release) gesi aina ya oksijeni na kuiongeza kwenye mfumo wa hewa angani.
Kwa maneno mengine: misitu, miti na mimea mingine juu ya nchi na majini; hutusaidia kuondoa gesiukaa hewani na kuingiza gesi safi ya oksijeni ambayo tunahitaji sana kwa uhai na maisha yetu wa kila situ.
Iwapo Mwenyezi Mungu aliumba dunia tunamoishi akaweka kiwango cha gesiukaa cha chini sana kiasi cha kutoleta madhara kwa binadamu na viumbe wengine, je, ongezeko la gesiukaa (zaidi ya asilimia 0.04) kwenye mfumo wa hewa angani linasababishwa na nini?
Kusema kweli dunia sasa imesheheni watu wengi zaidi ya bilioni saba; na China ikiwa na zaidi ya watu bilioni 1.4 wakati India ikiwa na zaidi ya bilioni 1.3. Bara la Afrika sasa lina watu zaidi ya bilioni 1.3. Kutokana na ongezeko kubwa la binadamu duniani pamoja na kiu ya kujitafutia maendeleo; shughuli nyingi kupitia mikono ya binadamu zikasababisha kuzalisha gesiukaa nyingi kupita kiasi. Isitoshe, dunia imeendelea kupoteza misitu ya asili kwa kasi kubwa kutokana na shaughuli za kilimo au ufugaji zisizo endelevu na pia kuchoma moto misitu na mapori kiholela. Shughuli za viwandani na nyumbani na katika maeneo ya biashara ikiwa ni pamoja na masuala ya usafiri hasa katika majiji na miji zimeshamiri sana na kusababisha ongezeko kubwa la gesiukaa angani.
Kwa majiji kama Dar es Salaam ambayo yana idadi kubwa ya watu na hali ya mazingira yake kuchafuliwa na gesiukaa na aina nyingine za gesi kama methane,ethanol na nyinginezo; kutokana na shughuli za viwandani, nyumbani na usafirishaji: kunahitajika “mapafu” ya kutusaidia kupumua vizuri. Mathalani, kama kutakuwapo miti mingi na maeneo yenye misitu iliyohifadhiwa ipasavyo katika Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake; hali hiyo itasaida kuleta unafuu kwenye mfumo wa gesi angani.
Kwa miaka ya karibuni jiji hilo limekuwa na magari mengi yanayotumia muda mrefu barabarani kutokana na foleni kupita kiasi. Hali hiyo imekuwa chanzo kikubwa cha kuchafua mazingira (environmental pollution). Madhara yake ni makubwa hasa kiafya kwa sababu ya kuendelea kuvuta gesi zilizofaa kwa uhai wa binadamu na viumbe wengine.
Kwa kuwapo misitu na kupanda miti ya kutosha kwenye sehemu tunazoishi (urban tree planting) na kutunza maeneo yenye misitu ya asili, kutasaidia kupunguza gesiukaa kwa manufaa ya afya zetu.
Kwa kuzingatia hilo, taasisi isiyo ya serikali ya Uhifadhi na Utunzaji wa Maliasili na Mazingira (Wildlife Conservation Society of Tanzania-WCST); inatoa mwito kwa wadau, taasisi binafsi na za umma, mashirika na wadau wetu katika maendeleo kuwa wakati ni sasa wa kuchukua hatua za kimkakati kuhakikisha kunakuwapo na Dar es Salaam ya kijani yenye maeneo ya misitu ya asili itakayokuwa ni mapafu ya jiji.
Manispaa zote ziweke mpango mahususi kuwezesha kila anayepewa kiwanja apande miti miwili, mitatu au zaidi katika eneo lake. Wataalamu wa misitu, kilimo na mazingira washauri ni aina gani za miti zinazofaa kwa mazingira ya Dar es Salaam. Angalizo ni kupata miti mizuri (ornamental trees) pamoja na kufyonza gesiukaa na kutupatia oksijeni, iweze kutoa kivuli kwa ajili ya kuboresha hali ya mahali (ameliorate microclimate) hasa nyakati za jua kali.
Vilevile, miti ya matunda itafaa sana kuongeza lishe kupitia matunda pia kuboresha mazingira.
Pamoja na kupanda miti, tujitahidi kusimamia na kutunza maeneo yenye misitu ya asili kama Pugu na Kazimzumbwi, Vikindu na Pande ili maeneo hayo yawe kichocheo cha kupunguza gesiukaa kwenye anga la Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake na wakati huo huo kuendelea kutoa gesi ya oksijeni kuboresha afya zetu.
Nichukue fursa hii kuwaomba wadau wote, hususani Marafiki wa Pugu na Kazimzumbwi “Friends of Pugu & Kazimzumbwi” kwa pamoja tuhakikishe maeneo hayo yaliyohifadhiwa kisheria tangu mwaka 1954 yanaendela kuwanufaisha wakazi wa Dar es Salaam na maeneo jirani. Hakuna lisilowezekana; tutimize wajibu wetu na penye nia pana njia – tutafanikiwa Mwenyezi Mungu atusaidie.
Mwandishi wa makala hii, Dk. Felician Kilahama, ni Mwenyekiti wa WCST; na pia ni Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Anapatikana kwa simu: 0783007400